Asimamisha kazi watuhumiwa wa ufisadi

Aichonga meno, aipa majukumu ZAECA

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amemsimamisha kazi Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sabra Issa Machano na watendaji wengine wakihusishwa na tuhuma mbalimbali.

Dk. Mwinyi alitoa kauli ya kuwasimamisha watendaji hao jana wakati alipozungumza na watendaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) katika ukumbi wa taasisi hiyo uliopo Victoria Garden.

Watendaji wengine waliohusika na hatua ya kusimamishwa kazi na kupisha uchunguzi dhidi yao ni Ramadhani Abdalla Ali na waratibu wote wa mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kutoka wizara ya Fedha.

Alisema amechukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Mkurugenzi ZSSF na Ramadhani Abdalla Ali kwa makosa ya kiutendaji katika ukarabati wa jumba la Treni liliopo Darajani.  

Alisema ni dhahiri kuwa katika utekelezaji wa mradi huo taratibu zilikiukwa na hivyo akabinisha ulazima wa kufanyika uchunguzi, wakati ambapo watendaji hao wakiwa nje ya kazi.

Alisema makosa dhidi yao hayatoi fursa ya wao kuendelea na kazi, hivyo ni vyema wakae pembeni kupisha uchunguzi na kusema serikali itasimamia haki na kamwe hakuna mfanyakazi atakaeonewa.

Aidha, alisema hafurahishwi na utekelezaji wa mradi wa ZUSP uliogharimu dola milioni 93, ambao ulikusudiwa kuondoa changamoto mbali mbali katika manispaa.

Alisema taarifa zilizopo zinaonyesha kuwepo makosa makubwa katika manunuzi pamoja na kufanyika udanganyifu juu ya kazi zilizoelezwa kufanyika, il-hali hazikufanyika.

Alisema amelazimika kuisimamisha kamati nzima ya uratibu wa mradi huo ili uchunguzi uweze kufanyika, wakati wafanyakazi hao wakiwa nje ya kazi zao.

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi aliagiza ZAECA kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya mfanyakazi wa TRA, Karama Awadha Karama anaetuhumiwa kushusha kiwango cha kodi katika tukio la kuingizwa bandarini kichwa cha Scania, sambamba na kampuni ya KEVIS aliyoaguiza ifanyiwe uchunguzi.

Alisema mfanyakazi huyo alijenga dhamira ya kujihusisha na rushwa, ambapo kwa nyakati tofauti aliteremsha kiwango cha kodi hiyo hadi kufikia shilingi milioni tano, fedha ambazo haziendani na thamani halisi ya kodi iliyopaswa kulipwa, ambapo hatimae gari hilo lilitolewa usiku bila fedha hizo kulipwa.

Alisema anasikitishwa na miradi mikubwa jinsi ilivyogubikwa na matatizo makubwa kiasi ambacho haionyeshi thamani ya fedha zilizotumika na hivyo akaahidi kuchukua hatua mara moja dhida ya wote waliokiuka kanuni za manunuzi.

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi alisema tangu serikali ya awamu ya nane iingie madarakani imebaini kuwepo matatizo makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, na hivyo akasisitiza dhamira ya Serikali ya kuchukua hatua madhubuti.

Aidha, alisema kuna miradi mingine inayoonesha dalili za kuwepo mianya ya rushwa na hivyo akaahidi kuifuatilia pamoja na kuhakikishia ZAECA kuwa serikali imefungua ukurasa mpya wa mapambano dhidi ya rushwa.

Mapema Waziri wa Nchi (OR) Katiba, sheria, utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema kuna mashirikiano makubwa ya kiutendaji kati ya ZAECA na wenzao wa Tanzania Bara (TAKUKURU) kutokana na vikao mbali mbali vilivyofanyika, na hivyo akaahidi kuendeleza mshirikiano hayo kwa lengo la kudumisha Muungano.

Nae, Mkurugenzi Mkuu ZAECA, Mussa Haji Ali alisema pamoja na taasisi hiyo kuasisiwa katika kipindi kifupi kilichopita, imeweza kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake makuu matatu.

Akigusia uchunguzi wa miradi mikubwa inayotokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya serikali, alisema ZAECA inaendelea kufanya uchunguzi katika miradi mbali mbali ikiwemo wa Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri na ukarabati wa jengo la treni ambayo imebainika kuwepo harufu za rushwa.

Alisema miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi ni Barabara ya Bububu – Mkokotoni Kaskazini Unguja pamoja na ile ya Ole – Kengeja inayoonekana kuwepo harufu ya rushwa katika suala la tathmini.

Aidha, aliitaja miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi kwa tuhma za kuwepo mianya ya rushwa, kuwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Amali Vitongoji, Bandari ya Mangapwani, Soko la Matunda Kangani, Ujenzi wa kiwanda cha ushoni cha Idara Maalum,  mradi wa kuendeleza vijana, ujenzi wa vituo vya Zimamoto Pemba, Kuimarisha majengo ya JKU Mtoni, Matengenezo kambi ya KVZ Pemba pamoja  Chuo cha Mafunzo Wete.