NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema viongozi wa umma watakaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili, watasimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi.

Dk. Mwinyi alisema hayo jana katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakili Kikwajuni jijini hapa, wakati alipozungumza na viongozi, watendaji na watumishi wa umma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu.

Alisema mara baada ya kuingia madarakani, serikali imeanza kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wasiowajibika na wasioshikamana na maadili ya kazi zao, kufuatia ziara zilizofanyika katika taasisi mbali mbali, ikiwemo Bandari, Hospitali ya Mnazi Mmoja na maeneo mengine yaliyomo katika mpango wa utekelezaji wa mradi wa kuendeleza huduma Mjini (ZUSP).

Alisisitiza na kurejea maelezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti dhidi ya watendaji wanaotiliwa shaka ya kuhusika na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili, kuwa serikali itakabiliana ipasavyo na vitendo hivyo vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Alisema amefurahishwa na hatua ya wananchi ya kuiunga mkono serikali na kubainisha kuwa yeyote atakaetuhumiwa na hatimae kutokutikana na kosa, atarejeshwa kazini na kupata haki zake kama sheria zinavyoelekeza.

“Kiongozi wa umma lazima afanye kila linalowezekana kuwa mfano na kigezo cha tabia njema na ajiepushe hata na vitendo vinavyoweza kumfanya atiliwe shaka”, alisema.

Dk. Mwinyi alisema ni jambo la kusikitisha kuona taarifa iliyowasilishwa kwake kutoka ZAECA, kuonyesha kuwepo tatizo kubwa la ubadhirifu wa mali za serikali na wizi katika utekelezaji wa miradi mikubwa.

Hata hivyo alisema amefurahishwa na kazi inayoendelea ya ufuatiliaji, hivyo akawataka viongozi wote watakaotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu huo kutoa ushirikiano wa kisheria kwa chombo hicho.

“Nimevutiwa sana na ari na utayari wa watendaji wa ZAECA katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, tutayazingatia maombi yao waliyotueleza”, alisema.

Aidha, alisema anatambua hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kuwa hazitowafurahisha watu wote, hivyo akawataka wananchi kuikubali hali hiyo kwa msingi kuwa wengi wataguswa, akibainisha nchi kugubikwa na muhali.

Alipongeza kazi kubwa iliyofanywa na awamu zote za serikali zilizotangulia ya kuunda taasisi na kutunga sheria zilizo bora katika kufanikisha dhana ya uimarishaji utawala bora.

Alisema ni jambo lisilokubalika fedha nyingi za serikali zinapotea huku Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Serikali ipo kimya ikiwa na majengo na vifaa vya kisasa pamoja na watendaji wa kutosha.

“Halitokuwa jambo la maana hata kidogo kuwepo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka yenye kulalamikiwa na kuonekana kikwazo katika kutafuta ushahidi wa kesi mbali mbali”, alisema.

Aidha, Dk. Mwinyi alisema serikali imeunda Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kuhakikisha viongozi wote wa umma waliotajwa na sheria ya maadili (Namba 4 ya mwaka 2015) wanajaza na kuwasilisha fomu ya tamko la rasilimali na madeni.

Alichukua fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wote waliotajwa chini ya sheria hiyo; kwa mujibu wa vyeo na nafasi zao kuhakikisha wanajaza fomu hizo sio zaidi ya Disemba 30 mwaka huu na kuzirejesha Ofisi ya Tume ya Maadili kwa wakati uliowekwa na sheria.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman, alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar katika kuimarisha Utawala Bora pamoja na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya Rushwa.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Asaa Ahmada Rashid, alisema maadhimisho hayo ni muhimu kwani yanaongeza uelewa kwa wananchi juu ya dhana ya utawala bora na misingi yake.

Alisema kuimarika kwa misingi hiyo kutaisaidia jamii kuzitambua na kupata haki za msingi ili kuendeleza ustawi wa maisha yao, kupunguza umasikini pamoja na kukuza uchumi.

Alisema kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utendaji wa taasisi hizo, ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa maadili kwa viongozi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu, matumzii mabaya ya fedha na rasilimali za umma.