NA MADINA ISSA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa msaada wa vyakula kwa watoto yatima wanaoishi kijiji cha kulelea watoto S.O.S na nyumba ya kulelea watoto Mazizini kwa ajili ya kusheherekea sikukuu ya Krimas na mwaka mpya.

Akikabidhi vyakula hivyo, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Mkurugenzi huduma za Rais, Ameir Ali Khatib, alisema kuwa msaada huo utawasaidia kwa ajili ya siku hiyo na kujifariji kama watoto wenzao.

Alisema kuwa katika chakula hicho Rais, alipenda kuwa nao ila kutokana na kutingwa na kazi za kiserikali hatokuwepo na kusema kuwa atakuwa yupo pamoja nao.

Hata hivyo, aliahidi msaada huo hautokuwa mwisho na kuendelea kuwapelekea pale inapohitajika kupatiwa vituo hivyo.

Wakipokea msaada huo wasimamizi wa watoto hao, walimshukuru Dk. Mwinyi kwa msaada wake waliopatiwa na kuahidi kutuumia kama ulivyokusudiwa kwa manufaa ya watoto wao.

Sambamba hayo, walisema kuwa wamefarajika na walichopewa na kusema kuwa wameona wazi kuwa dk Mwinyi ndio tumaini la watoto hasa waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu.

“Kwa kweli tumeona tumaini letu kwa Rais wa Zanzibar Dk. Mwinyi ambapo anaonesha wazi kuwa na nia ya kuleta maendeleo katika nchi wakiwemo watoto wanaishi katika mazingira magumu”, alisema Asha.

Nae, Naibu Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Mwanajuma Majid Abdallah, alitoa shukrani kwa niaba ya Serikali, alimshukuru Dk. Mwinyi kwa mwanzo mzuri kwa kutoa msaada wa watoto hao kwani ameonesha kuwajali na kuwathamini ambapo watoto hao wamefarajika na msaada huo.

Nae Mkurugenzi wazee na Ustawi wa Jamii, Wahida Maabadi, alisema msaada huo inaonesha wazi kuwa Dk. Mwinyi anaendeleza utekelezaji wa ahadi zake alizoziahidi kwa wananchi wakati wa kuomba ridhaa ya kuwa karibu na makundi yote ikiwemo ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima.

Sambamba na hayo, alisema kuwa amepokea kwa moyo mkunjufu msaada huo na kuufikisha kwa walengwa kwa wakati uliopo.