NA KHADIJA KHAMIS, MAELEZO

MWENYEKITI wa Muungano wa Maradhi yasioambukiza Zanzibar Dr. Said Gharib Bilali, amesema watu wanaoishi na maradhi yasiyoambukizwa ni rahisi kupata maambukizi ya ugonjwa mwengine kutokana na kinga yao kuwa dhaifu.

Alisema kutokana na udhaifu huo ni rahisi kupata maambukizi ya maradhi ya mripuko, jambo ambalo ni vyema kulijuwa na kulichukulia tahadhari.

Hayo aliyasema wakati alipofungua Mkutano wa siku moja uliohusisha wadau kutoka vitengo mbali mbali huko katika Ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe Mjini Unguja.

“Kuna uhusiano mkubwa kati ya maradhi yasiyoambukiza na maradhi ya mripuko yakiwemo maradhi ya homa kali ya mapafu hivyo iko haja ya jamii kujikinga .”alisema Dr. Said.

Aidha alifahamisha kuwa maradhi yasiyoambukiza huathiri kwa muda mrefu bila ya mtu kujijuwa hivyo aliitaka jamii kujichunguza Afya zao.

Nae Meneja wa Maradhi yasioambukiza kutoka Wizara ya Afya,  Omar Abdalla Ali, amesema maradhi hayo yamekuwa na kiwango kikubwa ambacho kinaiathiri zaidi jamii kutokana na mlo usio sahihi, kutofanya mazowezi, uvutaji wa Tumbaku pamoja na  Pombe.

Alisema maradhi hayo huiathiri jamii, hatua kwa hatua bila ya kujua hali ambayo inashindikana kudhibitiwa na tiba za maradhi hayo zina gharama kubwa.

Aidha alifahamisha kuwa maradhi ya kiharusi hutokana na athari ya maradhi ya kisukari na presha ambayo husababishwa na vichocheo vya mfumo wa mabadiliko ya maisha .

Pia alifahamisha kuwa kuna baadhi ya watu hupata maradhi hayo kutokana na urithi wa wazazi wao, jambo ambalo haliwezi kuzuilika na huengezeka na vichocheo vyengine.