Atoa siku tatu kuondolewa mchele mbovu

NA HAFSA GOLO

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla, amesema serikali haipo tayari kumvumilia ama kumuonea muhali mfanyabiashara yoyote anayeingiza vyakula vibovu nchini.

Akizungumza na viongozi na watendaji wa Shirika la Bandari Zanzibar, alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo na kugundua   kuwepo kwa shehena ya mchele mbovu ulioingia nchini tangu mwezi Machi mwaka jana ambapo hadi sasa hakuna uamuzi wa kisheria uliotekelezwa.

Alisema lazima kila mfanyabiashara ahakikishe anafuata matakwa ya kisheria ya uingizaji wa bidhaa nchini na vyenginevyo mamlaka husika isisite kumnyang’anya kibali.

Aidha alisema, serikali inahitaji kuona wafanyabiashara wote wanajali usalama wa maisha ya watu, wanaheshimu na kutii miongozi ya sheria na sio kuangalia maslahi yao binafsi.

Alisema, serikali haiwezi kuona wananchi wake wanapata maradhi kwa sababu ya kutumia vyakula vibovu vinavyoingizwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu huku viongozi wenye dhamana kushindwa kuchukua hatua za kisheria kwa kisingizio cha kuogopana.

“Lazima tusimamie usalama wa wananchi wetu na viongozi muondokane na tabia ya kuoneana muhali kwani hatuwezi kwenda katika hali ya kumuhofia mtu,” alisisitiza Hemed.

Katika hilo, Hemed aliwahakikishia wananchi wa Zanzibar kwamba iwapo serikali itabaini katika tukio hilo yupo mtendaji ama kiongozi amehusika na ucheleweshaji wa kuchukuliwa hatua, haitosita kuchukua nafasi yake na kumuwajibisha.

Hivyo Makamu huyo aliagiza kupatiwa nyaraka zote zinazohusiana na mwenendo mzima wa uingiaji wa mchele huo na hatua zilizoanza kuchukuliwa ili kuona sababu zilizochangia ucheleweshaji wa maamuzi juu ya hilo.

Mbali na agizo hilo, aliwataka wafanyakazi wa Shirika hilo kutokubali kukaa kimya wanapobaini uwepo wa bidhaa mbovu imeingizwa nchini, kwani kufanya hivyo ni uzalendo sambamba na kutimiza azma ya serikali. 

Aidha Hemed aliagiza kuondolewa kwa shehena hiyo ndani ya siku tatu na viongozi wahakikishe wamefuata maelekezo ya sheria.

Alipotoa fursa kwa wafanyakazi kueleza changamoto zao wakati wa ziara hiyo, mmoja ya wafanyakazi wa shirika hilo, mzee Panga Manyepa, alisema mbali na bidhaa hiyo zipo bidhaa nyengine ambazo zimepitwa na muda wa matumizi.

Kufuatia ombi hilo, Hemed aliagiza kutengwa siku maalumu ndani ya wiki hii ya kusikiliza kero na malalamiko ya wafanyakazi ili serikali iyafanyie kazi ichukue hatua.

Naye Mkurugenzi Idara ya Udhibiti Usalama wa Chakula, Khamis Ali Omar, alisema kwa mujibu wa sheria namba 2 mwaka 2006 na marekebisho ya sheria namba 3 ya mwaka 2017 inamtaka mfanyabiashara kurejesha bidhaa mbovu inakotoka ama kuiteketeza.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Shirika la Bandari Masoud Haji alimueleza Makamu kwamba yapo malalamiko mengi kwa wafanyakazi wa shirika hilo ya ukosefu wa maslahi yao na haki stahiki jambo ambalo linachangia kutofikia ufanisi na malengo ya serikali.