CALIFORNIA,Marekani
JUMBA kubwa la kifahari la Neverland alilokuwa akiishi Mfalme wa Pop Michael Jackson huko Los Olivos, California limeuzwa kwa bilionea Ron Burkle ambaye ni rafiki wa zamani wa Michael Jackson kwa dola milioni 22 (sawa na bilioni 51 za Kitanzania), ambayo ni robo ya thamani kwani kwa mara ya kwanza lilinadiwa kwa dola milioni 100 mwaka 2015.
Michael Jackson alilinunua jumba hilo mwaka 1987 kwa dola milioni 19 na kulifanya kuwa nyumbani kwake wakati wa umaarufu wake na alibadilisha jumba hilo na kuwa eneo la burudani, akijenga eneo la kufuga wanyama mbali, ukumbi wa chini ya ardhi na maeneo ya kuchezea watoto na familia zao
Jumba hilo lililonunuliwa na Ron Burkle limejengwa katika shamba la ekari 2700 na tayari limebadilishwa jina na kuitwa Sycamore Valley Ranch. Jumba hilo limefanyiwa ukarabati mkubwa tangu kufariki kwa Michael Jackson Mwezi June 2009.