Baada ya kupatiwa vifaa, elimu ya hedhi sasa wahudhuria

NA HUSNA MOHAMMED

BAADA ya gazeti hili mwaka jana kutoa makala kuhusiana na ukosefu wa taulo za kike zinazowafanya wanafunzi kukosa kuhudhuria masomo katika Skuli za Kijini na Mbuyutende huko Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja hatimae tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi.

Kama tunavyojua kuwa matumizi ya taulo za kike husaidia sana wanawake na wasichana hasa wanafunzi kushiriki harakati za kiuchumi licha ya kuwepo mtazamo potofu katika matumizi ya pedi hasa vijijini.

Awali Utafiti uliofanywa mwaka 2018 na mradi wa huduma za jamii wa Best of Zanzibar kwa kushirikiana na walimu na Wizara ya Afya Zanzibar, umeonyesha wasichana aslimia 90 hukosa ufahamu wa hedhi salama na vifaa vya kuwasitiri wakiwa katika siku zao.

Hivyo gazeti hili mwaka jana wa 2019 lilifika vijiji vya Matemwe vya Mbuyutende na Kijini, ili kujua hali halisi ya wasichana na wanawake katika vijiji hivyo juu ya suala zima la hedhi salama.

Ilibainika kuwa wanawake na wasichana hasa wanaosoma skuli wanekuwa na mitazamo hasi juu ya hedhi jambo ambalo walishindwa kushiriki katika shuhuli za kijamii n ahata kuhudhuria masomo darasani katika kipindi chao cha hedhi.

Hivyo, mradi wa Best of Zanzibar uliyo chini ya Program ya kusadia elimu ya usafi wa afya na mazingira umewasaidia wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari katika kijiji cha Kijini na Mbuyutende huko Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja, mara baada ya kuona makala kuhusiana na tatizo la wanafunzi wa kike kukosa masomo katika kipindi cha hedhi.

WANAVYOZUNGUMZA WANAFUNZI WA KIKE KUHUSINA NA HEDHI

“Kabla ya kupewa pedi nikiwa katika hedhi siku ya kwanza hadi ya tatu siendi skuli kwa sababu damu ya hedhi inatoka kwa wingi na hivyo naweza kuchafua sare yangu ya skuli, lakini baada ya kupata msaada wa taulo za hedhi sasa nahudhuria masomo kama kawaida”, alisema Mwamvua Kheri Ussi.

Mwamvua Kheri Ussi (15), ambae ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika skuli ya Kijini Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja aliyasema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya aliefika kijijini hapo ili kujua hali halisi ya masuala ya hedhi yanavyochukuliwa katika eneo hilo.

Nae Siti Koba, alisema kabla ya kupata vifaa vya hedhi alikuwa akitumia vitambaa vya kanga vilivyochakaa na kujistiri, jambo ambalo lilipelekea kuchafua nguo nyengine kama atakaa nacho kwa muda kidogo.

“Nilikuwa nikienda skuli sipati kubadilisha na kufua lakini hivi sasa vifaa tulivyopewa unaweza hata kusuuza na kutia kwenye kifuko maalumu na nikirudi nyumbani nafua vizuri kwa sabuni na kuwa kisafi zaidi”, alisema.

Nae Kondo Machano Ngwali (19) aliemaliza elimu yake ya kidato cha nne mwaka jana katika skuli hiyo ya Kijini, alisema wakati akisoma skuli alikatisha masomo yake kwa wiki nzima ili kuidhibiti hedhi akiwa nyumbani kwao.

“Naumwa na tumbo na damu ya hedhi inatoka kwa wingi, hata mama huniambia nisiende skuli kwa sababu sitoweza kusoma muda wote nitakuwa na wasiwasi wa kuchafua nguo zangu, lakini kwa sasa na mimi nimepata mgao wa taulo natumia bila ya tatizo lolote”, alisema Kondo.

Kwa upande wake Hamisa Salum (12) mwanafunzi wa darasa la tano skuli ya Kijini, anasema wakati alipopata hedhi alipelekwa kwa bibi yake na kumfundisha namna ya kujistiri kwa kutumia vipande vya kanga zilizochakaa.

“Miaka ya nyuma nikiwa kwenye hedhi nguo zangu za hedhi huanika pembeni ya kitanda lakini hivi sasa naanika sehemu za wazi nje kwenye Kamba baada ya kupewa mafunzo na taulo nzuri za kujistiri hedhi nimepata mwamko mkubwa sina wasiwasi nikiwa kwenye hedhi”, alisema Hamisa.

Nae Mashavu Machano kutoka skuli ya Mbuyutende Matemwe, ambae ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza anasema hedhi ni suala la usiri mkubwa kijijini kwao.

“Zamzni tliambiwa tusiende skuli kwa sababu vitambaa vya hedhi haviwezi kuhimili muda mrefu tunaweza kujichafua kama tutakwenda skuli, lakini kwa sasa tulipopewa vifaa na pedi maalumu tunajivunia tunahudhuria masomo yetu”, alisema Mashavu.

Kwa upande wake Tatu Kozi aliemaliza elimu yake ya sekondari mwaka jana skuli ya Mbuyutende yeye alisema wakati alipokuwa akisoma akiwa katika hedhi halazimiki kufanya jambo lolote na badala yake kuwa maeneo ya kwao.

“Nilipokuwa nasoma sikwenda hata siku moja skuli nikiwa kwenye hedhi mpaka nimalize hedhi kati ya siku moja hadi saba ndio niende skuli, nadhani ilichangia kutofaulu vyema masomo yangu ya kuendelea na kidato cha tano”, alisema Tatu. 

WAZAZI NA WALEZI

Zuhura Simai Jaku (48) yeye alisema mtoto wake alikuwa akimkataza kabisa kuhudhuria masomo skuli kwa dhana ya kujichafua sare zake za skuli na wenziwe pamoja na walimu kumjua kama yuko katika hedhi.

“Mara nyingi watoto wakiwa kwenye hedhi tulikuwa hatutaki kwenda mbali na nyumbani, tunataka wawepo mazingira ya hapa kwa sababu vitambaa wanavyopewa kujihifadhia viko dhaifu na wengine wanatoka damu nyingi siku za mwanzo, lakini sasa wanaenda kama kawaida”, alisema Zuhura mwenye watoto wawili wasichana wanaosoma skuli ya sekondari ya Kijini.

“Huku kwetu tulikuwa tukitumia vifaa vyetu vya asili vya hedhi, lakini tangu kupewa vifaa hivyo afadhali na vikeshachakaa tunaenda kununua Kinyasini ndiko vinakouzwa”, alisema.

Nae Miza Mati (63) anasema yeye kama bibi tayari ameshawafunza wasichana zaidi ya 10 namna ya kujistiri wakiwa katika hedhi.

“Kwa kweli masuala ya hedhi ni ya usiri mkubwa sana, hatutaki watu wajuwe kama watoto tukiwaruhusu kwenda skuli au kurandaranda kila mtu atajua, alkini wamepewa vifaa vizuri sasa hakuna anaejua unakwenda zao na shughuli zao kama kawaida.

Ingawa Miza anakiri kuweko kwa mabadiliko kidogo katika miaka ya sasa ambapo anasema miaka ya nyuma walitumia sana vitambaa vya kanga vilivyochakaa lakini sasa wanatumia vitambaa vizito vipya na kuwafundisha wasichana wanaokuwa kwenye hedhi namna ya kujistiri, na kusisitiza vifaa walivyopewa vinawasaidia sana.

WALIMU WANAZUNGUMZIAJE

Mwalimu Kazija Omar alisema bado kuna imani potofu kuwa mtoto wa kike akitumia taulo za kujistiri hatopata kizazi.” alisema Mwalimu Kazija.

Anasema kuna wanafunzi wanapewa Pedi za msaada lakini wanalazimika kuzitupa chooni kutokana na imani potofu na wengine hata kuzuiwa kutoka nyumbani wanapokua katika siku zao za hedhi jambo ambalo linawakosesha masomo.

“Hapa awali huku kwetu kijijini kulikuwa na dhana potofu suala la hedhi kwani wanafunzi wetu wakiwa katika hedhi hawaji skuli mpaka wamalize au karibu ya kumaliza kwa hofu ya kuchafua nguo zao, lakini sasa baada ya kupatiwa elimu ya hedhi pamoja na pedi sasa wanahudhuria masomo na kushiriki katika shughuli za kijamii wao na wazazi wao”, alisema.

Mwalimu Kazija alisema kwa kawaida darasa moja linakuwa na wanafunzi 20 hadi 25 huku wanawake wakiwa saba ambapo wanafunzi wa kike kama wanne wanaweza kupata hedhi kwa pamoja hivyo walikuwa hawahudhurii masomo lakini tangu kupatiwa vifaa sasa wanahudhuria kama kawaida.

Nae Mwalimu mwengine wa skuli ya Mbuyu tende aliejitambulisha kwa jina moja la Mtumwa, alikiri upungufu wa mahudhurio ya wanafunzi wa kike wanaopata hedhi siku za mwanzo wa hedhi.

“Ninapomwita mwanafunzi na kumsaili kwa nini hakuhudhuria masomo yake kama siku tatu hadi tano huniambia allikuwa katika hedhi, lakini kwa sasa hayo hakuna wamepatiwa vifaa sasa wanakuja kama kawaida”, alisema mwalimu huyo.

Mwalimu huyo aliiomba Serikali kutilia mkazo upatikanaji wa vifaa vya hedhi ili wanafunzi wanawake waendelee kuhudhuria skuli wakati wakiwa katika hedhi.

BEST OF ZANZIBAR

Aminata Keita, Afisa Mradi wa Best of Zanzibar, chini ya unafadhili wa na Kampuni ya Panroyal Limited, alisema kuwa waliona haja ya kuwasaidia wasichana wa skuli hizo ili nao kushiriki katika masomo na harakati za kijamii kwa ujumla.

“Pamoja na kuwapatia masomo ya ziada wanafunzi wa sekondari kwa lugha ya Kingereza, Hisabati na sayansi ili kuinua viwango vyao kitaaluma na ufaulu katika skuli hizo, lakini tumeona kuwapa taalumu juu ya hedhi salama sambamba na vifaa vya kuwasaidia wakati wanapokuwa katika hedhi”, alisema.

“Tumebaini kuwa mitazamo hasi imeota mizizi na kwamba suala la hedhi kwao wanaona kama ni mtihani, wengi tuliozungumza nao kama wamama wanasema hawashiriki hata shughuli za kijamii kama misiba na harusi, shughuli za kiuchumi na wasichana hawaendi skuli siku za mwanzo wa hedhi jambo ambalo kwa sasa limepitwa na wakati”, aliongeza.

Aminata alisema wamewapatia visaidizi vya hedhi ikiwemo pedi maalumu ambazo hufuliwa na kuendelea kutumia hata miezi mingine.

Pedi hizi ni nzuri kwani unaweza hata ukatumia miaka minne mitano kwa kuwa ukimaliza unafuaa na kubadilisha nyengine sasa wanahudhuria masomo yao kama kawaida.

AFISA WA AFYA

Naye Ofisa Afya wa Mradi huo, kutoka hospitali kuu ya Mnazi mmoja, Nahya Khamis Nassor, alisema utafiti huo umepelekea uazinzishwaji wa program maalum inayotoa elimu kwa mtoto wa kike kutambua mabadiliko ya miili yao, afya na usafi wa mwili na matumizi sahihi ya vifaa vya hedhi pamoja na ugawaji wa taulo (pedi) na nguo za ndani za wasichana.

Alisema ufahamu wa baadhi ya wanajamii kuhusiana na suala zima la hedhi hususan Zanzibar, kumekuwa na mila na desturi ambazo zinakwamisha wasichana kujiamini na kutoshiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii.

 “Imani potofu hizo hupelekea mtoto wa kike kutohudhuria masomo na hatimaye matokeo yao ya masomo darasani kuwa mabaya wakati mwengine hufungiwa majumbani wakikatazwa kutoka kwa siku kadhaa pamoja na kutoonana na watu wanapokua katika siku za hedhi”, alisema Nahya.

Nahya aliongeza kuwa kutokana na imani hizo hupelekea wasichana wengi kushindwa kutimiza ndoto zao, kujihisi kuwa ni dhaifu wakati wana uwezo wa kuendelea na shughuli za kijamii na kuhudhuria masomo kama kawaida iwapo watatumia visaidizi vya taulo.

Lakini utafiti huo umebaini mambo matano yanayowapa wakati mgumu wasichana hasa Vijijini kama ukosefu wa elimu ya utambuzi kuhusiana na afya ya maumbile ya mtoto wa kike, ukosefu wa vyanzo vya maji vijijini kunawafanya watoto wa kike kushindwa kujisafisha vizuri wakiwa katika siku zao jambo ambalo si zuri kiafya.

“Ukosefu wa taulo za kujistiri, mtoto wa kike kushindwa kuhudhuria masomo siku tano au saba za kila mwezi kutokana na suala la maumbile ya hedhi na kujikuta hawafanyi vizuri katika masomo.

Pia kutokujiamini na kuichukulia ni hali ni ya kawaida katika maumbile ya mwanamke pamoja na hali duni ya maisha”, aliongeza.

Hata hivyo ansema kumuelimisha mtoto wa kike ni sawa na kuelimisha jamii nzima kwani mtoto wa kike hukua na kuwa ndiye mama katika familia kwa kujenga misingi imara ya kiafya.

Aidha alisema kuwa kujitambua ni jambo la awali ili kutokomeza imani potofu zilizo tawala katika jamii nyingi hususani maeneo ambayo bado hayajaendelea.

Ofisa huyo wa Afya anaeleza kuwa wakati umefika kwa sekta binafsi, Wizara dhamana za afya na vikundi mbali mbali katika jamii, kuunga mkono katika kadhia hii ili kutoa elimu maskulini, majumbani na hosptali ili kuboresha afya kwa wanawake na wasichana kwa jumla.

Nahya anabainisha kuwa mradi huo umesadia kuboresha mifumo ya maji na kuweka sehemu za utupaji taka katika skuli za Kijini na Matemwe Mbuyutende kwa kutoa elimu ya usafi wa afya na mazingira kwa wanafunzi wa kike ili kushiriki harakati za kijamii pamoja na kuhudhuria masomo kama iwapo watatumia pedi.

AFISA WA WANAWAKE NA WATOTO

Ofisa Idara ya Uwezeshaji wanawake na watoto Zanzibar, Mohamed Jabir, alisema taasisi binafsi kwa kushirikiana na serikali, zinapaswa kuunga mkono na kusadia kutoa elimu kwa wasichana kujitambua pamoja na kuwezesha upatikanaji wa visaidizi kwa gharama nafuu.

“Pamoja na jambo hili kuwa lipo chini ya Wizara ya Elimu lakini sisi kama idara ya wanawake na watoto tunaendelea kutoa elimu ya kujitambua kwa mtoto wa kike ili aondokane na dhana potofu, pia taasisi binafsi kwa kushirikiana na serikali, nazo zinapaswa kusadia kuwajengea ufahamu na maendeleo ya wanafunzi”, alisema Jabir.

Hata hivyo anatahadharisha na kutilia mkazo mazingira ya skuli kuhitaji kuwa rafiki hasa upatikanaji wa huduma ya maji katika vyoo ili kuwaondolea hofu wanafunzi wanapokuwa katika siku zao za hedhi pamoja na kupatiwa elimu ya afya ya kujitambua.

IDARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA AMALI

Kwa Upande wake, aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Maandalizi na Msingi Safia Ali Rijal, alisema elimu ya Afya ya kujitambua kwa wanafunzi jambo muhimu ili kuondokana na dhana potofu wanapokuwa katika hedhi na kuendelea na masomo kama kawaida.

Lakini alisema elimu inahitajika kuanzia ngazi ya familia ili kuiondoa imani hiyo potofu na mtazamo hasi kwa msichana anapokua katika ziku zake za hedhi ili kuachana na utamaduni uliopitwa na wakati na badala yake kuongeza kasi ya matumizi ya taulo kwa wanafunzi.

“Vifaa walivyopewa ni rafiki kwao na vitawasaidia sana kufikia malengo yao kwani elimu hii waliyopewa itawaondosha katika dhana potofu ya kwamba ukitumia utakosa kizazi au kupata maradhi, baada ya kupewa vifaa wengi wamefurahi sasa wanahudhuria masomo yao”, alisema.

BARE FOOT INTERNATIONAL

Pendo Yaride Sambayi, ambae ni mratibu wa kituo cha mafunzo ya kazi za mikono cha Bare Foot Collage International kilichopo Kinyasini Mkoa wa Kaskazni Unguja, alisema walipata tenda ya kutengeneza taulo zakike (pedi) ambazo zinasaidia sana kujistiri wasichana na wanawake wakiwa katika hedhi.

“Tunashona kwa ustadi mkubwa baada ya kupatiwa mafunzo India tunaweka kama vitambaa vitatu na aina ya pamba na kwamba hata kama itaroa sana haiwezi kuvujisha”, alisema.

Alisema pedi hizo zina uwezo wa kudumu hata miaka 10 iwapo watumiaji watakuwa nadhifu kwa kuwa baada ya matumizi kidogo tu mtu analazimika kuzifua na kuzianaika.

“Akimaliza matumizi tu anatakiwa kuzifua na kuziweka nadhifu sehemu ya kikoba maalumu tunachompa na pedi kwa kweli tumemwagiwa sifa nyingi husaidia wasichana wengi kuhudhuria masomo kuliko awali”, alisema.

Pendo, alisema kifuko kimoja chenye pedi huwemo nne na zinauzwa kwa shilingi 10,000, hata hivyo watu wa vijijini alisema hupunguziwa bei.

Pamoja na kuwepo kwa wanafunzi wenye uelewa katika matumizi ya taulo lakini tatizo la umasikini ni miongoni vikwazo kwa familia ambazo zimekuwa zikishindwa kumudu gharama za kununua pedi hasa katika mazingira ya vijijini.

Zipo bei tofauti za taulo za kujistiri (pedi) kama za free style, Rosemarry, Always nakadhalika ambazo huuzwa kati ya shilingi 1,500 nyegine 2,500 mpaka 10,000 ndani yake zikiwa nane hadi 10 wakati za shilingi 10,000 zikiwa 40 kutokana na umasikini baadhi ya familia zinashindwa kumudu.

Hata hivyo, baada ya kupatiwa elimu juu ya suala la hedhi salama na matumizi ya pedi zilizotolewa na mradi wa Best of Zanzibar, hivi sasa wanafunzi hao wanafurahia matumizi ya taulo za kike (pedi) na walisema ni rafiki sana kwao.

Program ya kusadia elimu ya usafi wa afya na mazingira katika skuli za msingi na sekondari katika kijiji cha Kijini na Matemwe na Mbuyutende kupitia mradi wa Best of Zanzibar, unafadhiliwa na Kampuni ya Panroyal Limited pamoja na kuwapatia masomo ya ziada wanafunzi wa sekondari kwa lugha ya Kingereza, Hisabati na sayansi ili kuinua viwango vyao kitaaluma naufaulu katika skuli hizo.

Mradi huo umewasaidia sana wanafunzi wazazi na walimu juu ya uelewa wa hedhi salama, jambo ambalo kwa sasa wamehamasika na kuachana na mila potofu na kuhudhuria masomo yao skuli kama kawaida.

CAP

OFISA afya kutoka mradi wa Best of Zanzibar, akitoa elimu ya hedhi salama kwa wanafunzi wa kike huko skuli ya Kijini Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja, namna ya kutumia vifaa vya hedhi (pedi) kwa wanafunzi hao.

&&&&&&&&&&&&&&

BAADHI ya wanawake na wasichana wa kijiji cha Mbuyutende Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja wakizungumza na makala haya namna ya mtazamo wa hedhi kwa wasichana na wanawake wa kijiji hicho.