NA TATU MAKAME

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK. Hussein Ali Mwinyi, leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha la Asasi za Kiraia Zanzibar litakalofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni mjini hapa.

Tamasha hilo la siku mbili linaloandaliwa na mwamvuli wa asasi za kiraia Zanzibar (ANGOZA) ni la 14 na linatarajiwa kushirikisha wadau 110 kutoka taasisi mbalimbali za serikali na binafsi.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari ofisini kwake Mombasa, wilaya ya Magharibi ‘B’, Mwenyekiti wa ANGOZA, Asha Aboud Mzee, alisema tamasha hilo linadhaminiwa na ‘The Foundation for Civil Society (FCS)’ na kwamba mada tano zitawasilishwa.

Alieleza kwamba miongoni mwa mada hizo ni mchango wa asasi za kiraia katika maendeleo  ya Zanzibar, maono ya sekta ya kiraia juu ya mswaada wa sheria ya asasi za kiraia Zanzibar pamoja na mada ya uwajibikaji.

Mada nyengine mapitio ya dira ya maendeleo ya Zanzibar ya 2020/2050 kama  nguzo ya uchumi wa Zanzibar na mchango wa asasi za kiraia kwenye dira  hiyo pamoja na muundo wa kitaasisi kusimamia asasi za kiraia Zanzibar.

Pamoja na uwasilishaji wa mada hizo, tamasha hilo litaambatana na maonesho ya kazi na shughuli za baadhi ya asasi za kiraia ili kuonesha mafanikio waliyoyapata na changamoto walizokutana nazo.

Akizungumzia tamasha la mwaka uliopita, Mwenyekiti huyo alisema lilijenga hoja juu ya ushiriki wa asasi za kiraia katika kutumia haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi kupitia uchaguzi mkuu.

“Kupitia hoja hiyo, kuna asasi za kiraia zilipata fursa ya kutoa elimu ya mpiga kura na kushirikishwa katika utayarishaji wa dira ya maendeleo ya Zanzibar ya 2020 – 2050 ambayo ni muhimu katika maendeleo ya nchi yetu,” alisema Asha.

Mapema Mkurugenzi wa ANGOZA Hassan Khamis Juma, alifafanua kuwa waandishi wa habari wameisaidia serikali kuchochea maendeleo ya nchi kama ilivyo katika mafanikio ya Mwamvuli huo na asasi za kiraia.

Hivyo alihimiza kuwepo kwa mahusiano ya karibu kati ya pande mbili hizo na kwamba wanategemea kuzijengea uwezo asasi za kiraia ili zifanye kazi zake vizuri na kuongeza mafanikio kwa jamii.