Majina mengi yapoteza uasili wake, yamezwa na Sayansi na Teknolojia

BIMKUBWA ABDULRAHMAN HEMED

 Dhana ya majina

KATIKA miaka ya hivi karibuni wanajamii, familia wamekuwa wakitumia majina yasioendana na utamaduni wa wazanzibari na hivyo kuwapa majina watoto ambayo wakati mwengine

DHANA ya majina si ngeni kwa wanajamii, maandiko yanatueleza kuwa baada ya kuumbwa binaadamu alifundishwa majina ya vitu vyote ili aweze kuyakabili mazingira yake (Alfarsi, 1993).

Majina aliyofundishwa mwanadamu ni ya vitu vyenye uhai na visivyo na uhai atakavyovitumia mwanadamu katika maisha yake ya kila siku.

Fasiliya majina imeelezwa katika mitazamo tofauti. Khamis (2011) Saluhaya (2010), Kihore na wenzake (2008), wameeleza jina ni aina ya neno linalotaja au kubainisha viumbe hai, vitu visisvyo uhai, mahali, hisia, hali, maarifa au tukio katika tungo.

Ally na wenzake (1930), wamefafanua kuwa jina ni kila tamko analoitiwa mwanadamu, mnyama, mmea vitu vigumu (jamadu) au kitu kingine chochote.

Hivyo, majina ni maneno yanayotaja vitu, viumbe au hali ili kuviainisha au kuvitafautisha na vitu vyengine.

Yapo majina ya kawaida kama vile, meza, nyumba, viti na jabali au majina ya pekee ambayo huwa na umbo au tabia ya kipekee au ni kitu kimoja tu, ulimwenguni majina ya watu kama vile Kazija, John na Ali.

Aidha kuna majina ya mahali kama Manzese, Kariakoo na Jang’ombe kwa mifano hiyo ni dhahiri kuwa duniani wapo Kazija wengi lakini kila Kazija mmoja ni tofauti na mwengine kiumbo na kitabia halikadhalika, Dar es Salaam, Mombasa na Unguja ziko sehemu ziitwazo Kariakoo lakini, kila Kariakoo moja ni tofauti kimaumbile na kimazingira na hizo nyengine.

Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha jina ni neno linalotumika kutambulisha mtu, mnyama, kitu, jambo, pahali au hali.

Kamusi Pevu ya Kiswahili (2017) wao wameona kuwa jina ni neno la kumtajia mtu au kutajia kitu; jina la kupanga, jina lisilokuwa na asili, jina la kupewa au kujipa tu.

Aidha Kamusi Kuu ya Kiswahili (2015) wanadai kuwa jina ni neno linalotumika kutaja mtu au kitu.

Majina ya watoto ni aina moja ya majina ya pekee yanayopatikana ndani ya mji, Mfano, mjini Unguja ambako mtafiti amekusanya data zake kuna majina ya aina mbalimbali ambayo hupewa watoto.

Wako baadhi ya wazazi hadi leo wanawaita watoto wao majina ya urithi, yaani, majina ya bibi na babu zao.

Baadhi hupewa majina mawili moja la urithi na moja la kileo na kwa kawaida hakuna baadhi ya majina yule bibi aliyekusudiwa kuitwa jina lake hutoa jina jengine kwa visingizio mbali mbali, kama vile anaogopa kuvunjiwa heshima yake pindi mtoto anapofanya makosa, na kuadhibiwa kwa makosa yake hayo huona kavunjiwa yeye heshima.

Wengine husema kwamba jina langu lishakuwa la kizamani na limepitwa na wakati mkimwita mtoto wenu wenzake watamchokoza.

Mfano wa majina hayo ni kama vile, Mashavu, Mafunda, Mwatima, Patima, Nyafu na mengineyo kwa upande wa wanawake na Pandu, Jecha, Machano, Pakacha, Makame, Mwita nakadhalika kwa wanaume.

Mutembei (2009:31) katika kuzungumzia umuhimu na utaratibu wa utoaji wa majina anauliza: kwa nini watu huwapa watu, vitu, hali au matukio majina? Je jina ni jina tu au lina maana nyuma yake? Je ni utambulisho au kielelezo cha yale yaliyopita au ni utabiri wa yale yatakayotokea?

Akijibu maswali hayo Mutembei (keshatajwa) anaeleza kwamba, kwa vyovyote vile huwa kuna msukumo fulani unaofanya watu watoe majina.

Ama kwa hakika majina tunayopewa mara nyingi huwa ni utambulisho wa asili zetu ambapo baadhi ya majina yanatambulisha mtu eneo analotoka, tabia na sifa yake na majina ni sehemu muhimu ya kila utamaduni.

Majina yana umuhimu mkubwa kwa watu wanaopewa majina, pia kwa jamii inayotoa majina hayo, kwa kawaida mtu anaepewa jina huwa kapewa utambulisho na kuwa sehemu ya jamii husika.

Kupitia jina mtu anaweza kuwa sehemu ya historia ya jamii, pia majina huweza kutofautisha matendo ya mtu mmoja na mwengine.

Uhusiano wa jina na utambulisho ni aina ya alama na mahusiano kati ya mtu na jamii husika ambapo kwa kumpa mtu jina jamii inatambua uwepo wa mtu huyo na majukumu yake katika jamii.

Muzale (1998) anafafanua kwamba; kutoa jina ni kutoa maana na majina ya binaadamu yanaweza kutusaidia kuwa na mkabala mwengine katika isimujamii na isimu historia wa kujifunza vipengele vya historia na kijamii katika jamii husika.

Maelezo haya yanabainisha wazi kwamba, majina ni kipengele muhimu katika kuelezea masuala yanayohusu jamii na historia ya jamii husika hivyo, kuwa sehemu ya utambulisho wa jamii hiyo.

Kuna mambo kadhaa yanayoamua jina fulani litokee kama lilivyo hasa majina yanayotolewa katika jamii mbalimbali za kiafrika. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na matukio ya kihistoria na amali za jamii husika.

Akiunga mkono suala la utoaji majina, Funk (1997) anaeleza kuwa mchakato wa utoaji jina hueleza mengi kuhusu mwanadamu na jinsi anavyohusiana na ulimwengu unaomzunguka.

Anaendelea kusema kuwa, utoaji jina ni tendo kama matendo mengine yoyote, na limo katika muktadha wa kisiasa.

Hivyo kuita mtu au kitu jina fulani ni tukio la kisiasa kama vile kutoa jina kunaibua masuala ya mtu mmoja mmoja na masuala ya jamii, kwa kuibua masuala ya jamii ni wazi kwamba majina huweza kuibainisha jamii moja na kuipambanua au kuitofautisha na jamii nyengine.

Guina (2001) akimuunga mkono Funk (keshatajwa) anafafanua kuwa mchakato mzima wa utoaji wa majina ni tukio la kijamii na kiutamaduni lenye kuonesha historia ya jamii husika, pia majina husimamia tajriba ya mtu au kikundi cha watu, mila, desturi, hadhi, mamlaka katika jamii. hivyo, majina hubeba utambulisho wa jamii husika.

Mwansoko (2004), katika ripoti yake ya utafiti aliyofanya katika viwanda mbalimbali katika manispaa za mji wa Tanga na Dar es Salaam kuhusu majina ya kibiashara katika Kiswahili anaeleza kwamba uzalishaji wa bidhaa viwandani uliandamana na uibukaji wa majina ya kibiashara, mengi yao yakiwa katika lugha ya Taifa ambayo ni Kiswahili, kwa vile idadi kubwa zaidi ya wanunuzi wanatumia lugha ya Kiswahili.

Takwimu zilionesha kuwepo kwa njia mbalimbali zilizotumika kubuni majina ya kibiashara katika lugha ya Kiswahili ambazo ni pamoja na kutumia maneno ya sitiari yaliyopo kwa mfano Simenti chapa simba, Sabuni chapa kiboko na Chapa swala.

Utafiti mwengine ni ule uliofanywa na Rubanza, (2000) kuhusu ubunifu wa kiisimu wa majina ya watu katika lugha ya Kihaya.

Lengo likiwa kuhusisha ubunifu huo na ule wa jamii nyingine ambapo alihusisha na jamii ya Wayoruba.

Utafiti wake ulijikita zaidi katika uchambuzi wa kimofolojia unaohusika katika uundaji wa majina. Rubanza (keshatajwa) alieleza kuwa majina ya Kihaya huwa yana maana inayozingatia; mazingira ya kuzaliwa kwa mtoto anayepewa jina hilo, hali ya kipato cha familia, mfuatano wa watoto katika kuzaliwa na migongano katika jamii kwa ujumla ikihusianishwa na muundo wa kifamilia.

Msanjila na wenzake (2009), wanazungumzia umuhimu wa majina katika suala zima la utambulisho. Katika ufafanuzi wao, wameeleza mahusiano ya majina ya familia; majina ya vitu na majina ya matukio muhimu katika jamii.

Katika kuelezea majina ya familia wamebainisha kwamba majina mengi hutolewa kwa lugha inayozungumzwa na jamii husika, hivyo, kubeba maana inayotokana na utamaduni wa mazingira ya jamii hiyo.

Majina hayo hueleweka kwa wanajamii wenyewe kwani huchukuliwa kuwa wana maarifa, elimu na uzoefu wa maisha unaofanana.

Maana za majina hayo huwa na uhusiano na utamaduni wa wazungumzaji, mazingira ya jamii ilipo, majira ya mwaka na matukio muhimu katika jamii inayohusika.

Katika kufafanua zaidi wametoa mfano wa majina ya wanafamilia kutoka jamii ya Wagogo waishio mkoa wa Dodoma nchini Tanzania. Katika jamii hiyo, majina yalitolewa kuwa na maana mbalimbali.

Kwa mfano jina la Matonya maana yake alizaliwa wakati mvua zikinyesha na kwa kawaida kwa kabila la Kigogo jina hili na la kiume.

Aidha jina la Mwamvula alizaliwa wakati mvua zikinyesha na hili ni makhsusi kwa wanawake katika jamii hiyo ya kigogo.

Jina la Mazengo alizaliwa wakati wa kukata miti ya kujengea huku jina la Matika alizaliwa wakati mazao yamekwisha wiva sambani na watu wanavuna na jina la Manzala ni wakati wa nnjaa kali watu walipokosa chakula.

Licha ya kuwa majina hayo yana maana tuliyoeleza hapo juu, pia mtu anaweza kupewa jina la aina hiyo kwa heshima tu ya kurithi kutoka kwa bibi au babu yake na si kwa sababu amezaliwa katika kipindi kinachohusiana na jina alilopewa mtu yoyote alitumia majina ya aina hiyo, ni wazi kwamba atatambuliwa kuwa anatoka katika jamii ya Wagogo.

Majina yana kazi kubwa katika maisha ya kijamii ikichunguzwa kwa makini majina hubeba maana, ambazo kimsingi, hueleweka na wanajamii wenyewe kwa sababu ni watu wenye maarifa, elimu na uzoefu wa maisha.

Waandishi wa kazi za kifasihi huyatumia majina ya wahusika ambayo yanaakisi wasifu, tabia na itikadi zao. (Wamitila, 2006), uteuzi wa majina ya wahusika unaweza kujitokeza kwa kuzingatia tabia zao katika matendo, maneno na mwelekeo wa nje.

Majina ni kipengele kimoja wapo cha fasihi chenye manufaa makubwa kwa jamii ya Ki Unguja na hutambulisha utamaduni wao, huwajuza asili na siri nyengine zilizomo ndani ya majina.

Kutokana na maelezo hayo, inadhihirika kuwa majina ya mitaa ni moja ya majina ambayo huwa na chanzo na hutoa ujumbe maalum kwa jamii. (Kennan, 2007) Majina ya mitaa yanaakisi hali halisi ya wenyeji.

Mfano wa mtaa wa Jang’ombe unajulikana kwa vituko vyake, unapopita mitaa hiyo lazima uwe imara, amelinganisha jina la Jang’ombe na tabia za wenyeji kwa kusema “Ja” ni sawa na neno kama, hivyo watu wake wana tabia kama za ng’ombe, akiusifu mtaa wa Mwera Regeza Mwendo ambako ni makaazi ya mwanzo ya utawala wa Kiarabu ukipita ukiambiwa na askari regeza mwendo ili usifanye fujo za viatu, hivyo majina ni ishara fulani kwa jamii husika.

 FUMBO JINA

Majina mengi ya watu, mifugo, vijiji, vitu nakadhalika katika makabila yetu ni aina ya mafumbo ambayo hudokeza hali, tukio au funzo fulani.

Kwa mfano mtoto aliyezaliwa na dosari za kimaumbile huitwa “njiti”. Mtoto aliyezaliwa wakati wa njaa akiitwa “Mwanjaa”. Anayezaliwa wakati wa vita akiitwa “Mwamvita” nakadhalika.

Haya ni mafumbo mepesi yapo mafumbo yenye utata zaidi mathalan jina la “Ashibaye” linadokeza hali na mtazamo fulani wa familia ya mwenye jina hilo.

Kirefu chake ni methali isemayo; “Ashibaye hamjui mwenye njaa”. Jina la “Msanjila”. Au “Mihanda”, au “Kamuhanda”, au “Kalimanzila” hudokeza safari au njia.

Ama mwenye jina hilo alizaliwa safarini au alizaliwa wakati baba/mama yake alipokuwa safarini hivyo majina mengi ya mafumbo huhusiana na imani za dini.

Mathalan,” Riziki”, “Zawadi”, “Elikunda”, “Eleshi”, “Binamungu”, “Kawamala” na kadhalika. Katika jamii ya Wahaya huko Bukoba majina ya wajakazi yalikuwa ni mafumbo yenye mwito na mwitiko.

Katika mfano huu unaotoka katika utenzi wa Kachwenyanya (Mulokozi 1987:98) jina la mjakazi, “Nshekel’okumanya”, ni fumbo ambalo jibu lake ni “amagenzi gage guli omunda”. Ujumbe uliomo ni kwamba vitu vya siri havioneshwi hadharani, bali hufichwa moyoni au kutumika pale inapohitajika tu.

Katika jamii ambazo zilitumia ngoma kama ishara ya utawala, majina ya ngoma hizo yalikuwa ni mafumbo.

LAKABU

Ni majina ya kupanga ambayo baadhi ya watu hupewa au hujipatia kutokana na sifa zao za kimwili, kinasaba, kitabia au kimatendo. Majina haya huwa ni maneno au mafungu ya maneno yenye maana iliyofumbwa.

Mara nyingi majina haya huwa ni sitiari. Baadhi ya majina humsifia muhusika, lakini mengine humkosoa au hata kumdhalilisha. Mifano mizuri ni lakabu zinazotumika katika vivugo na tendi.

Mfano wa majina hayo ni Mukwavinyika (Kihehe): Mtekaji wa nyika.

Jina la ushujaa la Mutwa Mukwava wa Uhehe (kama 1850 – 1898)

Ka Itaba Mbibi: Mtoto wa Mchanganyamipaka

Jina la mtawala wa Kyamutwala, Bukoba (kama 1860 -1890) aliyejulikana kwa ufupi kama Kaitaba.

 MAJINA YA WATOTO

Majina ya watoto ni majina wanayoitwa watoto baada ya kuzaliwa kwao. Hapo zamani waliokuwa na mamlaka ya kutoa majina ya mtoto aliyezaliwa ni bibi au babu, majina hayo mara nyingi yalikuwa ni majina ya urithi kutoka kwa mabibi au mababu zetu. Hii ilisaidia kuongeza heshima kwa wazazi na kutunza historia yetu. Lakini kwa sasa hali imebadilika jambo ambalo limempelekea mtafiti kujiuliza maswali mengi kuhusiana na hilo na ndio kiini cha tatizo lake.

Baadhi ya watu aliowahoji mtafiti walitoa majibu mbalimbali kuhusiana na mabadiliko hayo ya uitaji wa majina ya watoto.

Kwanza walikiri kuwepo kwa mabadiliko hayo na walisema kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia ndiyo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa cha mabadiliko hayo.

Kupitia intaneti, watu hutafuta majina kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii na kuwapatia watoto ili kwenda na wakati na ulimwengu wa kileo. Tofauti na zamani ambapo watoto walipewa majina kulingana aidha na historia ya nchi, majanga mbalimbali yaliyojitokeza kipindi cha uzazi wa mtoto huyo au pia kurithi jina la bibi na babu yake.

Kwa mfano zamani watoto waliozaliwa nje ya ndoa wakipewa majina ya mafumbo.

Mara nyingi majina hayo hutoa mama wa mtoto aliyepata ujauzito kwa kuiambia jamii yake jambo kuhusiana na tukio lile alilofanya mtoto wake. Mfano wa majina hayo ni pamoja na Jina la Semeni lenye maana ya kwamba jamii iendelee tu kusema kwa kila kitu.

Aidha jina la Sikujua linamaanisha kuwa hakujua kama mtoto wake atamtia aibu huku jina la Siajabu liwa na maana ya mtoto wake si wa kwanza kufanya tukio na kwamba wengi wanaendelea kufanya.

Pia watoto zamani wakipewa majina kutokana na matukio ya kijamii.  Mfano, harusi, sherehe ya uzao wa bwana Mtume Muhammad (S.A.W), dhiki, shida na tabu anazopitia mama mpaka kumzaa mtoto wake, sikukuu, matukio ya kisiasa, kumtukuza baba au mama kwa kutomkata jina wakati wa kumpa jina mtoto na pia matukio ya kupoteza watoto sana yaani kila mama anapozaa mtoto anakufa nakadhalika.

Kwa mfano watoto waliozaliwa kukiwa nyumbani kwao kuna harusi mtoto huyo huitwa Mwanaharusi.

Waliozaliwa kipindi cha sherehe ya uzao wa Bwana Mtume Muhammad (S.A.W) huitwa Maulid pia jina hili hutumiwa na wanaume na wanawake.

Watoto waliozaliwa kipindi cha shida na dhiki watoto hao hupewa majina kama vile Tabu, Shida, Mashaka na hayo huitwa wanawake na wanaume.

Watoto waliozaliwa kipindi cha watu kwenda kufanya ibada ya Hijja huko Makka Saudi Arabia wanaume huitwa Hijja na wanawake Mwanahijja.

Watoto wanaozaliwa sikukuu baada ya mfungo wa Ramadhani huitwa Iddi kwa mwanamme na mwanamke Mwanaidi na wengine huitwa Shawwal jina hili ni kwa mtoto wa kiume tu.

Kuna baadhi ya watu wakizaa hawapati hivyo hulazimika kuwanunua watoto wao baada ya kuwazaa, nahii dhana ya kununua mtoto haimaanishi kwamba unatoa pesa kwa ajili ya kumnunua mtoto huyo bali ni kama itikadi flani ambayo huja mzee wa makamo na kumbatiza jina lolote kama vile Mtumwa kwa kusema kuwa huyu ni Mtumwa wangu ili kumgomboa mtoto na kifo, Kibaya kumaanisha hicho kitoto ni kibaya hivyo ubaya usimdhuru. Inapotokezea mtu kuzaa pacha basi mtoto mmoja kati ya hao humwita Riziki kumaanisha kwamba ni riziki yake kupata pacha.

Lakini pia, kuna wale wanaoamua kuwazaa wazazi wao lakini kwa kuhofia kuwakata jina basi mtoto wa kiume humwita Shaib na wakike Bimkubwa. Na kuna wale wanaozaliwa tarehe za kihistoria kama vile Karume day na siku ya uhuru basi watoto hao huitwa Karume na Uhuru.

Kutokana na mabadiliko ya dunia yaliyokumbwa na Sayansi na Teknolojia uitaji wa majina ya watoto umebadilika sana hasa pale panapopatikana mwingiliano wa kitamaduni baina ya nchi moja na nyengine.

Kupitia tovuti mbalimbali za Intaneti watu huangalia majina humo na kuwaita watoto wao yaliyo kinyume kabisa na majina ya tamaduni zao. Baadhi ya majina wanayoitwa watoto wa zama hizi ni Jina Merwa na maana yake ni Mlima ulioko Makka.

Aidha jina la Rumaisa maana yake ni upole huku jina la Raifat likimaanisha mzuri na Mennal ni ua maalumu la peponi ambapo Malak ni malaika huku Khabira akiwa ni mjuzi sambamba na Khalifa likiwa na maana ya kiepnzi.

Haya ni miongoni mwa majina yanayoonekana yanakwenda na wakati wa zama hizi. Majina kama Fatuma, Asha, Khadija, Maryamu, Ali, Abdalla, Khamis, Hamad na mfano wa yale tuliyoyaainisha huko nyuma yanaonekana kupitwa na wakati na hayana nafasi tena katika jamii.

Baadhi ya watu wanadai kuwa majina hayo yamezagaa sana kiasi ambacho huwezi kupita nyumba mbili usikutane na jina moja kati ya hayo na hayo ni kwa upande wa mjini na kwa upande wa shamba majina kama Mwatima, Patima, Mwazume, Kombo, Makame, Pandu, Jecha haya ni majina maarufu sana huko vijijini.

ATHARI ZINAZOPATIKANA

Kwanza kupoteza historia ya jamii, kwani badala ya kuita majina yanayoendana na historia ya nchi yetu tunajikuta ni watumwa wa historia za jamii nyengine.

Pili, kupoteza majina ya asili yanayoendana na utamaduni wetu kwa mfano utamaduni wetu ni kuita majina ya urithi kutoka kwa bibi na babu zetu, ama kuita majina kulingana na matukio mbalimbali yanayotokea katika jamii kama tulivyokwisha ona huko nyuma.

HITIMISHO

Kutokana na takwimu mbalimbali zilizokusanywa na mtafiti, imedhihirika kwamba vijana walio wengi hususan wa mijini, wameacha mila na desturi zao katika suala zima la uitaji wa majina ya watoto wao kwa visingizio tofauti.

Sababu kubwa ambayo imetolewa na wahojiwa wote ni mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ambayo imeifanya dunia kuwa kama kijiji, na kuifanya dunia yote ikumbwe na mabadiliko yote yanayotokea ulimwenguni.

Mabadiliko hayo hayapo tu kwenye uitaji wa majina lakini hata katika mavazi, makaazi, chakula nakadhalika.

Waliendelea kusema kwamba majina ya urithi yameshapitwa na wakati na hayana nafasi tena katika ulimwengu huu tunaokwenda nao, kwani kumpa mtoto jina la kizamani anaweza kuchekwa na kumnyima uhuru wa kujieleza popote kutokana na jina lake hilo kukosa mvuto wa kileo.

Kwa kumalizia tunaweza kusema kuwa tuende na wakati ila tusipoteze asili yetu wala kuutia doa utamaduni wetu.