Na  Ali  Shaaban Juma

Nembo ni alama ya utambulisho inayotumika kama kielelezo kinachowakilishi kampuni, chama cha siasa, timu ya mpira, jumuiya ya kiraia, shirika au madhehebu fulani. Nembo ni mchoro au michoro yenye vielelezo vilivyochorwa kisanii ambavyo huwakilisha taswira halisi ya  jamii, timu, taasisi au shirika husika. Vielelezo vinavyochorwa katika nembo ni ishara inayowakilisha jambo fulani liwe la kijamii, kisiasa, kiuchumi au kiutamaduni  linalohusu wamiliki au mmiliki wa nembo hiyo.

Mbali ya aina mbalimbali  za nembo binafsi, lakini pia kuna nembo za mataifa ambazo ni alama maalum zinazotumiwa na nchi au taifa fulani kama alama rasmi ya utambulisho wa taifa hilo. Mbali ya bendera na wimbo wa taifa ambavyo ni vielelezo vya taifa, lakini pia nchi na serikali  zote duniani huwa na nembo inayotumika kuwasilisha taifa hilo ambapo nembo hiyo huonekana katika noti za nchi hiyo, hati ya kusafiria na hata katika barua rasmi za serikali zinazotoka katika taifa hilo.

Baadhi ya nchi mbali ya kuwa na nembo ya taifa, lakini pia nchi hizo huwa na mti, ndege, mnyama au mchoro fulani wa sanaa ambao ni kielelezo cha taifa hilo.

Pia kuna baadhi ya nchi ambazo zimeundwa na majimbo mbalimbali, nchi hizo huwa na nembo za majimbo hayo.

Mfano  India ni nchi yenye majimbo 28 ambapo kila jimbo lina nembo yake inayowakilisha jimbo hilo.

Nembo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilichorwa na Jeremiah Wisdom Kabati, wa  Bwiru huko Mwanza nchini Tanzania hapo mwaka 1964. Nembo hiyo ilitokana na nembo ya Jamhuri ya Tanganyika baada   ya taifa hilo kupata uhuru wake tarehe 9 Disemba, 1961.  Baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hapo tarehe 26 Aprili, 1964, nembo hiyo ya Tanganyika ilifanyiwa marekebisho na kuwa nembo ya Tanzania.

Nembo ya Tanzania ina vielelezo kadhaa ambapo kielelezo kikubwa ni Ngao yenye vielelezo vyengine ndani yake. Ndani ya Ngao hiyo kuna bendera ya Tanzania ambapo sehemu ya juu ya ngao hiyo, kuna mwenge unaowaka ambao ni ishara ya uhuru, elimu na kufuta ujinga. Mwenge huo uko katika rangi ya dhahabu ambayo ni kielelezo cha madini yanayopatikana katika taifa hilo.

Chini ya bendera ya Tanzania, kuna rangi nyekundu inayowakilisha ardhi ya bara la Afrika yenye rutba. Chini ya rangi nyekundu kuna mawimbi meupe na buluu ambayo ni kielelezo cha bahari, mito, maziwa na ukanda wa pwani wa Tanzania. Katikati ya ngao hiyo kuna mkuki ambao ni kielelezo cha ulinzi wa taifa ambapo shoka na jembe ni vielelezo vya vitendea kazi vinavyotumiwa na Watanzania katika harakati za uzalishaji mali, ujenzi wa taifa na kutafuta maendeleo.

Ngao iko juu ya Mlima Kilimanjaro ambao ni kielelezo cha Tanzania ambapo pembeni ya ngao hiyo upande wa kushoto na kulia kuna pembe za ndovu zilizoshikiliwa na mwanamme upande wa kushoto na mwanamke upande wa kulia.

Chini ya miguu ya mwanamme kuna kitawi cha Mkarafuu na kitawi cha Mpamba kipo chini ya miguu ya mwanamke. Mazao hayo yanasafirishwa nje na kuingiza fedha za kigeni.  Mwanamke amevaa kilemba chenye rangi ya dhahabu ikiwa ni kielelezo cha ushirikiano. Maandishi uhuru na umoja  ni kauli mbiu ya taifa hilo.

Nembo ya Msumbuji iliyoidhinishwa hapo mwaka 1990  ina vielelezo kadhaa ikiwemo gurudumu lenye rangi ya manjano lililozungukwa na shuke la mahindi upande wa kulia na shuke la muwa upande wa kushoto. Juu katikati baina ya mashuke hayo mawili kuna nyota yekundu.

Katikati kuna jua linalochomoza juu ya ramani ya taifa hilo yenye rangi ya kijani na mawimbi ya bahari yenye rangi  buluu na nyeupe yapo chini ya ramani hiyo. Pia katikati ya gurudumu hilo lenye rangi ya manjano, kuna  jembe, bunduki chapa ya AK-47 na kitabu chenye rangi nyeupe kilichofunguliwa. Vielelezo vyote hivyo vimo ndani ya koja lenye maandishi ya jina la nchi hiyo yaliyoandikwa kwa lugha ya kireno.

Vielelezo vyote hivyo vinawakilisha mambo mbali mbali ya kitaifa ambapo shuke la mahindi na mua ni kielelezo cha utajiri wa kilimo. Gurudumu ni kielelezo cha kazi na uzalishaji mali viwandani ambapo kitabu kilichofunguliwa ni kielelezo cha elimu.

Jembe linawakilisha kilimo na wakulima ambapo kwa vile taifa hilo lilipata uhuru wake kwa njia ya mtutu wa bunduki kutoka kwa wakoloni wa Ureno, bunduki ni kilelezo cha ukombozi, ulinzi na ushujaa. Nyota nyekundu ni ishara ya umoja na mshikamano wa watu wa Msumbuji na jua linalochomoza ni ishara ya maisha mapya yenye matumaini, tija na faraja.

Nembo  ya Djibouti ilianza kutumika rasmi  tarehe 27 Juni, 1977 baada ya taifa hilo kupata uhuru wake kutoka kwa Ufaransa.  Nembo hiyo imezungukwa na  majani ya mti uitwao “laurel” ambao ni mti maarufu huko Mashariki ya Kati na unatumiwa  katika mapishi mbalimbali. Katikati ya nembo hiyo kuna mkuki uloelekea juu ya nyota  uliyo nyuma ya ngao.

Chini ya ngao hiyo kuna mikono miwili iliyoshika mapanga kushoto na kulia. Mikono hiyo miwili inawakilisha makabila makuu mawili ya taifa hilo ambayo ni Afar na Issa. Nyota iliyo juu ya mkuki ni kielelezo cha mshikamano wa makabila hayo mawili ya taifa hilo.

Nembo  ya Uganda ilidhinishwa wiki tatu kabla ya taifa hilo kupata uhuru wake  hapo mwaka 1962. Baadhi  ya vielelezo vilivyomo katika nembo hiyo  ni pamoja na Ngoma, Mikuki, Ngao, Ndege, Jua, Swala na Ardhi ya kijani. 

Mkuki na ngao ni vielelezo vinavyowakilishi nia ya dhati ya watu wa taifa hilo kulinda nchi yao.  Ndani  ya ngao hiyo kuna mawimbi  ya maji, jua na ngoma. Mawimbi ya maji ni kiwakilishi cha maziwa Viktoria na Albert yaliyoko nchini humo, ambapo jua ni kielelezo  cha siku njema kwa watu wa taifa hilo. Ngoma ni kielelezo cha utamaduni  wa taifa hilo na njia moja wapo ya kuita watu katika mikutano mbalimbali. Pia ngoma hiyo ni kielelezo cha utawala wa jadi wa Uganda  wa Bunyoro. Ndege aitwae, “Crane” aliye upande wa kulia wa ngao hiyo ni  ndege wa taifa hilo ambapo Swala ni kielelezo cha aina mbalimbali za wanyama wanaopatikana katika mbuga za taifa hilo.

Ngao hiyo iko juu ya ardhi tambarare ya kijani inayowakilisha utajiri wa ardhi na misitu ya kijani ambapo chini ya ardhi hiyo kuna maji ya mto yanayotiririka yanayowakilisha Mto Nile. 

Upande wa kulia wa mto huo kuna kitawi cha Mpamba na upande wa kushoto kuna kitawi cha  Mbuni  ambayo ni mazao makuu yanayolimwa nchini humo na kusafirishwa nje na kuliingizia taifa hilo pesa za kigeni.

Wakati wa vita vya ukombozi vinamalizika hapo mwaka 1945, Korea ya Kaskazini haikuwa na nembo ya taifa. Hata hivyo, nembo rasmi ya taifa hilo ilianza kutumika mwaka 1948, baada ya kugawika Korea na kuwepo Korea ya Kusini na ile ya kaskazini. Baadhi ya vielelezo vilivyomo katika nembo ya Korea ya Kaskazini ni pamoja na bwawa la kuzalisha umeme la Supung. Juu ya bwana hilo kuna Mlima Paektu ambao pamoja na mambo mengine, ni kielelezo muhimu cha utawala wa ukoo wa Kim katika taifa hilo. Juu ya Mlima huo kuna nyota ambayo mwangaza wake umegusa mashuke ya mpunga yaliyoko kulia na kushoto mwa koja lenye ufito mwekundu chini yake. Katikati ya koja hilo kuna maandishi yaliyoandikwa kwa herufi za “Chosongul” ambayo tafsiri yake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea.

Mali ni taifa lilioko Afrika ya Magharibi ambalo nembo yake ilianza kutumika mwaka 1973.  Vielelezo vilivyomo katika nembo hiyo ni pamoja na Njiwa, Msikitiki, Jua linalochomoza na mshare na upinde. Vielelezo vyote hivyo vinawakilisha utamaduni, siasa na uhusiano wa  kikanda. Msikiti uliomo katika nembo hiyo ni kielelezo cha Msikiti Mkuu ulioko katika mji wa kihistoria wa Djenne uliojengwa katika karne ya 13. Pia msikiti huo ndani ya nembo hiyo ni kielelezo cha dini ya kiislamu ambapo asilimia 94% ya watu wa taifa hilo ni waislamu. Juu ya msikiti huo kuna njiwa anayeruka ambaye ni ishara ya amani na utulivu katika taifa hilo. Pia kuna mshare na upinde na jua linalotoka.

Nembo  ya Papua New Guinea imechorwa na mchoraji wa Australia aitwae Hal Holman na kuidhinishwa  na bunge la nchi hiyo kuwa nembo rasmi ya taifa hapo tarehe 24 Juni, 1971. Vielelezo vikuu vilivyomo katika nembo hiyo ni pamoja na ndege aitwae, “Bird of Paradise” ndege ambao hupatikana kwa wingi huko Papua New Guinea. Pia kuna mkuki na ngoma.

Nembo  ya Kuwait  ilichorwa mwaka 1962 ikiwa na ngao yenye rangi za bendera ya taifa  hilo chini ya nembo hiyo. Ngao hiyo yenye rangi ya bendera za taifa hilo iko chini ya Mwewe mwenye rangi ya dhahabu.

Juu ya kichwa cha mwewe huyo, kuna duara lenye dau lenye bendera ya nchi hiyo linaloelea baharini lililoandikwa jina la taifa hilo kwa lugha ya herufi za kiarabu.

Dau hilo ni kielelezo cha mawasiliano na usafiri wa baharini wa kale ulotumiwa na watu wa taifa hilo kusafiri hadi mataifa mengineyo. Mwewe ni kielelezo cha kabila la Makuraish walokuwepo mji mtukufu wa  Makka  kwa karne kadhaa. 

Nembo  ya Uruguay  taifa ambalo  liko Marekani  ya Kusini ilichorwa na mchoraji aitwae  Juan Manuel Besnes Irigoyen hapo  mwaka 1788 na iliidhinishwa rasmi hapo  tarehe 19 Machi, 1829. Nembo  hiyo ina vielelezo kadhaa vilivyopangwa kwa usanifu wa hali ya juu ambapo duara kubwa mithili ya yai limegawiwa katika sehemu nne zilizokatwa sawa sawa.

Juu  ya duara hilo kuna picha ya jua linalochomoza ambalo linajulikana kama, “Jua  la Mei”.  Jina hilo linatokana na historia ya harakati za kudai uhuru za taifa hilo ambapo  kati ya tarehe 18-25 Mei, 1810 huko Buenos  Aires  katika koloni la Wahispania la Rio de la Plata  eneo ambalo kwa sasa ni nchi za Argentina, Bolivia, Paraguay, Uruguay  na sehemu  ya  Brazil kulitokea mapambano yaliyosababisha kuanguka kwa utawala wa Baltasar Hidalgo de Cisneros  de la Torre  na hatimaye kuasisiwa kwa taifa hilo la Uruguay huru. Duara la nembo hiyo limezungukwa na vitawi vya Mzaituni  ikiwa ishara  ya amani na utulivu.

Rangi ya buluu na nyeupe iliyoko ndani ya duara hilo ndiyo rangi rasmi ya bendera ya taifa hilo ambapo mizani yenye rangi ya dhahabu iko upande  wa juu kushoto wa duara hilo ikiwa ni ishara ya usawa na sheria. Upande wa juu kulia kuna picha ya kasri  maarufu la kihistoria nchini humo, lilioko juu ya  Mlima Montevideo.  Upande wa chini  kushoto kuna picha ya farasi mweusi ambae  ni kielelezo cha uhuru wa watu wote bila vikwazo. Picha ya Ng’ombe dume iko chini upande wa kulia ndani ya duara hilo ambayo ni kielelezo cha ufugaji na kitoweo kikuu kinachopendwa na watu wa taifa hilo ambacho ni nyama ya ng’ombe.

              Nembo  ya  Jamhuri  ya  Muungano wa  Tanzania

           Nembo ya  Msumbiji taifa  lililopata uhuru wake kwa mtutu wa bunduki

Nembo  ya  Uruguay  taifa lilioko Kusini Mashariki mwa Amerika  ya Kusini

        Nembo  ya Djibouti taifa lilioko katika pembe ya Afrika

                         Nembo  ya  Uganda  taifa  lilioko Afrika  Mashariki

 Nembo  ya Jamhuri  ya  Kidemokrasia ya Watu wa  Korea (Korea  ya Kaskazini)

                              Nembo   ya Papua   New Guinea

                    Nembo  ya  Mali taifa lilioko  Afrika Magharibi

                  Nembo  ya Kuwait  taifa lilioko Ghuba  ya Uajemi