Akitaka kijikite kwenye tafiti zenye tija

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kupambana na rushwa, ubadhilifu na uzembe katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Dk. Mwinyi aliyasema hayo jana katika hotuba aliyoitoa kwenye mahafali ya 16 ya SUZA mara baada ya kutawazwa kuwa mkuu wa chuo hicho, hafla iliyofanyika katika kampasi ya chuo hicho iliyopo Tunguu.

Alisema akiwa mkuu wa SUZA atafuatilia kwa karibu makusanyo, ruzuku kutoka serikalini kutoka kwa wahisani, matumizi ya thamani ya vitu vinavyonunuliwa na vyanzo mbalimbali vya mapato vya chuo hicho.

Aliutaka uongozi wa chuo hicho kusimamia vizuri, kwa umakini na uadilifu rasilimali za chuo, watunze nyaraka zenye kuonesha mali zinazomilikiwa na chuo zikiwemo hati miliki za ardhi, nyumba na majengo.

Aliwataka wahadhiri na wafanyakazi kuekeleza majukumu yao kwa bidii, nidhamu, kuzingatia sheria na maadili yanayoongoza na kujiongeza kitaaluma.

Alisema rais mstaafu wa awamu ya saba, Dk. Ali Mohamed Shein ameonesha njia kwamba chuo hicho ni miliki ya watu wa Zanzibar na kinaendeshwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo ni lazima kifundishe masomo yanayoendana na mahitaji ya wananchi kiuchumi na kijamii.

Dk. Mwinyi aliitaka SUZA kuwa mfano wa chuo chenye mitaala na programu za ufundishaji zinazozingatia mahitaji sera za nchi na mipango ya maendeleo.

Alieleza kuwa SUZA ina kazi kubwa ya kufundisha wataalamu wa kutosha wanaohitajika kusimamia uchumi wa buluu.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kumkabidhi chuo kikiwa kimepiga hatua kubwa za maendeleo katika kipindi cha miaka 10 cha uongozi wake.

Aidha alikitaka chuo hicho kuandaa utaratibu wa kufanya tafiti na kuweka mkazo wa matumizi ya tafiti katika maeneo yanayohusu uchumi wa buluu na sekta nyengine za uchumi.

Alieleza kuwa ni kazi ya SUZA, kwa kushirikiana na taasisi nyengine za elimu ya juu kufanya tathmini ya tafiti zilizofanywa ndani ya kipindi cha 2015-2020 na uhalisia wa tafiti hizo kwa mahitaji ya nchi.

Alisema Zanzibar ina haja ya kuwa na ajenda mpya ya utafiti wa kitaifa na kusisitiza kuachana na tabia ya kutegemea wahisani hata katika mambo muhimu ya maendeleo yanayoweza kufanywa na wazanzibari wenyewe.

Alieleza kuvutiwa na dhamira ya kuifanya SUZA kuwa ni Oxford ya Kiswahili na iwe chimbuko la wataalamu, waandishi na malenga wa mashairi na kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA), iwe ni kitovu cha kutoa Kamusi zinazopendwa na zinazoaminika katika lugha ya Kiswahili.

Aidha, aliutaka uongozi wa SUZA, kuandaa mikakati mizuri ya kulinda lahaja  za kizanzibari, kuwa wepesi, kubuni misamiati na istilahi zinazohitajika ili kuweza kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

Dk. Mwinyi alitoa kazi kwa uongozi wa SUZA kushirikiana na uongozi wa BAKIZA katika kuandaa mikakati na kufanya jitihada za kutafuta ajira za Kiswahili nje ya nchi kwa ajili ya wataalamu mbali mbali waliopo Zanzibar.

Kwa wale walioomba mikopo ya elimu ya juu na wakapata, Dk. Mwinyi aliwahimiza wawe tayari kulipa deni lililopo kwa kuzingatia sheria na makubaliano yaliyo katika mikataba waliyoijaza.

Aliwapongeza wahitimu wote na kuwataka kujiepusha na vishawishi na anasa vinavyoweza kuathiri masomo yao huku akieleza kwamba serikali itaendelea kuweka mkazo kwenye sekta ya elimu.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alimtunuku shahada ya heshima ya Udaktari wa Falsafa katika Sayansi za Tiba, Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu ya Saba, Dk. Ali Mohamed Shein na kumpongeza huku akisisitiza kwamba wananchi wa Zanzibar wataendelea kumkumbuka kwa ubunifu wake wa kuanzisha mambo mazuri ambayo watu wengi walihisi hayawezekani.

Kwa upandewa rais huyo mtaafu akitoa salamu za shukurani aliupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kumtunuku shahada hiyo ambayo itaendelea kumpa hadhi huku akieleza imani yake kwamba Dk. Mwinyi atakiendeleza vyema chuo hicho.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Simai Mohamed Said alieleza jinsi wizara yake itakavyoendelea kumuunga mkono Dk. Mwinyi pamoja na kueleza mikakati mbali mbali iliyowekwa na wizara ili iweze kuleta manufaa katika sekta ya elimu.

Mapema Makamu Mkuu wa SUZA, Dk. Zakia Mohammed Abubakar alisema kwamba chuo hicho kipo tayari kwa moyo mkunjufu kufanya kazi na yeye kwa kufuata kikamilifu ushauri na maelekezo katika kukiendeleza chuo hicho.

Makamu mkuu huyo alieleza kuwa mwaka huu chuo hicho kina wahitimu  1524 ambao Dk. Mwinyi  aliwatunuku vyeti vyao kutoka programu 56 zinazofundishwa na  chuo hicho.