NA MWAJUMA JUMA

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan’ King’, ametangaza majina ya wajumbe wanane wa kamati ya uhamasishaji ya michuano ya kombe la mapinduzi yanayotarajiwa kuanza kati ya Janauri mosi au 3, mwakani.

Majina ya wajumbe wa kamati hiyo aliyatangaza jana huko Ofisini kwake iliyopo Migombani Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kamati hiyo itakayojumuisha wajumbe kutoka Zanzibar na Tanzania bara itaongozwa na mwenyekiti Taufiq Salim Turkey na wajumbe wake ni Hassan Mussa Ibrahim, Aalum Issa Ameir, Mwanahawa Rajab Iddi, Khamis Mwinjuma (Mwana FA), Jerry Muro, Salama Jabir na Ali Saleh .

Akitangaza majina hayo kwa niaba ya waziri wa wizara hiyo alisema lengo la kamati hiyo ni kunogesha na kuwahamasisha wananchi kupitia wasanii wa sanaa za asili, maigizo na kizazi kipya kujitokeza kwa wingi kushuhudia michuano hiyo kwa ajili ya kuyaenzi mapinduzi.

Alisema kamati hiyo itakuwa na majukumu ya kuratibu na kusimamia wasanii pamoja na upatikanaji wa fedha kutoka kwa wadau wa michezo, wafadhili na taasisi binafsi kwa ajili ya uendeshaji wa burudani kutoka kwa wasanii hao.

King alitumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi , wapenda soka kuuunga mkono michuano hiyo kwa kwenda kwa wingi viwanjani .

Alifahamisha kuwa katika michuano ya mwakani hamasa za wasanii mbali mbali zitatumbuiza uwanjani kabla ya mechi , wakati wa mapumziko na baada ya mechi.

Timu tisa za Zanzibar na Tanzania bara tayari zimethibitsha kushiriki michuano hiyo kuwania taji la mapinduzi ambapo kwa sasa linashikiliwa na timu ya Mtibwa Sugar ya Turiani mjini Morogoro.

Timu hizo ni Malindi, Mlandege, Chipukizi, Jamhuri, Simba, Yanga, Azam, Namungo na mabingwa watetezi timu ya Mtibwa Suger.