Lengo ni kuwafanya watu kuwa wamoja

Na Rajab Mkasaba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi hivi karibuni aliungana na wananchi pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu katika dua maalum iliyosomwa kwa ajili ya kuiombea amani nchi pamoja na viongozi wake, dua iliyofanyika kwa nyakati tofauti Unguja na Pemba.

Kisomo cha dua hiyo kilitayarishwa na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kilianza kufanyika Unguja mnamo Disemba 10, 2020 katika Msikiti wa Mwembeshauri, Mjini Zanzibar ambapo Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alikuwa mgeni rasmi ambapo pia, viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya siasa walihudhuria wakiwemo viongozi wakuu wastaafu wa Zanzibar, Mashekhe, Maulamaa pamoja na wananchi.

Ofisi ya Mufti wa Zanzibar ambayo ilianzishwa rasmi mnamo mwaka 1992 kwa amri ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa wakati huo, Dk.Salmin Amour Juma ambayo baadae ilianzishwa upya kwa Sheria ya Mufti Namb.9 ya mwaka 2001.

Kabla ya kuanzishwa  Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar baadhi ya kazi  za msingi zilikuwa zikifanywa na Mashekhe mbali mbali wakiwemo Sheikh Hassan bin Ameir, Sheikh Fatawi bin Issa na wengineo ambao walikuwa wakitoa Fatwa mbali mbali, utatuzi wa migogoro na kutoa Miongozo kwa kadri ilivyohitajika kwa wakati huo.

Kutokana na kujua umuhimu mkubwa wa dua kwa viumbe wa Mwenyezi Mungu, wakiwemo wananchi na viongozi wao  pamoja na nchi yao, Ofisi ya Mufti wa Zanzibar iliona ipo haja ya kukaa pamoja na kupitisha kisomo hicho kilichosomwa kwa nyakati tofauti Unguja na Pemba.

kisomo hicho cha dua ambacho kilianza kusomwa katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Zanzibar na kwa upande wa kiswani Pemba kisomo kama hicho kilifanyika Mskitiki Mwintani uliopo Mtemani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba mnamo Disemba 18, 2020 na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali, Mashekhe, Maulamaa pamoja na wananchi.

Visomo hivyo, vimefanyika kwa kutambua kwamba viumbe vyote ulimwenguni vinamuhitaji Mwenyezi Mungu katika kupata manufaa yao au kuzuia madhara yasiwafikie katika  maisha yao hapa duniani na kesho siku ya mwisho.

Kama inavyofahamika kwamba kila mja anapojikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, basi huwa  anamuinua daraja na kumfanya kuwa mtukufu mbele ya viumbe vyake.

Mwenyezi Mungu anawapa mitihani viumbe vyake kwa misukosuko mbali mbali ili waweze kurudi kwa Mola wao na kuomba msaada kwake katika kupambana na mitihani hiyo.

Hivyo basi, MwenyeziMungu anapenda kuombwa msaada na waja wake na anapenda waja wake kurudi kwake pindi wanapofikwa na shida na misukosuko ya ulimwengu hasa ikizingatiwa kwamba kufanya hivyo ndio msingi wa ibada.

Kutokana na hali hiyo, ndipo Ofisi ya Mufti wa Zanzibar ikaona haja ya kuandaa kisomo hicho ambacho Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alishiriki kikamilifu kwa kutambua kwamba dua ni ibada bora mbele ya Mwenyezi Mungu kwani amewaamrisha viumbe wake wamuombe kwa lengo la la kupata kheri na kuzuia shari.

Dua ni sababu kubwa ya kupata kheri na Baraka za Mwenyezi Mungu na pia, ni sababu kubwa ya kukinga madhara na shari zote na hakika Mwenyezi Mungu ameamrisha waja wake kuomba Dua katika Aya nyingi.

Kwa mfano Mwenyezi Mungu katika Suratul Al-Ghafif: amesema kuwa “Na Mola wenu anasema; Niombeni nitakujibuni”[Al-Ghafir: 60]

Dua hutunza mapenzi ya mja kwa mola wake katika kuomba msaada wakutatuliwa matatizo ya ulimwenguni na matatizo ya Akhera, kuhakikisha ukweli wa kumuabudu Mola wa walimwengu wote ambapo kufanya hivyo ni kufungamanisha moyo wa mja na Mola wake na kumtakasia ibada zote Mwenyezi Mungu na kutotegemea mtu au kitu kingine chochote.

Aidha, kuwa na yakini kamili ya kuwa MwenyeziMungu ndie Mweza wa kila kitu, hakuna kitu kinacho mshinda, Mjuzi wa kila kitu, hakuna kitu kilicho fichika mbele ya Allah sambamba na kudhihirisha mja unyonge wake mbele ya Muumba wake na  kumhitaji Mwenyezi Mungu katika mambo yake yote kwani huo ndio ukweli wa kumuabudu Mwenyezi Mungu.

Ifahamike kwamba dua ni ubongo wa ibada, kwa sababu Dua imekusanya ibada zote, kunyenyekea, kutegemea, kutarajia, kuogopa, kuomba msaada, na mengineyo ambapo pia, dua ni ibada tukufu kushinda ibada zote na Mtume Muhammad (S.A.W), alisema katika hadidhi iliyopokelewa na Ahmad kwamba “Hakuna jambo tukufu mbele ya Allah kushinda Dua”.

Kwa kawaida viumbe wanamuhitaji Mola wao awapatie mambo ya kuwanufaisha na awaondolee mambo ya kuwadhuru ili wapate kutengenekewa na dini yao na dunia kwani mja hakosi kupata mitihani na maonjo yanayomfanya daima amhitaji Mola wake.

Hivyo, Mwenyezi Mungu amemuwekea dua na ameiwekea hiyo dua adabu na masharti pamoja na nyakati za kukubaliwa ambapo dua huwa iko karibu zaidi na kujibiwa.

Katika Sura ya Pili ya Aya ya 186 ya Suratul Al-Kashif imeonesha jinsi Mwenyezi alivyokuwa karibu na viumbe wake pale anaposema “Naitikia Maombi ya Mwombaji…”.

Inasemekana kuwa Bedui mmoja alimwendea Mtume (S.AW) na kumuuliza: “Mola wetu yuko karibu ili nimnog’oneze? au yuko mbali nimpigie kelele?” Ndipo ikateremshwa Aya hiyo kuwa ni jawabu la Bedui huyo.

Dua ni katika ibada bora na imehimizwa sana katika Qur’an na hadith kwa sababu ni dhihirisho la utumwa wa mtu kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kumhitajia.

Mnamo Disemba 10 mwaka huu 2020, Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi Alisema yeye binafsi anaamini Wazanzibari wote ni kitu kimoja wakiwa na dhamira ya kuijenga Zanzibar na hivyo akawataka viongozi wa Dini kuendelea kuwaombea dua viongozi ili waendelee kuiongoza nchi kwa ufanisi.

 “Viongozi wana dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu maridhiano yaliofanyika yameonyesha mwelekeo sahihi  wa nchi“

Alieleza kuwa pamoja na Wazanzibari kuwa na mengi ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, pia wanapaswa kuendeleza amani iliopo nchini ili kazi ya kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa iweze kufanikiwa.

Alisisitiza kwamba Viongozi wa kisiasa wana dhima kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kubainisha maridhiano ya kisiasa yaliofanyika yameonyesha njia sahihi katika kudumisha umoja na mshikamano uliopo nchini.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema hayo katika Dua maalum ya kuiombea nchi na viongozi wake amani, katika kisomo hicho maalum kilichofanyika katika Msikiti Mushawar, Muembeshauri Jijini Zanzibar.

Alisema kuna umuhimu kwa wananchi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwaongezea neema ya maridhiano yaliofanikisha uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Alisema viongozi wana dhima kubwa ya kuhakikisha wanadumisha amani na mshikamano na hivyo akatumia fursa hiyo kumpongeza Makamo wa Pili wa Rais, Maalim Seif Sharrif Hamad na Chama chake cha ACT Wazalendo kwa kukubali kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Alhaj Dk. Mwinyi alisema wakati wa kampeni za Uchaguzi mkuu uliopita alitowa ahadi nyingi sana kwa wananchi ikiwemo ile ya kusisitiza kuendeleza amani na utulivu  iliopo nchini pamoja na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha azma hiyo.

Aidha, aliwataka Wazanzibari kufanya kazi kwa bidii kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake kikamilifu mahala alipo ili kuleta ustawi wa maisha ya wananchi.

Alitoa shukurani kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa hatua zao za kumtumia pongezi kwa kuleta maridhiano na kubainisha kuwa hatua hiyo inaleta matumaini kuwa wananchi wengi wameridhia na kukubali jambo hilo.

Vile vile alisiitiza dhamira yake ya kuendelea kusimamia Umoja na mshikamano katika nchini ili kuharakisha kasi ya maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuibariki Zanzibar na  kubaki katika hali ya mani, sambamba na kuwapongeza waandaaji wa Dua hiyo kwa kuona umuhimu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupokea maombi yao , ikizingatiwa dua kama hiyo ilifanyika kabla ya Uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2020.

Mnamo Disemba 18, 2020 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi aliungana na wananchi pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu huko katika Mskitiki Mwintani uliopo Mtemani Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba kwa ajili ya kisomo maalum cha dua ya kuiombea nchi pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa kisomo hicho kilichotayarishwa na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar.

Katika maelezo yake, Alhaj Dk. Mwinyi akizungumza na Waumini waliofika msikitini hapo pamoja na wananchi wote kwa ujumla ambao walikuwa wakifuatilia kisomo hicho kupitia vyombo vya habari alisema kuwa hakuna maendeleo yoyote yanayoweza kupatikana kama nchi haina amani, umoja na mshikamano.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alitoa shukurani kwa viongozi wote waliohusika katika maandalizi ya dua hiyo na kuwashukuru Waumini na wananchi waliohudhuria kwa wingi katika dua hiyo maalum.

Alieleza haja ya kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijaalia nchi kuwa na amani na kuhakikisha amani iliyopo inadumishwa ili neema na rehema za Mwenyezi Mungu zizidi kupatikana hapa Zanzibar.

Alisema kuwa dhima kubwa ni kuhakikisha amani inadumishwa na kusisitiza kwamba umoja wa kitaifa nao unadumishwa kwa kuunganishwa watu kama kitabu cha Mwenyezi Mungu kilivyosisitiza.

Aliongeza kuwa hapo siku za nyuma mifarakano ilikuwa mikubwa kwa sababu tu ya itikadi za kisiasa na kusisitiza kwamba wakati wa mambo hayo umeshapita na tayari kwa upande wao viongozi wameshaanza kufanya kwa vitendo kwa kukubaliana kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Alieleza kuwa bado wako wengi ambao hawajakubaliana na dhana hiyo na kusisitiza haja ya kuendelea kuwaelimisha juu ya umuhimu wa wananchi kuwa wamoja.

Alieleza kuwa katika kuleta maendeleo yanayokusudiwa kuletwa ni lazima kuwepo kwa umoja, amani na mshikamano.

Alisema kuwa suala muhimu ni kuwepo kwa amani nchini sambamba na kuwaunganisha wananchi na kuwashukuru wananchi kwa utulivu waliouonesha pamoja na kuipokea Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikiwa ni sababu ya kuleta umoja kutoka ngazi ya kisiasa mpaka kwenye familia.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa ukurasa mpya umefunguliwa wa amani na maridhiano na kumuomba MwenyeziMungu aendelee kuidumisha amani hiyo pamoja na kuyatekeleza yale yote yaliyoahidiwa na viongozi.

Aliwataka wananchi kuendelea kuwaombea dua viongozi wao, kuliombea dua Taifa lao sambamba na kudumisha amani na mshikamano na kusisitiza kwamba  iwapo yakifanywa hayo maendeleo makubwa yatapatikana kwani MwenyeziMungu amesisitiza hilo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa dini kwa kuiombea dua nchi pamoja na kuidumisha amani iliyopo na kuweza kuhubiri amani hiyo na kuwataka wale wote waliokuwa hawajakubali umuhimu wa umoja waendelee kuwaelimisha pole pole kwnai watafahamu umhimu wa umoja, mshikamano na kuondoa chuki.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alimshukuru Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabih pamoja na viongozi wote kwa kushiriki dua hiyo.

Dua hiyo maalum iliongozwa na Sheikh Ahmada Hussein Bakari na Sheikh Jamal Mohammed Abeid alitia fatha ya dua hiyo huku mufti akisoma dua maalum ya kufungia kisomo hicho. hiyo.

Hivyo basi, kumshukuru Mwenyezi Mungu ni jambo la busara na kwa vile mwanaadamu anaishi kwa kumtegemea yeye ni vyema akumshukuru na kumuomba kutokana na shida alizonazo na kumuomba msamaha pale anapokosea.