NA MADINA ISSA

JESHI la polisi kitengo cha dawati la jinsia na watoto, kimejumuika na wazee wa nyumba za wazee Welezo na Sebleni katika hafla ya chakula cha mchana kwa lengo la kuwaweka pamoja.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyoambatana na zoezi la usafi wa mazingira, Kamishna wa ushirikishwaji jamii wa polisi Tanzania, Dk. Mussa Ali Mussa, alisema hatua hiyo inakusudia kuondoa dhana iliyojengeka katika jamii juu ya kuwaogopa askari wa jeshi hilo ambao wapo kwa ajili ya kutunza usalama wao.

Alisema wananchi wakiwemo wazee ndio hazina ya taifa, hivyo ni vyema kuchanganyika nao ili kuwapa matumaini na kuwathamini hasa ikizingatiwa walikuwa na mchango mkubwa katika kujenga nchi yao.

“Wazee wetu ndio rasilimali yetu hivyo hatuna budi kukaa nao pamoja kwa shida na raha,” alisema.

Mkuu wa dawati la jinsia Tanzania, Marry Nzuki, alisema, wanashirikiana na wananchi katika kufichua vitendo vya udhalilishaji baada ya kutambua kazi zinazofanywa na dawati hilo.

Alisema mikusanyiko hiyo inakusudia kutangaza kazi zinazofanywa na dawati hilo ili kuhakikisha wananchi wanalitumia kuwasilisha changamoto zao.

Mkuu wa nyumba ya kutunza wazee Sebleni, Khamis Ali Haji, alipongeza hatua ya jeshi la polisi kuwafikia katika makaazi yao  na kuziomba taasisi nyengine kuiga mfano huo.

Kwa upande wao, wazee hao walisema kuwa wamefarajika na kwamba wanajisikia kama ni sehemu ya jamii pale wanapotembelewa.