NAIROBI, KENYA

KIKOSI maalumu cha Jeshi la ulinzi la Kenya (KDF) kimeshambulia maficho ya kundi la kigaidi la al-Shabaab katika Msitu wa Boni kaunti ya Lamu, pwani ya Kenya na kuangamiza wanachama kadhaa wa genge hilo.

Picha ya video za opereseheni hiyo zilisambaa katika mitandao ya kijamii.

Haijabainika ni magaidi wangapi wa al-Shabaab waliuawa katika shambulio hilo lakini duru za habari zinasema kwa pamoja wanachama wanne wa genge hilo waliangamizwa.

Wanajeshi hao wa KDF walifanikiwa kunasa silaha zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao, yakiwemo maguruneti, risasi, radio za mawasiliano na kanda za video.

Inaarifiwa kuwa, genge hilo la kigaidi lilikuwa linakula njama za kutekeleza wimbi la mashambulizi katika pwani ya Kenya katika kipindi hiki cha shamrashamra za sherehe za kufunga mwaka 2020 Miladia.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya kundi hilo la kigaidi kukiri kuwa ndilo lililomteka nyara na kumuua kwa kumkata kichwa Naibu Chifu mmoja wa kaunti ya Wajir, huko kaskazini mashariki mwa Kenya.

Magaidi hao wa al-Shabaab walimteka nyara ofisa huyo wa Serikali baada ya kushambulia kituo cha polisi katika kaunti hiyo, ambapo mbali na kuwahutubia kwa lazima wakaazi wa kijiji hicho, waliiba chakula cha msaada cha wakaazi wa eneo hilo.