Na Ali Shaaban Juma

NOTI ni pesa halali iliyoidhinishwa na Benki Kuu ya taifa husika kwa ajili ya kutumika kama malipo halali ya ununuzi wa bidhaa au huduma yenye thamani ya pesa hizo. Kwa tafsiri hiyo, noti hutumika kulipia madeni fulani anayodaiwa mtu, shirika, kampuni, taasisi au serikali.

Matumizi ya noti yameanza duniani karne kadhaa zilizopita ambapo hapo awali malipo ya vitu vikubwa vyenye thamani yalifanyika kwa kubadilisha bidhaa hizo kwa madini kama vile dhahabu na fedha.

Lakini kutokana na kutokuwepo kwa usalama wa mtu au wafanyabiashara kusafiri masafa marefu na madini hayo ndipo zilipoanzishwa noti ambazo zilitumika kama mbadala wa madini.

Hivyo basi kuanzia wakati huo, wafanyabiashara ambao walikuwa wakichukua  vipande vya dhahabu ili kubadilisha kwa bidhaa nyenginezo walianza kusafiri na noti ili kulipia bidhaa fulani.

Kihistoria, noti zilianza kutumika katika jimbo la Sichuan nchini China katika karne ya saba wakati wa utawala wa Tang na Song. Noti hizo zilianzishwa kwa vile baadhi ya wafanyabiashara wakati huo walikuwa wakisafiri masafa ya mbali na kubeba mzigo mkubwa wa pesa za mapeni ya shaba (sarafu) kununulia bidhaa mbalimbali.

Wafanya biashara wakubwa waliwaruhusu wanunuzi walobeba pesa hizo kubadilisha kwa kuwapa karatasi maalum ambayo thamani yake ilikuwa ni sawa na pesa za shaba (mapeni) alizoweka.

Katika karne ya 11, kundi la wafanyabiashara wakubwa wa China walichapisha aina fulani ya noti zilizoitwa “Jiao Zi” zilizobadilishwa kwa bidhaa na kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadae. Noti hizo zilikuwa  na alama mbalimbali kuepuka kughushiwa.

Benki  ya kwanza kuanzishwa duniani ilianzishwa nchini Uingereza katika mwaka 1694  na kuitwa Bank of England ili kuchangisha pesa kusaidia jeshi la Mfalme  William wa Tatu wa taifa hilo dhidi ya vikosi vya Ufaransa.

Ghalfa benki hiyo ikaanzisha utaratibu wa kupokea pesa na kutoa mikopo ambapo aliyeweka pesa alilipwa pesa hizo muda wowote alipozihitaji pesa zake. Hapo awali karatasi za noti ziliandikwa kwa mkono na kutiwa saini na mshika fedha wa benki.

Taratibu matumizi hayo ya noti yalisambaa duniani ambapo Waingereza, Wafaransa, Wareno na Wahispania walichapisha noti mbalimbali kwa ajili ya matumizi katika makoloni yao. Pia noti zilichapishwa huko barani Ulaya na Marekani  na hivyo kuwa ni mfumo wa malipo uliokubalika duniani ambapo huduma na bidhaa zililipiwa kwa noti hizo katika eneo la nchi noti hizo zinapotumika.

Noti nyingi zinazotumika hivi sasa duniani hutengenezwa kwa karatasi maalum itokanayo na pamba na huwa na uzito wa kati ya gramu 80 hadi 90. Hakuna kipimo maalum cha urefu na upana wa noti, bali noti zote duniani huwa na urefu na upana unaolingana. Lakini baadhi ya noti huwa na urefu na upana wa aina moja.

Kwa mfano nchi ya Jamaica ina noti za Dola 50, 100, 500, 1,000 na 5,000 ambapo noti zote hizo zina urefu wa Milimita 145 na upana wa Milimita 68.

Noti za Tanzania za Shilingi 10,000, 5,000, 2,000 na shilingi 1,000  zinatofautiana urefu, lakini zote zina upana unaolingana wa Sentimita 7.5.

Noti ya Shilingi 10,000 ina urefu wa Sentimita 15 na upana wa Sentimita 7.5. Noti ya Shilingi 5,000 ina urefu wa Sentimita 14.5 na upana wa Sentimita 7.5 ambapo Noti ya Shilingi 2,000 ina urefu wa Sentimita 14 na upana wa Sentimita 7.5 nayo Noti ya Shilingi 1,000 ina urefu wa Sentimita 13.5 na upana wa Sentimita 7.5.

Pia karatasi inayotengenezewa noti huchanganywa na aina fulani ya nyuzi za kitambaa ziitwazo linen au nyuzi za mmea uitwao Acaba unaotengenezewa kamba. Mti huo unapatikana kwa wingi  katika nchi za  Philippines, Ecuador, na Costa Rica.

Tofauti na aina nyengine za karatasi ambazo huroana, huchafuka na huregea kwa urahisi zinaposhikwashikwa, mchanganyiko wa karatasi za pamba na nyuzi za linen na Acaba hudumu kwa muda mrefu na kuifanya noti iliyotengenezwa kwa mchanganyiko huo wa karatasi  kutoboba  kirahisi inaporoa  au  kuingia katika maji. 

Kwa kawaida karatasi zinazotumiwa kuandikia maofisini, mashuleni na magazeti  hutengenezwa kiwandani kwa kuchanganywa maji na unga wa karatasi unaotokana na miti.  Lakini noti zinapochapishwa kiwandani ambazo ni mchanganyiko wa karatasi za pamba pia huchanganywa na aina fulani ya kemikali iitwayo gelatin ili kuifanya noti hiyo idumu kwa muda mrefu.

Kwa sababu za kiusalama, pia noti za benki ambazo wastani wa  muda wake wa matumizi bila kuharibika ni miaka miwili, hutiwa alama maalum zinazong’ara katika mwangaza na kiza ambazo kitaalamu huitwa watermark.

Alama hizo ambazo hujificha katika noti, huonekana kwa kuigeuza geuza noti hiyo katika mwangaza na alama hizo hujidhihirisha kwa kubadilikabadilika rangi kutokana na vile noti hiyo unavyoigeuza. Lengo kuu la alama hizo ambazo hutofautiana katika noti za nchi mbalimbali ni kuepusha uwezekano wa kughushiwa noti hizo kwa urahisi. 

Kitu chengine ambacho huonekana katika noti ni aina fulani ya uzi uliojificha ambao kwa sababu za kiusalama uzi huo huonekana upande mmoja tu wa noti hiyo.

Utaalamu huo wa kuingiza uzi katika noti ulivumbuliwa mwaka 1896 na kampuni ya De La Rue ya Uingereza inayoongoza kwa kuchapisha noti duniani.

Kampuni hiyo  ya De La Rue ya Uingereza ndiyo inayochapisha noti za nchi nyingi duniani zikiwemo pesa za Armenia, Barbados, Belize, Uingereza, Fiji, Guatemala na Honduras. 

Nchi nyengine ambazo kampuni hiyo inachapisha pesa zao ni Iraq, Visiwa vya Man, Jamaica, Kenya, Kuwait, Macedonia, Visiwa vya Meldives, Scotland, Sir Lanka, Tanzania na Benki ya Jumuiya ya Ulaya.

Mbali ya hayo, pia   noti hupakwa aina fulani ya gundi laini mithili ya palastiki ili kuifanya noti hiyo isikunjane katika pembe zake nne kama inavyokunjana karatasi ya kawaida ambapo gundi hilo pia hupunguza uwezekano wa kuikopia noti hiyo.

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, aina mpya za noti zinazotengenezwa kwa kutumia plastiki iitwayo polimer zimeanza kutumika katika miaka ya hivi karibuni.

Noti zilizotengenezwa kwa palastiki ya polimer ziko salama zaidi kuliko zile zilizotengenezwa kwa kutumia karatasi za pamba. Vilevile noti za polimer zinadumu muda mrefu zaidi kuliko noti za kawaida na hivyo kupunguza athari ya uchafuzi wa mazingira na gharama za kuchapisha noti nyengine mpya mara kwa mara.

Kwa mara ya kwanza noti hizo zilichapishwa nchini Australia katika mwaka 1988, kufuatia utafiti wa kina ulofanywa na Benki Kuu ya Australia, Chuo Kikuu cha Melbourne na Shirika la Utafiti na Sayansi la Jumuiya ya Madola.

Noti za mataifa yote duniani zina vielelezo vikuu Banknote Identities ambavyo hutambulisha utaifa wa nchi hiyo na mtizamo wa Benki Kuu ya taifa hilo kwa watumiaji wa noti hizo.

Vielelezo hivyo ni pamoja na vielelezo vya pekee, vielelezo vya kitaifa, vilelezo vya jumla, vielelezo vya kitamaduni na vielelezo vya kimtizamo wa pamoja.

Kwa mfano ukiziangalia noti za Tanzania za Shlingi 10,000, 5,000, 2,000 zote zina vitu vinavyolingana upande wa mbele na nyuma.

Upande wa mbele wa noti zote hizo, kuna tarakimu na maneno ya thamani ya pesa hiyo na uzi unaong’ara ulioko upande wa kushoto wa pesa hizo.

Pia kuna jina la Benki Kuu, Nembo ya Tanzania, Nambari zenye tarakimu saba zilizoanza na irabu mbili. Katika noti zote za Shilingi 10,000, 5,000 na 2,000, nambari hizo zimeandikwa kwa kulala (horizontal) kwa wino mweusi upande wa kushoto na kuandikwa kwa kusimama (vertical) kwa wino mwekundu upande wa kulia.

Kitu chengine ambacho kinajitokeza juu ya nambari nyeusi za kushoto katika noti zote hizo ni alama ya “V” iliyoelekea chini mithili ya tepe za askari ambapo katika 10,000 kuna alama hizo tatu, alama mbili katika noti ya 5,000 na alama moja katika noti ya 2,000, alama zote hizo zina rangi ya mji (Background) ya noti husika.

Vitu vyengine vinavyonekana mbele ya noti hizo ni Mnyama anayewakilisha mali asili ya taifa na kuandikwa kwa Kiswahili ambayo ni lugha ya taifa. Pia kuna saini ya Gavana wa Benki Kuu na Waziri wa Fedha.

Si hayo tu, bali pia unapoziangalia katika mwangaza, upande wa kushoto wa noti zote hizo za Shilingi 10,000, 5,000 na 2,000 kuna picha ya Mwalimu Nyerere na tarakimu ya thamani ya noti hiyo alama ambazo zimejificha.

Upande wa nyuma wa noti hizo kuna majengo, alama ya Twiga na kuandikwa kwa Kiingereza jina la benki na thamani ya noti hiyo. Tofauti na upande wa mbele wa noti hizo ambao kuna michoro ya msumeno katika pembe mbili za noti hizo, unapogeuza nyuma noti hizo misumeno hiyo imejificha na huonekana pale unapoangalia noti hiyo katika mwangaza. Hivyo ni baadhi tu ya vielelezo ambavyo vinaonekana katika noti za Tanzania.

Hata hivyo utafiti ulofanywa na Mtandao wa Golobos kwa noti zote 157 zinazotumiwa duniani umeonesha kuwa asilimia 23 ya noti zote duniani zina rangi ya kijani ambapo picha za wanaume zinaonekana katika asilimia 93 ya noti zote ulimwenguni.

Picha za wanasiasa ni asilimia 39 ya picha zilizomo katika noti zote ulimwenguni ambapo asilimia 12 ya noti hizo za dunia zina picha za majengo ya Kasri za Kifalme au Ikulu. Ndege ambaye ametumika katika noti nyingi ulimwenguni ni Kipanga ambaye yumo katika asilimia 12 ya noti hizo za dunia.

Hata hivyo, mbali ya vielelezo hivyo, lakini pia noti nyingi hasa za bara la Afrika na Asia zimetumia picha za baadhi ya  wanyama ambao wanaonekana katika noti za mataifa mbalimbali.

Kwa mfano picha ya Simba iko katika Randi 50 ya Afrika ya Kusini, Faranga 20 ya Congo DRC, Dola 100 ya Hong Kong, Emalangeni 100 ya Swaziland, Kwacha 5,000 ya Zambia na Shilingi 2,000 ya Tanzania. 

Picha ya Tembo iko katika Randi 20 ya Afrika ya Kusini, Franga 100 ya Congo DRC, Franga 100 ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Shilingi 10,000 ya Tanzania, shilingi 500 ya Uganda pamoja na Dola 1,000 ya Zimbabwe.

Picha ya Nyati iko katika Shilingi 500 ya Tanzania ambayo kwa sasa haitumiki na katika Randi 100 ya Afrika ya Kusini.

Picha ya Kifaru iko katika Rupia 900 ya Sir Lanka, Franga Tano ya Congo DRC, Shilingi Elfu Tano ya Tanzania na Randi Kumi ya Afrika ya Kusini.

Vielelezo hivyo huingizwa katika noti kwa kuzingatia aina na mtazamo wa  watumiaji wa noti hizo. Pesa zote duniani zina watumiaji wa aina mbili ambao ni watumiaji  mmoja mmoja  na watumiaji wa jumla. Watumiaji mmoja mmoja ni watu wa kawaida ambao hutumia fedha hizo kwa matumizi ya reja reja ya kila siku. Watumiaji wa jumla ni serikali ambayo matumizi yake ni ya jumla ndani na nje ya taifa hilo.

Kwa mfano visiwani Zanzibar, serikali hutumia pesa za jumla kulipia mishahara wafanyakazi wake au kulipia miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara. Vilevile ifahamike kuwa watumiaji wa noti au pesa hizo ni raia wa nchi hiyo na wageni ambapo pesa za nchi fulani zinaweza kuchukuliwa na kutumika nje ya mipaka ya taifa husika.

Kwa mantiki hiyo, Benki Kuu za nchi zote duniani zinapochapisha noti huzingatia mambo yote hayo ikiwepo  pia usalama wa noti hizo na mahitaji halisi ya mzunguko wa pesa hizo katika matumizi.

Ubunifu  wa  michoro ya  rangi, nakshi, mtindo wa maandishi, picha  na maingiliano ya rangi katika noti ni kitu chenye kuleta  mvuto wa muonekano wa noti hiyo kwa watumiaji.

Kisaikolojia vielelezo vya noti vilivyochorwa vizuri na kuvutia huacha kumbukumbu ya taifa hilo kwa mtu aliyeiona, aliyeitumia au anayetumia noti hiyo.

Noti ya Randi Hamsini ya Afrika ya Kusini yenye  picha  ya  Simba

Noti ya Kwacha Elfu Tano  ya Zambia  yenye  picha  ya  Simba

Noti ya  Shilingi Elfu Mbili  ya Tanzania  yenye  picha  ya  Simba

Noti ya  Franga Ishirini  ya Congo DRC  yenye  picha  ya  Simba

Noti ya  Randi Kumi ya Afrika ya Kusini  yenye  picha  ya  Kifaru

Noti ya  Shilingi Elfu Tano ya Tanzania  yenye  picha  ya  Kifaru

Noti ya  Franga Tano ya Congo  yenye  picha  ya  Kifaru

Noti ya  Randi Ishirini  ya Afrika ya Kusini yenye  picha  ya Tembo

Noti ya  Franga Mia moja ya  Congo DRC yenye  picha  ya Tembo

Noti ya  Shilingi Elfu Kumi ya Tanzania yenye picha ya Tembo