NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema anapata faraja kila anapoiona miradi ya wananchi inayosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), inasaidia kuwapunguzia umasikini wananchi.

Hemed alieleza hayo jana wakati alipofanya ziara ya kukagua miradi ya wananchi inayotekelezwa kupitia TASAF ikiwemo shamba la upandaji wa miti na mboga huko Kitogani, shamba darasa la wanakaya wa kijiji cha Kizimkazi Dimbani na mradi wa bwawa la ufugaji na umwagiliaji la wakaazi wa Mtende.

Makamu huyo alisema serikali imebuni mfuko wa TASAF ili usaidie miradi ya wananchi ikiwa na lengo la kupunguza umasikini jambo ambalo limeleta mafanikio makubwa.

Alifahamisha kuwa maendeleo ya miradi ya wananchi inayosimamiwa na TASAF inamtia moyo kwa kiasi kikubwa na kwamba mfuko huo umekuwa daraja linalowaunganisha wananchi katika kupambana na umasikini.

“Miradi ya jamii inayotekelezwa na wananchi kupitia mfuko wa TASAF hapa nchini Tanzania, imesaidia kupunguza ukali wa maisha hasa kwa wananchi wa kaya masikini”, alisema.

Makamu huyo alisema kutokana na kasi ya maendeleo ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini, viongozi wa mikoa na wilaya wanapaswa kutafakari njia za kuzingatia upatikanaji wa soko la ushindani kwa bidhaa zinazozalishwa na wananchi.

Hemed aliviagiza vyombo vya ulinzi vishirikiane na vikundi shirikishi ili kudhibiti uzoroteshaji wa kesi za wahujumu wa miradi ya jamii kwa vile wahalifu si watu wanaopaswa kufumbiwa macho.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wananchi hao kwamba serikali kupitia mikoa, wilaya na shehia kwamba itaendelea kutafuta njia muafaka itakayokidhi mahitaji ya wananchi hao katika kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakwaza.

Mapema hapo jana Makamu wa Pili wa Rais, alikutana na uongozi na watendaji wa TASAF kanda ya Unguja hapo Mazizini ambapo alisema Zanzibar lazima iendelee kubakia kuwa mfano bora wa utekelezaji wa miradi ya mfuko huo.

“Nategemea kipindi hichi cha pili katika TASAF ya awamu ya tatu kitakuwa mfano mzuri mno”, alisema Makamu huyo ambaye pia ni mkuu wa shughuli za serikali.

Alisema kwa vile watendaji hao wamepewa jukumu la kuwahudumia wananchi  wanyonge hawana budi kuendelea kuwa waaminifu  kama walivyofanya katika TASAF awamu za vipindi vilivyotangulia.

“Wananchi lazima waendelee kuwezeshwa kwa vile Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania ni muhimu kwa kubadilisha maisha yao”, alisisitiza Hemed.

Alieleza umuhimu wa kuendelea kuzingatiwa matumizi bora ya fedha za serikali Mfuko wa Tasaf ikiwa miongoni mwake kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi anavyotilia mkazo jambo hilo.

Akitoa taarifa fupi mratibu wa TASAF Unguja, Makame Ali Haji alisema utekelezaji wa TASAF awamu ya tatu kipindi cha pili tayari imeshaanza kwa hatua ya uhakiki wa wanakaya wapya watakaoingizwa kwenye mradi huo.

Makame alisema jumla ya kaya 34,962 zimeandikishwa katika zoezi la awali ikiwa ni sawa na asilimia 85 na limepangwa kukamilika rasmi ifikapo Mwezi Januari Mwaka ujao unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa Wiki hii.