LONDON, England
KOCHA wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amezungumzia maendeleo ya mashetani wekundu hao, miaka saba tokea alipoondoka Old Trafford.


Ferguson, alipokuwa kocha wa United, kila baada ya sikukuu ya Christmas,alisema, anaweza kuanza kuzungumzia nani atakuwa bingwa wa England.


Lakini safari hii amekuwa akizungumzia hali ya United na mabadiliko katika timu hiyo. Alisema walimchagua, David Moyes kwa kuwa alikuwa na muendelezo mzuri akiwa na Everton na alidumu kwa muda mrefu, lakini, kwa bahati mbaya mambo hayakuwa mazuri kwake ingawa hakufanya vibaya.


Alisema, pia walimchagua Louis van Gaal ambaye alifanya mabadiliko mengi, kujenga timu upya kwa sababu ya uzoefu na uwezo mzuri wa kufanya hivyo, lakini, hakupata mafanikio ya haraka.


Aidha, Jose Mourinho ambaye ametwaa mara mbili mataji ya Ulaya, na kubeba ubingwa wa ligi katika kila nchi aliyokwenda na amenyakua vikombe vingi vikubwa, lakini, alikumbana na changamoto kila alipotaka kuleta mabadiliko.


Alisema, hivi sasa klabu ikiwa chini ya Ole Gunnar Solskjaer ambaye ameiongoza kwenye mechi 110 akishinda 61, ana muelekeo mzuri.


Hata hivyo amekumbusha kuwa mahitaji ya mafanikio ya haraka yatakuwa ni changamoto kwa kila kocha wa timu ya Ligi Kuu ya England.


Wakati huo huo, mechi ya Everton na Manchester City iliahirishwa kutokana na maambukizi ya ‘corona’.
Everton imesema itaomba ufafanuzi kamili kutoka wasimamizi wa Ligi Kuu ya England kutokana na kitendo cha kuahirishwa kwa mechi hiyo, iliyokuwa imepangwa kuchezwa katika uwanja wa Goodison Park.


Everton walipewa taarifa kuhusu kuahirishwa kwa mechi, saa nne kabla ya mchezo kuwa baadhi ya wachezaji wameguduliwa kuambukizwa ‘corona’.


Wachezaji hao ni mbali na Kyle Walker na Gabriel Jesus, waliokuwa wamethibitishwa kabla ya siku ya Krismasi.


Habari pia zilisema vipimo vipya vilithibitisha wachezaji wengine watatu zaidi wameambukizwa.
Mkutano wa bodi ya Ligi Kuu ya England ulikubali kupanga upya mchezo huo baada ya ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya.


Kabla ya kuahirisha mchezo huo ambao ungelihudhuriwa na mashabiki 2000, maandalizi yote yalikuwa yamekamilika, kitendo ambacho kimeikasirisha Everton.(BBC Sports).