NA ASYA HASSAN

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa, amesema vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuendelea kushajiisha jamii juu ya kuongeza mshikamano, kutunza amani ya nchi na kuvumiliana.

Kitwana alieleza hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazohamasisha amani, umoja, mshikamano na mtangamano wa kijamii baada ya uchaguzi yaliyofanyika Kidongo chekundu.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) kwa kushirikiana na Shirika la Internews Tanzania.

Aidha alisema amani, umoja na mshikamano ni muhimu katika nchi yoyote kwani ndio msingi wa maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Alisema, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anasisitiza amani, utulivu na mshikamano wa jamii katika kuijenga nchi yenye maendeleo, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuandaa habari na vipindi vitakavyoimarisha umoja na mshikamano wa wazanzibari badala ya kuwagawa.

“Hakuna kitu muhimu na chenye thamani zaidi ya uzanzibari na umoja wetu, kwani huo ndio msingi imara utakaochochea kasi ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.

Alisema nchi isiyokuwa na amani haiwezi kupata maendeleo, hivyo ni lazima amani iwepo kwa kila kundi katika jamii.

Akitolea mfano wa nchi zilizoingia katika machafuko, Kitwana alisema zimeingia katika migogoro kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo uchochezi uliofanywa na waandishi wa habari, hivyo aliwataka waandishi wa habari kujifunza makosa ya wenzao.

Aliwapongeza waandishi wa habari kwa kazi kubwa waliyoifanya wakati wa uchaguzi mkuu kwa kutoa taarifa ambazo zilichangia kupatikana kwa amani na upendo miongoni mwa jamii.

“Dhima hii ni yetu sote na mliifanya kazi hii kwa kuamini kwamba nanyi mnahusika katika ujenzi wa amani kwani kazi hii ilikuwa tuifanye sisi viongozi wa siasa katika majukwaa yetu,” alisema.

Aidha aliishukuru ZPC kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwashajiisha wanachama wake kuona umuhimu wa kuhamasisha amani, utulivu na mshikamano wa kijamii katika maeneo yao.

“Naamini kama mtatumia kalamu zenu na midomo yenu vizuri na kuongeza hamasa ya kuwaonya ya kuhakikisha wazanzibari wanabaki katika hali ya amani na utulivu, bila shaka mtakuwa mnathibitisha uzalendo wenu,” alisema.

Akizungumzia ushirikiano kati ya ofisi yake na waandishi wa habari, aliwasisitiza watumishi walio chini yake kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari wanapokwenda kufuata taarifa kwao.

 Alisema mtumishi yeyote ambaye hatotoa ushirikiano kwa waandishi wa habari na kuficha taarifa atashughulikiwa.

Aliwashauri wanahabari na vyombo vya habari kuibua changamoto zinazotokea katika jamii kwa lengo la kuisaidia serikali ya awamu ya nane kufikia malengo yake.

Mapema Mwenyekiti wa ZPC, Abdalla Abdulrahman Mfaume, alisema mafunzo hayo yanayofadhiliwa na shirika la Internews ni muhimu katika ujenzi wa jamii yenye mshikamano na umoja.

Mapema mtoa mada, Ali Nassor Sultan, alisema waandishi wa habari wana wajibu wa kuhamasisha ujenzi wa jamii yenye mshikamano.

Hata hivyo, aliwahimiza wanapoandika habari zao wasipuuze mawazo mbadala kutoka makundi mengine katika jamii.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo vyombo vya habari katika kudumisha amani na umoja wa kitaifa baada ya uchaguzi.