NA ABOUD MAHMOUD

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho wa siku ya maadili na haki za binadamu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma Zanzibar, Asaa Hamad Rashid kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, alisema maadhimisho hayo yatafanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.

Alieleza kuwa maadhimisho hayo yanayoadhimishwa kimataifa Disemba 10 kila mwaka, yana lengo la kuungana na mataifa mengine duniani katika mapambano dhidi ya rushwa na haki za binadamu.

“Kila ifikapo Disemba 10 ya kila mwaka, Tanzania huadhimisha siku hiyo pamoja na mataifa mengine lakini kutokana na sababu mbali mbali Zanzibar ilishindwa kufanya shughuli hiyo katika kipindi hicho na kuisogeza mbele,” alisema Mwenyekiti huyo.

Aliongeza kuwa katika maadhimisho hayo, taasisi zinazohusika na usimamizi wa haki za binadamu ikiwemo Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Idara ya Utawala Bora na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora kwa pamoja hufanya shughuli mbali mbali ikiwemo kuratibu matukio yenye mnasaba na uimarishaji wa maadili na utawala bora nchini.

“Katika maadhimisho ya siku hii adhimu, taasisi hizi zimefanya shughuli mbali mbali ikiwemo utoaji elimu kwa kuandaa na kurusha vipindi kupitia vyombo mbali mbali na kuandaa mikutano na makongamano ya utoaji elimu,” alifafanua.

Aidha alifahamisha kwamba maadhimisho wa mwaka huu yamekuja na ujumbe mahususi unaosema ‘ Tuimarishe utoaji wa huduma za jamii kwa kuzingatia kuheshimu haki za binadamu na mapambano dhidi ya rushwa’.