NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Jang’ombe boy’s imewatambia watani wake wa jadi Taifa Jang’ombe kwa kuwafunga mabao 2-0, katika mchezo wa ligi daraja la kwanza Kanda ya Unguja uliochezwa jana uwanja wa Amaan.

Mchezo huo ambao ni wa tatu kwa kila timu ulikuwa na ushindani wa hali ya juu na kuhudhuriwa na umati wa mashabiki ambao walionekana kuvutiwa nao.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilikuwa ikishambuliana kwa zamu na kudiriki kwenda kwa mapumziko kwa Jang’ombe boy’s kuongoza bao 1-0.

Kipindi cha pili kilianza na timu hizo kuendelea kushambuliana ambapo Taifa licha ya kujenga mashambulizi hayo lakini walijikuta  wakishindwa kusawazisha mabao hayo.

Boys ambao mechi iliyopita walitoka sare ya kufungana bao 1-1 na New King walionekana kucheza kwa ari ili kuweza kuondoka na ushindi huo.

Mabao hayo ya boys ambayo yalipeleka sherehe katika mtaa wa Jang’ombe yalifungwa na Khatib Ameir dakika ya 11 na Shaaban Hassan dakika ya 51.

Mbali na mchezo huo pia katika uwanja wa Mao Zedong nako kulikuwa na mchezo kati ya Ngome na Idumu ambao ulimalizika kwa Ngome kushinda mabao 2-0.

Aidha katika uwanja wa Jambiani Dulla Boy’s alikuwa uso kuwa uso na New King ambao ulimalizika kwa timu ya New King kufungwa mabao 5-2.

Ligi hiyo itaendelea tena Disemba 31 mwaka huu kwa kuchezwa mechi tatu, ambapo katika uwanja wa Mao Zedong Uhamiaji itacheza na Mwembemakumbi City, wakati Kilimani City na Gulioni FC watacheza uwanja wa Amaan na katika uwanja wa Mchangani FC itaikaribisha Mchangani United.