NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi jana aliongoza kikao cha kwanza cha baraza la Mapinduzi kilichofanyika ikulu mjini hapa.

Dk. Mwinyi aliongoza kikao hicho cha kwanza cha serikali ya awamu ya nane iliyoingia madarakani hivi karibuni kufuatia kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka mwaka huu.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Baraza la Mapinduzi uliopo ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na wajumbe wa baraza hilo.

Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla.

Wengine waliohudhuria ni pamoja na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, mawaziri, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dk. Mwinyi Talib Haji.

Dk. Mwinyi, alikifungua kikao hicho na kukiongoza kama Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 45 (1) inavyomtaka, ambapo  kikao hicho ni cha kwanza tokea aingie madarakani akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.