NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza juhudi zinazochukuliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuondoa changamoto za muungano.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana ikulu jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo kati yake na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Ummy Mwalimu.

Alitumia fursa hiyo kupongeza hatua zinazochukuliwa katika kutatua changamoto hizo na kueleza matumaini yake kwamba jitihada hizo zitaleta mafanikio kwa pande zote mbili.

Alisema kuwa mategemeo yake ni kupatiwa ufumbuzi wa changamoto hizo na kueleza kwamba yale yanayohitaji kupatiwa ufumbuzi kwenye ngazi ya juu wapo tayari kuyafanyia kazi.

Kwa upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Maziringira, Ummy Mwalimu alitumia fursa hiyo kwa kumpongeza Dk.  Mwinyi kwa kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Ummy ambaye alifuatana na mkurugenzi wa muungano, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk alieleza matumaini kwamba Zanzibar itafika mbali na kupata mafanikio chini ya uongozi wa Dk. Mwinyi.

Waziri Ummy alimueleza Dk. Mwinyi juhudi zinazoendelea kuchukuliwa katika kuzipatia ufumbuzi changamoto za muungano ambazo kwa kiasi kikubwa juhudi hizo zimezaa matunda.

Aliongeza kwamba changamoto nyingi zimeshapatiwa ufumbuzi na chache zilizobaki utekelezaji wake unatarajiwa kufanyika katika vikao vitakavyokutana hivi karibuni.

 Sambamba na hayo, waziri Ummy Mwalimu alieleza azma ya kukaa kikao cha kamati  ya pamoja ya serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa kuondoa changamoto zilizobaki.

Naye waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Mohammed Salum alisema kuwa mbali ya waziri Ummy kuja kujitambulisha kwa rais pia, waziri huyo anatarajia kufanya ziara katika miradi ya Maendeleo ya Jamii (TASAF) pamoja na miradi ya miundombinu ya masoko, uongezaji thamani na huduma za kifedha vijini (MIVAP).

Mnamo Oktoba 17 mwaka huu 2020, SMT na SMZ zilisaini hati za makubaliano ya kuondoa hoja tano za changamoto zilizopatiwa ufumbuzi ambapo nyengine sita zinasubiri kupatiwa ridhaa ya kikao cha kamati ya pamoja.