Watanzania waungana na wenzao duniani kusherehekea siku hiyo

NA MARIA INVIOLATA (DSM)

WAKRISTO kote duniani hii leo wanaadhimisha siku kuu ya Krismasi, siku ambayo wanakumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristu mjini Bethlehem.

Wakati mamilioni ya watu duniani kote wakisherehekea msimu wa huu wa Sikukuu, karne kadha zilizopita baadhi ya Wakristo walipiga marufuku kusherehekea siku ya Krismasi.

Kulikuwepo wakati ambapo Waingereza waliona haja ya kudhibiti shughuli ambayo waliiona imekuwa kinyume na mafundisho ya Kikristo.

Kila Desemba, ilikuwa imeanza kuwa kawaida kwa watu kutekwa na hisia na msisimko, na kujihusisha na matendo ambayo hayakufuata mafundisho ya dini.

Kunywa pombe kupita kiasi, mkusanyiko wa watu wengi wanaopiga kelele za shangwe, biashara kufungwa mapema, familia na marafiki kujumuika pamoja kwa ajili ya chakula maalum cha sikukuu, nyumba kupambwa kwa miti na hata mitaani nyimbo za Krismasi kutawala.

WAKRISTO WA KWELI

Mwaka 1644, walokole wa Kiprotestanti nchini Uingereza ambao walifahamika kama Puritans walinuia kuifuta kabisa sikukuu ya Krismasi.

Walikuwa ni kundi ya Wakristo waliokuwa na msimamo mkali na walipigania kutekelezwa kwa mafundisho ya dini kikamilifu.

Serikali ya wakati huo ilikuwa ya Puritan na waliitazama Krismasi kama sikuu ya watu wasiokuwa na dini, au wapagani).

Waliamini kwamba hakukuwa na pahala popote kwenye Biblia ambapo ilikuwa imeandikwa au kudokezwa kwamba Yesu Kristo alizaliwa 25 Desemba.

Mbona basi tarehe hiyo ilikuwa inasherehekewa kama siku ya kuzaliwa kwa Yesu? Hawakufurahishwa na hilo.

Sherehe zote za krismasi zilipigwa marufuku Uingereza hadi kufikia mwaka 1660.

Tarehe 25 Desemba, maduka yote yalilazimishwa kuwa wazi, na makanisa yakashurutishwa kufunga milango yao.

Ilikuwa kinyume cha sheria kuandaa ibada za Krismasi.

MARUFUKU HIYO HAUKUKUBALIWA KWA URAHISI.

Maandamano yalifanyika yakidai uhuru wa kunywa pombe, kuimba na kufurahia siku kuu hiyo.Ilikuwa ni baada ya Charles wa pili kuwa mfalme ndio sheria hiyo ya kupiga marufuku Krismasi ilipoondolewa.

Utamaduni wa kuandaa sherehe na kufanya shangwe ni jambo ambalo lilidharauliwa na waumini wa Puritan wa Marekani pia.

Na Marekani pia walipiga marufuku sherehe hizo wakiwa na sababu zinazofanana na za Uingereza.

Katika jimbo la Massachusetts, Marekani hawakuwa na Krismasi kati ya mwaka 1659 mpaka 1681.Hata baada ya marufuku ya sherehe za Krismasi kufutwa, waprotestanti wengi waliendelea kuamini kuwa sherehe ya Krismasi ni ya wapagani na imelaaniwa.

YESU ALIZALIWA LINI?

Bado hakujakuwa na maafikiano kuhusu ni lini hasa Yesu alizaliwa.

Wataalam wa dini wanafikiri kwamba labda ilikuwa majira ya kuchipua kwa sababu kuna taarifa za wachungaji wakiwa nyikani wakiwachunga kondoo wao.

Ingekuwepo Desemba, ambapo huwa msimu wa baridi, basi hawangekuwa malishoni, wangekuwa wametafuta hifadhi maeneo yenye joto.

Au pengine ilikuwa majira ya kupuputika kwa majani. Kuna uwezekano kwamba wachungaji walikuwa wanawaangalia kondoo wao msimu wao wa kutungishwa mimba ili kuwatenganisha kondoo jike ambao tayari walikuwa wamepandwa na kutungishwa mbegu.

BIBLIA HAIJATOA TAREHE YOYOTE.

Lakini tunafahamu kuwa kumekuwa na msimu wa matamasha na sherehe za wapagani mwishoni mwa Desemba tangu wakati wa Warumi, ambao ulikuwa utamaduni wa wapagani.

Licha hii ya ucheshi ya karne ya 19 inaonyesha Warumi walipenda sana kusherehekea

Ilikuwa ni tamasha la mavuno ambapo zawadi zilikuwa zinatolewa, nyumba zinapambwa kwa maua, chakula kilikuwa kingi cha kusaza na vinywaji vya kulewesha vilikuwepo tele.

Kwa mujibu wa mtaalam wa historia Simon Sebag Montefiore, Wakristo wa enzi hizo walilazimika kujaribu kushindana na raha na starehe ambazo ziliahidiwa na sherehe za kipagani wakati huo.

Warumi aste aste waliacha upagani na kuingia kwenye Ukristo. Lakini kubadilika huku kwa imani yao kulibadilisha kalenda ya Kikristo, kwa kipindi fulani, Warumi walisherehekea tamaduni zote mbili.

 KWANINI ILICHAGUA DESEMBA 25?

Mamia ya miaka kupita baadaya kifo cha Kristo, Desemba 25 ilichaguliwa kuwa tarehe ya kuzaliwa kwake.

Wanahistoria wengi wanaamini kwamba wakati ambao sasa Krismasi husherehekewa ulikuwa wakati wa sherehe za kipagani. Kwa mfano “Encyclopedia Britannica inasema hivi:” Ufafanuzi wa chanzo cha tarehe hii ni kwamba sikukuu ya ‘dies solis invictinati’ ( ‘Siku ya kuzaliwa kwa jua lisiloshindwa’ ) iliyosherehekewa Desemba 25, ilibadilishwa na kuwa ya Kikristo. 

Hiyo ilikuwa sikukuu maarufu ya Milki ya Roma iliyosherehekewa wakati jua lilipochomoza katika majira ya baridi kali kama ishara ya mwisho wa majira hayo na mwanzo wa majira ya kupukutika na kiangazi.”

Kitabu cha “The Encyclopedia Americana” kinasema hivi: sababu ya kutenga Desemba 25 kuwa Krismasi haijulikani lakini inaaminiwa kwamba siku hiyo ilichaguliwa ili ilingane na sherehe ya kipagani  iliyofanyika jua liliochomoza katika majira ya baridi kali, wakati mchana ulipoanza kuwa mrefu, ili kusherehekea ‘kuzaliwa tena kwa jua.’…… Satanalia ya Kiroma ( sherehe ya Saturn, mungu wa kilimo, na nguvu mpya za jua ), pia zilifanyika wakati huo.” 

Kawaida sherehe hizo zilichangamana  na matendo maovu ya kingono pia watu walisherehekea bila kujizuia  kwa kelele nyingi sana ambapo tabia hizo hizo huonekana katika sherehe nyingi za Krismasi za wakati  wa sasa.

Tukio moja muhimu ambalo Wakristo wa mwanzo walilifahamu vizuri sana, tukio hilo ni mwadhimisho au ukumbusho wa Kifo cha Yesu Kristo.

Yesu mwenyewe aliwaambia wanafunzi wake tarehe ya tukio hilo, na kuwafundisha jinsi ya kuliadhimisha. Maagizo hayo ya kipekee pamoja na tarehe ya kifo chake, yameandikwa kwenye Biblia.—Luka 22:19; 1 Wakorintho 11:25.

Namna gani wale walio na tumaini la kuishi milele katika Paradiso duniani? Wanatii amri ya Yesu kwa kuhudhuria “Mlo wa Jioni wa Bwana”,  maadhimisho hayo yanathaminiwa na Wakristo wote. Ni kipindi ambacho wote wanaweza kufikiria juu ya upendo usio na kifani wa  Mungu na Yesu Kristo.—Yohana 3:16.

Kufikia mwisho wa karne ya 4, matambiko na sherehe za kipagani za Kikristo zilifanyika kwa pamoja kwa kipindi cha siku 14 mwezi Desemba. Lakini hilo halikufanyika bila mfarakano.

Krismasi kote duniani huwa msimu wa sherehe, kula vinono, mapambo, kuvalia mavazi mapya na ya kupendeza, kujumuika na marafiki, kuwatembeleza marafiki, kuwajulia hali wazazi, kwenda likizoni, kufurahia kwa pombe na vileo na kadhalika.