RUSHWA ni adui wa haki na maendeleo na usemi huo hubainika pale ambapo haki inaponunuliwa kwa gharama yoyote.

Rushwa ni jambo linalowafanya wanyonge kukosa haki yao na hivyo kuwapa nafasi walionacho kuinunua haki ya mtu.

Ni ukweli usiopingika kuwa tatizo la rushwa limeshamiri karibu maeneo yote ya upatikanaji haki hasa kwa baadhi ya taasisi za umma au kwa baadhi ya watumishi wa umma.

Kwa mfano unapokwenda baadhi ya hospitali, polisi, mahakamani na sehemu zozote ambazo zimekuwa na usumbufu wa kuipata haki kwa njia ya urahisi ni lazima utoe chochote kitu ili kufanyiwa kazi zako kwa haraka ama kwa ufanisi mkubwa.

Mara kadhaa tumekuwa tukishuhudia watu wakikosa haki zao kwa dakika za mwisho na pia tunaona watu wakipata haki kwa njia zisizokuwa za halali kutokana na kutoa rushwa.

Pamoja na taasisi nyingi kuhusishwa na rushwa, lakini jeshi la polisi limekuwa likisemwa vibaya juu ya madai ya kupokea rushwa kwa baadhi ya askari wake na ndio maana hata makamanda wamekuwa wakikemea jambo hili hivi karibuni.

Askari wanaohusishwa zaidi na rushwa ni wale wa usalama barabarani, jambo ambalo linalipaka matope jeshi hilo.

Tumekuwa tukiona kupitia kwenye mitandao ya kijamii baadhi ya askari wakidai na kupokea rushwa kwenye matukio mbalimbali yaliyofanyika hapa Tanzania.

Tufahamu kuwa jeshi la polisi ni kimbilio la watu wengi kwa ajili ya kutafuta haki, hivyo rushwa inapotawala katika eneo hilo wananchi wakimbilie wapi?

Tunasema hivyo kwa sababu mara kadhaa tumeona kuwa askari polisi wamekuwa wakifanya masuluhisho kwa makosa mbalimbali kwa mfano kesi za udhalilishaji wa kijinsia, madereva wa vyombo vya moto kama magari na vespa na kulazimika kulipwa fedha na wakati mwengine hazifiki hata sehemu husika kama ilivyo baadhi ya mifano tulioiyona kwenye mitandao ya kijamii.

Mbali na kutozwa faini zilizo kisheria, lakini tunaliomba jeshi la polisi hasa kitengo cha usalama barabarani kuweka mfumo wa kutoa risiti pale ambapo mtu atapatikana na kosa la papo kwa papo na sio kulipana kichochoroni kwani ni wazi kuwa fedha hizo hazitafika popote na kutengeneza mazingira ya rushwa.

Hivi sasa jeshi la polisi Tanzania bara, lina utaratibu mzuri ambapo dereva au abiria anaepatikana na kosa barabarani hutozwa faini ya papo kwa papo inayoambatana na risiti.

Tunaupongeza utaratibu huu kwa kuwa jeshi la polisi mara nyingi limekuwa likinyooshewa vidole kwa tuhuma za rushwa, hivyo hali hii itapunguza rushwa.

Kila mmoja wetu anaweza kuepuka rushwa kama msemo usemao usipokee rushwa wala usitoe rushwa.