DODOMA

RAIS John Magufuli, amewataka watanzania kuendelea kumuomba Mungu alilinde taifa dhidi ya janga la corona katika kipindi hiki ambacho mataifa mengine yanaendelea kuathiriwa na ugonjwa huo.

Pia amewataka viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kukubali kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa huo badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee.

Rais Magufuli alitoa wito huo aliposhiriki misa takatifu ya krismasi katika kanisa katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata mjini Dodoma iliyoongozwa na Padre Paul Mapalala.

Alisema, “Upendo na miujiza ya Mungu kwa Tanzania inajidhihirisha katika kipindi hiki ambapo dunia inapita katika wakati mgumu wa janga la ugonjwa wa corona (Covid-19) ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, lakini Tanzania imeepushwa na janga hilo na maisha ya Watanzania yanaendelea kama kawaida.

Tuendeleea kumshukuru Mungu na kumuomba azidi kutuepusha na tuwaombee wananchi wa mataifa mengine waepushwe na ugonjwa huu ambao umeshaghalimu maisha ya wengi,”.

Kauli hiyo ya Rais Magufuli imekuja kipindi ambacho katika mataifa mengi ya Ulaya watu wameshindwa kuhudhuria ibada ya krismasi kutokana na hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo unaoendelea kusambaa katika mataifa hayo.

Maadhimisho ya krismasi mwaka huu yametandwa na janga la virusi vya corona linalozidi kuangamiza maisha ya watu ambapo kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis alitoa tamko la kuwataka waumini wa kanisa hilo kufuata maagizo yote ya mamlaka za kidunia juu ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Hali inaonekana kuwa tete zaidi nchini Uingereza ambako kuna taarifa za mlipuko wa kirusi kipya cha corona hali iliyosababisha shughuli nyingi zinazohusisha mikusanyiko kusitishwa kutokana na kasi yake ya kusambaa.

Kirusi hicho kipya cha corona kimetajwa kuingia pia nchini Ujerumani na taratibu kinasambaa katika mataifa mengine ya Ulaya.