LONDON,UINGEREZA

BAADA ya miezi kumi ya mazungumzo, hatimaye Uingereza na Umoja wa Ulaya zimefikia makubaliano ya kibiashara, yanayowawezesha kuulainisha mtikisiko wa kiuchumi unaotakana na Uingereza kujiondowa kwenye Umoja huo.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyotangazwa , wakati Uingereza itakapoondoka kwenye soko la pamoja la Ulaya katika Mkesha wa Mwaka Mpya, haitokabiliwa na vikwazo vya ushuru wa forodha kwa biashara inayofanyika kupitia bahari.

Akitangaza makubaliano hayo,Waziri Mkuu Boris Johnson alisema walifanikiwa kurejesha udhibiti wa sheria zao na pia mustakabali wao kikamilifu na kwa mujibu wa uamuzi wa Waingereza.

Kwa upande wake, Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema licha ya furaha ya kuhitimisha mazungumzo kwa mafanikio, lakini kutengana kwa umoja huo na Uingereza ni jambo la huzuni.