NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema serikali itahakikisha inashirikiana vyema na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) katika kuendeleza misingi ya dini ya kiislamu.

Dk. Hussein Mwinyi alieleza hayo jana wakati alipofanya mazungumzo na wajumbe wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar wakiongozwa na kaimu katibu wa jumuiya hiyo Sheikh Ali Abdalla  Amour.

Alisema kuwa miongoni mwa mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika kuendeleza misingi ya dini ya kiislamu ni umoja, amani na mshikamano.

Alieleza kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar kumetoa nafasi  ya kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa viongozi, wananchi na kuamsha ari ya kushirikiana.

Alisema kuwa hatua hiyo, imesaidia kuweka pembeni kasoro zilizokuwepo hapo awali, ambapo maridhiano hayo yataongeza kasi ya maendeleo nchini.

Dk. Mwinyi alieleza kuwa kasi ya kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia itaongezwa ili kuliondoa tatizo hilo lililokithiri katika jamii na kwamba viongozi wa dini wanapaswa kusaidia vita hivyo.

Aidha Dk. Mwinyi alieleza haja ya kutafutiwa ufumbuzi changamoto za hijja huku akieleza umuhimu wa kuwepo mfuko wa hijja ambao umezinufaisha nchi nyingi duniani ambazo zimeuanzisha.

Dk. Mwinyi alieleza umuhimu wa kuwekwa kwa utaratibu maalum kwa ajili ya walimu wa madrasa ikiwa ni pamoja na kuwepo miongozo ya utoaji elimu ya madrasa kwa mashirikiano ya viongozi wa dini, serikali kupitia Wizara ya Elimu, Ofisi ya Mufti na wadau wengine.

Nao wajumbe wa JUWAZA, walimpongeza Dk.Mwinyi kwa kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar na kuweza kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha alipongeza kasi aliyoanza nayo katika kuwaletea maendeleo wananchi ikiwa ni pamoja na kuona umuhimu wa kuwepo amani, umoja na mshikamano katika jamii na kuamua kusimamia maridhiano.

Walieleza kuwa hatua zake za kurudisha mshikamano nchini na kuleta umoja ni jambo kubwa na la kuungwa mkono na kupongezwa  kwani bila ya kuwepo amani, umoja na mshikamano maendeleo hayawezi kupatikana.

Uongozi huo pia, ulieleza changamoto zilizopo katika utekelezaji wa safari za hijja, haja ya kuwepo mfuko wa hijja, benki za kiislamu na  utaratibu wa kuwasaidia walimu wa madrasa kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika jamii.

Wajumbe wengine wa JUMAZA waliofika ikulu ni pamoja na Dk. Mohammed Hafidh Khalfan, Sheikh Masoud Hemed Nassor, Sheikh Yussuf Khamis, Sheikh Abdalla  Issa Makame, Sheikh Muhiddin Zubeir Muhiddin na Ukhti Halima Qasim Mohammed.