Asema yaimarisha amani, kuleta maendeleo

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa ili iwaletee maendeleo.

Dk. Hussein alisema hayo jana huko masjid Jibril, Mkunazini mjini  Zanzibar wakati akitoa salamu kwa waumini wa dini ya kiislamu mara baada ya kumaliza sala ya Ijumaa.

Alieleza kuwa serikali ya Umoja wa Kitaifa imeshaundwa na viongozi wamekubaliana kuweka tofauti zao kando ili kuwaunganisha wananchi wote wa Unguja na Pemba bila ya kujali imani za kidini itikadi zao za kisiasa na wamekubali kuwa wamoja kwa azma ya kuijenga nchi yao.

Alisema kuwa Mwenyezi Mungu amekubali dua za waumini na  vyama vimekubali kushirikiana kwani ilifikia wakati wa uchaguzi watu wanapoteza amani, wanafarakana, mume anamuacha mke kwa sababu za itikadi za kisiasa, watu hawazikani, hawasali pamoja mambo ambayo ni kinyume na maamrisho ya dini ya Kiislamu.

Aidha, alisema kuwa dini ya kiislamu inawataka watu wote wawe wamoja, washikamane, wapendane na kuwaomba waumini kwamba serikali ya Umoja wa Kitaifa iachwe ifanye kazi ya kuleta maendeleo na isiwe na kazi ya kuwaunganisha watu kwa mifarakano yao.

Alisema kuwa si wote waliofurahia maridhiano hayo, lakini bado kuna nafasi ya kuwaelimisha watu na kusema kuwa dini ya kiislamu inawataka watu kuwa wamoja hivyo, watu wote wenye kinyongo wawe kitu kimoja katika kuijenga nchi.

Aliongeza kuwa, umoja wa kitaifa unahitajika na tayari umeshapatikana katika ngazi za juu ya kujenga serikali lakini pia, unahitajika kupatikana kwa wananchi wote ili kuweza kutimiza majukumu yaliyo mbele.

Dk. Mwinyi alisema kuwa hivi sasa kuna kila dalili ya maridhiano baina ya wananchi na kumuomba Mwenyezi Mungu kuwawezesha wananchi wote wawe kitu kimoja ili waweze kujiletea maendeleo na mafanikio makubwa katika nchi yao.

Dk. Mwinyi alikwenda msikitini hapo akiwa mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi na kupewa fursa ya kuzungumza ambapo aliwaomba Waumini kuhakikisha amani iliyopo inalindwa  wakati wote wa uchaguzi.

Alisema kuwa Mwenyezi Mungu amekubali dua za waumini hao na kupelekea nchi kuwa na amani na utulivu wakati wote sambamba na kuendelea kuwepo hadi hivi leo kwani yote yaliyoahidiwa wakati wa kampeni hayatekelezeki bila ya kuwepo kwa amani na umoja baina ya wananchi.

Alisema kuwa baada ya amani kuwepo kinachotakiwa hivi sasa ni umoja, mshikamano, maelewano, maridhiano na mapenzi miongoni mwa wananchi wote kwani ndivyo dini ya Kiislamu inavyosisitiza.

Alisema kuwa ushirikiano ni lazima katika kupambana na madhila hayo ambapo kwa upande wa kadhia ya udhalilishaji jambo hilo ni rahisi kupambana nalo kwani wanaofanya vitendo hivyo wamo katika jamii lakini kuna kila aina ya kufifisha ili wanaohusika wasifikishwe katika vyombo vya sheria.

Maeneo mengine ambapo kesi zinafifishwa alieleza kuwa ni katika vituo vya polisi, utaratibu wa kisheria ambapo pia katika jamii wamekuwa wanawaficha na wamo wanaopatana na wadhalilishaji ambao hulipwa fedha ili wanyamaze huku akisisitiza kwamba ni lazima madhila hayo yaondoke.

Aliushukuru uongozi wa masjid Jibril na kuwaahidi waumini wa dini ya kiislamu kwamba kazi yake kubwa itakuwa ni kuwaunganisha wananchi wote wa Zanzibar  ili lao liwe moja.