JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni moja ya taifa lenye eneo kubwa la ardhi, lakini pia limejaaliwa kuwa na maliasili nyingi zenye mahitaji makubwa sehemu mbalimbali ulimwenguni.

Kwa mabahati mbaya mali asili zote zikiwemo zile nadra kupatikana maeneo mengine duniani zinaopatikana nchini DRC, kwa miaka yote hiyo haijalinufaisha taifa hilo na wananchi wake.

Kutokana na hali hiyo, nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limekuwa kuwa miongoni mwa mataifa masikini pamoja na wingi mkubwa wa rasilimali ilizojaaliwa kuwa nazo.

Kwa kiswahili cha kawaida, DRC ni kama nchi ambayo unaweza kuiita shamba la bibi kwani inasemekana baadhi ya nchi zinaingia nchini humo na kupora mali asili muhimu.

Taarifa zinaeleza kuwa migogoro na machafuko makubwa yanayotokea nchini humo chanzo chake kikubwa kinatokana na rasilimali ilizobarikiwa nchi.

Ripoti iliyotolea hivi karibuni na Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa baadhi ya nchi jirani zinajipenyeza nchini humo na kupora rasilimali za aina mbalimbali.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN), wameeleza kuwa kuna usafirishaji wa dhahabu ya DRC kwa njia za magendo kupitia mashariki ya nchi hiyo na kuelekea nchi jirani za eneo hilo la maziwa makuu.

Katika ripoti hiyo, mji wa Kampala uliopo nchini Uganda unatajwa kama kituo kikuu cha biashara ya dhahabu inayosafirishwa kimagendo inayoporwa kutoka nchini Congo.

Ripoti hiyo imeibaini kwamba uchimbaji wa madini ya dhahabu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo unaendelea kwa aina fulani kutoripotiwa inavyostahili, huku tani kadhaa za madini hayo ya tunu zikisafirishwa kwa magendo nje ya taifa hilo kwenye masoko ya dunia kupitia nchi jirani za taifa hilo kwa upande wa mashariki.

Nchi jirani na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zilizoko kwenye eneo la mpaka wake wa mashariki kwa kipindi kirefu zinatumiwa kama chochoro ya kusafirisha madini ya dhahabu ya mabilioni ya dola yaliyochimbwa kwa njia zisizo za kisasa na wale wanaoitwa wachimba migodi wadogo. 

Kutokana na kuwepo ugumu wa kufuatilia biashara ya madini hayo ya thamani,  kumechochea vita vya kikanda, ufadhili wa makundi ya wapiganaji na kusababisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya wafanyabiashara wanaojihusisha katika harakati za kufanikisha biashara ya usafirishaji madini hayo ya Congo.

Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo limebaini kwenye ripoti yao ya mwaka kwamba katika mikoa ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri imeripotiwa kwamba kiwango rasmi cha madini hayo kilichochimbwa na wachimbaji wadogo kilikuwa ni zaidi ya kilo 60 katika mwaka 2019 ingawa kiwango jumla cha dhahabu iliyosafirishwa ni zaidi ya kilo 73.

Ripiti ya wataalamu hao iliongeza kwa kueleza kuwa inakaridia kwamba kiasi tani 1.1 ya dhababu ilisafirishwa kwa njia ya magendo kutoka mkoani Ituri katika mwaka 2019 pekee.

Kiwango hicho cha dhahabu kingeiwezesha serikali kujipatia zaidi ya dola milioni 1.8 kupitia ushuru endapo ingesafirishwa kwa njia halali. Kwenye mikoa yote inayochimbwa dhahabu nchini humo inatajwa kwamba hasara iliyoshuhudiwa huenda ni kubwa zaidi.

Wachimbaji wadogo nchini Congo wanachimba tani 15 hadi 22 za madini hayo kila mwaka kwa mujibu wa makadirio ya taasisi ya kijerumani ya masuala ya uchimbaji unaohusu ardhi na mali asili.

Hata hivyo waziri anayehusika na madini nchini Congo, Willy Kitobo Samsoni, alipoulizwa na shirika la habari la reuters kuhusu ripoti hiyo iliyotolewa, alisema hawezi kutoa jibu mara moja kuhusu kiwango cha madini kinachosafirishwa kwa njia za magendo kutoka mashariki mwa nchi hiyo.

Watalaamu wa Umoja wa Mataifa pia wamebaini kwamba Uganda na nchi nyingine jirani zinasafirisha kiwango kikubwa cha dhahabu kuliko kile kinachochimbwa na nchi hizo hali inayoashiria kwamba huenda zinahusika kwenye dhahabu inayosafirishwa kimagendo kutoka Congo.

Zaidi ya asilimia 95 ya dhahabu iliyosafirishwa mwaka 2019 kutoka Uganda ambayo ni kiasi zaidi ya tani 25 haikuwa dhahabu asili ya Uganda, kundi hilo la wataalamu limekadiria hayo kwa kuzingatia uzalishaji wa nchi hiyo wa mwaka 2018 na takwimu za usafirishaji madini hayo ya mwaka 2019.

Takwimu za benki kuu ya Uganda ya mwezi Machi mwaka 2020 zilionesha kwamba kiwango cha dhahabu iliyosafirishwa kutoka Uganda iliongezeka zaidi ya mara mbili katika mwaka 2019 ikilinganishwa na miaka iliyopita. Waziri wa nishati wa Uganda naye hakujibu ombi la kumtaka atoe tamko kuhusu ripoti hii.

Lakini wasafirishaji magendo waliwaambia wataalamu kwamba Kampala ndio kituo kikuu cha biashara ya dhahabu kutoka mkoani Ituri. Dhahabu iliyosafirishwa kutoka Kivu Kusini ilipelekwa Burundi, Rwanda, Umoja wa Falme za kiarabu na Tanzania kwa mujibu wa ripoti hiyo.