Aagiza kusimamishwa kazi ofisa aliyedharau wito

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amemuagiza katibu mkuu wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto kumsimamisha kazi ofisa wa Idara ya Ustawi wa Jamii aliyedharau wito.

Makamu huyo alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara fupi ya kukagua mradi wa ujenzi wa majengo ya watoto yatima huko Jumbi wilaya ya Kati, ambapo alipofika katika eneo hilo hakukuta ofisa yoyote wa idara hiyo licha ya kupewa taarifa ya ziara hiyo.

Ofisa huyo ambaye Makamu wa Pili wa Rais aliagiza kusimamishwa kazi anahusika na dhamana ya utoaji wa vibali kwa ajili ya uendeshaji wa huduma za watoto yatima.

Hemed alisema kitendo cha mtumishi huyo wa umma kushindwa kuitikia wito kimeonesha dharau hasa ikizingatiwa kuwa hadi anamaliza ziara katika eneo hilo hakuna sababu yoyote iliyowasilishwa kwa nini ameshindwa kuitikia wito.

Alisema haiwezekani kuona watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa mfumo wa kufuata mazoea, huku taasisi, jumuiya na baadhi ya mashirika ya kiraia yakionesha kusaidia nguvu katika uwezeshaji wa hifadhi ya watoto waliopoteza wazee wao.

Katika ziara hiyo, Makamu wa Pili, alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja kulifuatilia suala la ucheleweshwaji wa upatikanaji wa kibali kwa ajili ya uendeshaji wa huduma za watoto yatima katika majengo hayo ya Jumbi na lazima kipatikane mara moja.

Akizungumza na wasimamizi wa mradi wa ujenzi huo mara baada ya kuutembelea, Hemed alisema watumishi watakaopewa jumuku la kuwahudumia watoto yatima lazima wawe makini na kuwaepusha watoto hao na wimbi la vitendo vya udhalilishaji.

Alisema watoto yatima wanahitaji matunzo mazuri na uangalizi utakaowapa faraja ya kujihisi kama wenzao, mfumo utakaohitaji kwenda sambamba na haki zao zote zinazowajibika kuzipata katika mazingira yao.

Hemed alisisitiza umuhimu wa kuzingatia mazingira ya usafi ndani ya majengo hayo ili watoto wote waendelee kuishi kwa amani, afya na upendo.

Awali msimamizi wa mradi huo wa ujenzi Mohammed Mansour alisema makaazi hayo yatahudumia watoto yatima 15, wanawake wanane na wanaume na watakuwepo walezi wao.

Mohammed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, kwamba kasi ya ujenzi wa majengo hayo inaendelea vizuri kwa lile la ghorofa moja nyumba ya mwalimu, sehemu ya kuishi walezi wawili, sehemu ya jiko na mahali maalum pa kulia.

Naye Zainab Ali kutoka ubalozi wa Kuwait nchini Tanzania, alisema uongozi wa kituo hicho umezingatia watu watakaoajiriwa katika kazi hiyo tayari wana uzoefu wa kina katika huduma za usimamizi wa malezi kwa vile tayari wameshastaafu.

Zainab alisema ujenzi wa mradi huo umetokana na michango ya wananchi wa Kuwait waliojiwekea utaratibu wa kusaidia makundi ya watu wakiwemo watoto yatima na wazee wasiojiweza.

Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, katika kukagua mradi huo wa ujenzi wa makaazi ya watoto yatima katika kijiji cha Jumbi imekuja baada ya kupata taarifa ya wasimamizi wa kituo hicho kuzungushwa katika upatikanaji wa kibali cha kuendesha kituo.