NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman amesema kuna umuhimu kwa wataalamu kutafuta suluhisho litakalosaidia kuondokana na mmongo’onyoko wa ardhi unaosababishwa na nguvu za maji ya bahari.

Hemed alieleza hayo jana huko ofisini kwake Vuga mjini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, anayesimamia muungano na mazingira wa serikali ya Jamhuri, Ummy Ally Mwalimu.

Alisema maeneo kadhaa ya Zanzibar yanayokabiliwa na athari za kimazingira kutokana na nguvu za maji ya bahari, ambapo hali hiyo inatokana na mabadiliko ya tabianchi.

Makamu huyo alisema miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa sana na athari za nguvu za bahari ni katika kijiji cha Sipwese kilichopo Mkoa wa Kusini Pemba, na kueleza kuwa wataalamu lazima wachukue nafasi kuhakikisha athari hizo zinaondoka.

Alisema wananchi wa kijiji wanapata usumbufu kutokana na sehemu wanayovuka kwenda upande wa vijiji jirani kuvamiwa na mmong’onyoko mkubwa wa ardhi unaosababishwa na kasi ya maji ya bahari, ambayo pia inahatarisha maisha.

Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti kutoa ushirikiano katika kuona kero hiyo inayowakabili wananchi wa Sipwese inapatiwa ufumbuzi kama ilivyoshughulikiwa changamoto ya athari ya tabia nchi iliyokikumba Kisiwa Panza.

Katika hatua nyengine, Makamu huyo alieleza kwamba yapo matumaini ya kuendelea kuimarika kwa muungano wa Tanzania kutokana na marais wote kuwateuwa mawaziri madhubuti wenye nguvu ya kusimamia masuala ya muungano.

Alisema hana shaka ya mawaziri hao walioonesha matumaini mema kwa kuanza kusimamia vikao vya wataalamu na viongozi wa pande hizo mbili kuyaangalia maeneo ambayo yana dalili za changamoto za muungano kwa pande zote mbili.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza waziri Ummy kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo ambayo pamoja na mambo mengine inahusika moja kwa moja na masuala ya muungano.

Awali waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia muungano na mazingira, Ummy Ally Mwalimu alisema wizara yake imepewa jukumu la kuratibu masuala ya muungano na mazingira.

Waziri huyo alisema wanapaswa kuimarisha masuala ambayo yako nje ya muungano lakini yanajumuisha moja kwa moja miradi ya maendeleo inayotekelezwa upande wa Zanzibar ambayo inapata dhamana ya serikali ya Jamhuri.

Ummy alielezea faraja yake kutokana na wataalamu na viongozi waandamizi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanza majadiliano katika utekelezaji wa changamoto zilizopo kwenye sekta ya mazingira.

Awali waziri Ummy alikutana na kufanya mazungumzo na waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid Salum Mohammed.

Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Vuga Mjini Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohammed alisema pande hizo mbili zinapaswa kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika taasisi za kiutendaji badala ya kusubiri kutatua kero za muungano.