IWAPO ulikuwa hufahamu kwamba tabia ya mtoto kwa kiasi kikubwa hutegemea namna tunavyomlea basi hii ni habari kwako.

Badala ya makatazo na makaripio mbalimbali toka vinywani mwetu kuhusu miendendo ya watoto, hebu tujaribu kuwatia moyo.

Wataalamu wa makuzi ya watoto wanakubaliana kwamba kutia moyo ni njia chanya inayolenga hasa kwenye kuboresha tabia ndogondogo, badala ya kusubiri matokeo na kuanza kugomba.

Kutia moyo ni kutambua, kukubali, na kuwasilisha imani kwa mtoto katika mambo madogomadogo bila kusubiri afikie ‘ubora ili umtambue. Namna hii mtoto anapata faraja kujua kwamba unamjali naye atajitahidi ‘kutokukuangusha.’

Moja ya mafanikio ya aina hii ya malezi ni uwezo wa kutenganisha makosa na mkosaji, hivyo hapa hakuna kitu kama mtoto ‘mzuri’ au mtoto ‘mbaya.’ Hii ni njia bora katika ujenzi wa tabia ya mtoto kwani nafsi yake hutenganishwa na matendo yake.

Anapofanya mema, mema husifiwa na anapokosea, mabaya huambiwa pia. Mtaalamu na mbobezi katika magonjwa ya akili ndugu Rudolf Dreikurs, anasisitiza kuwa watoto wanahitaji kutiwa moyo ‘mithili ya mti unavyohitaji maji.’

Kumtia moyo mtoto kamwe hakupaswi kuchanganywa na sifa, yaani kumsifiasifia mtoto. Hasha. Kumsifia mtoto mara nyingi huwa na matokeo hafifu katika kujenga tabia, ikilinganishwa na njia ya kumtia moyo! Muhimu hapa ni kujua kuwa sifa.

Mara nyingine humfanya mtoto ‘kujiona mjuaji’ ‘keshafika’ na aina nyingine za ‘kudhani’ kwani ndivyo mzazi/mlezi anavyompamba. Lakini unapomtia moyo, taratibu mtoto hujijenga huku akijua kuwa juhudi zake zinasaidia kupata matokeo bora kitabia.

Tunachosema hapa ni kwamba bahati mbaya, mara nyingi sifa hutolewa kwa mtoto anayeonekana ‘kufanikiwa’ hata kama hatujui ‘mafanikio yake kayapataje.’ Namna hii tunamnyima fursa mtoto ‘anayejikongoja’ katika kuelewa na kujifunza mambo.

Malezi yaliyojengwa katika kutia moyo yanajikita katika kanuni kwamba ‘tabia njema hutuzwa; tabia mbaya hupuuzwa.’ Kwamba tabia njema inapotuzwa mara kwa mara hukua, na tabia mbaya inapokemewa mara nyingi hufa. Iwapo tunakubaliana katika hili, basi ni wazi kuwa wazazi/walezi wanapaswa daima kuwa waangalifu ili kuziona tabia njema za watoto wao. Ieleweke kuwa tabia nzuri za watoto zipo tele; ila tatizo lipo kwetu wazazi kwani hatuzioni.

Badala yake, wazazi wengi tunaziona tabia mbaya za watoto wetu, ambazo kila mara huzikemea kwa matumaini kwamba namna hii watoto watajifunza nidhamu.

Malezi ya kutiana moyo huwasaidia watoto kujifunza kujithamini na pia kuthamini kila wanachokifanya. Hatua kwa hatua. Hii inatoa fursa kwa wazazi kuzielezea hisia zao juu ya tabia za watoto wao.

Kwamba badala ya kuangalia makosa ya mtoto, mzazi anapata fursa ya kuziona juhudi za mwanae katika kujijenga kitabia huku akitoa sifa stahiki na kumtia moyo pale anapojikwaa.

Kwa maoni na ushauri tupigie simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto nchini. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile unaweza kutupata kupitia ukurasa wetu wa Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania na www.sematanzania.org