NA MWAJUMA JUMA

TIMU za soka za JKU na Chuoni juzi ziliona mwezi baada kutoka na ushindi katika michezo yao ya ligi kuu ya Zanzibar iliyochezwa kwenye viwanja viwili tofauti.

Timu hizo ambazo zote ni ushindi wao wa kwanza kufatia ushindi huo JKU atakuwa nafasi ya tisa akiwa na pointi tano wakati Chuoni ikipanda hadi nafasi ya 11 kutoka mkiani akiwa na pointi nne katika msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na KMKM wenye pointi 12.

Chuoni ilijipatia ushindi wa mabao 3 – 2 dhidi ya timu ya Polisi katika mchezo wake uliochezwa uwanja wa Amaan wakati JKU ilishinda mabao 2 – 0 dhidi ya Mlandege.

Chuoni katika mchezo wake huo mabao yake yalifungwa na wachezaji wake Ali Khamis katika dakika ya 11, Mustafa Zakaria dakika ya 36 na Mundhir Abdallah dakika ya 50.

Kwa upande wa timu ya Polisi ambao wapo nafasi ya 10 wakiwa na pointi nne mabao yake hayo ya kufutia machozi yaliwekwa kimiyani na wafungaji wake Suleiman Ali Nuhu dakika ya 30 na Ali Khatib dakika ya 57.

Nao maafande wa timu ya JKU mabao yake hayo ya ushindi yalifungwa na wachezaji wake Shehu Magaji dakika ya 88 na Mustafa Hamad dakika ya 89.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Disemba 23 mwaka huu, ambapo jumla ya michezo mitatu itachezwa katika viwanja vitatu viliopo visiwani Zanzibar.

Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo katika uwanja wa Amaan Kipanga itacheza na KVZ, wakati Mao Zedong, Black Sailor itacheza na Zimamoto na Hard Rock na Polisi watacheza Gombani Pemba.