KWA wakati huu wananchi wa Uganda wamekuwa kwenye kampeni ngumu za kisiasa zitakazohitimika kupatikana kwa rais mpya kwenye uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Januari 14 mwakani.

Ugumu wa kampeni unatokana na janga la maradhi ya corona, ambapo kumewekwa sheria kali za mikusanyiko ya wafuasi wa vyama vya siasa, ambapo mwanasiasa haruhusiwi kukutana na kundi la watu kunadi sera zake wasiozidi 200.

Kampeni za kisiasa kwenye uchaguzi utakaofanyika mapema mwakani hazina tofauti sana na zile zinazofanyika kwenye chaguzi zilizopita kwani kumeshuhudiwa matumizi makubwa ya kutumia nguvu kupita kiasi kunakofanya na vikosi vya usalama.

Aidha kwenye kampeni zinazoendelea matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa vikosi vya usalama yamesababisha watu kadhaa kufariki wengi wao wakielezwa kuwa ni wafusi wa upinzani.

Katika tukio la karibuni kabisa lililoripotiwa ni kufariki katika mazingira ya kutatanisha kwa mmoja wa walinzi wa mgombea wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine.

Ripoti za vyombo vya habari nchini Uganda zinaeleza kuwa mlinzi huyo aliyetambulika kwa jina la Francis Kalibala, aligongwa na gari la jeshi la Uganda (UPDF) wakati msafara wa Bobi Wine ulipokuwa njiani ukirudi Kampala kutoka mji wa Masaka kwenye kampeni.

Kupitia mitandao ya kijamii Bobi Wine alisema anasikitika kutangaza kifo cha mmoja wa walinzi wake Francis Kalibala aliyegongwa na gari la jeshi namba H4DF 2382 ambalo liliziba njia karibu na Busega kuuzuia msafara wake.

Lakini msemaji wa jeshi la Uganda, Brig. Flavia Byekwaso alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba Francis alianguka kutoka kwa gari lililokuwa linaendeshwa kwa mwendo wa kasi.

“Francis hakugongwa na gari la jeshi la UPDF. Alianguka kutoka kwa gari namba UBF 850Z”, alisema Byekwaso katika ujumbe wa twitter.

Kabla ya tukio hilo la kuuawa kwa mlinzi wa mgombea huyo wa urais, waandishi kadhaa wa habari waliokuwa wakiripoti taarifa za mgombea huyo wa upinzani walishambuliwa na polisi na kujeruhiwa vibaya.

Waandishi hao walikuwa wanafuatilia tukio ambalo polisi walimzuia Bobi Wine kufanya kampeni na kuzua makabiliano kati ya polisi na wafuasi wa Bobi wine katika mji wa Masakaa.

Miongoni mwa waandishi walioonja joto ya jiwe kwenye sakata hilo ni mpiga picha wa televisheni ya Bobi Wine ya Ghetto TV, Ashraf Kasirye, mwandishi wa shirika la habari la Nation Media Group – NTV Ali Mivule.

“Gesi ya kutoa machozi ilitumika kutawanya wafuasi wa Bobi Wine na kwa bahati mbaya waandishi wa habari walijeruhiwa,” alisema msemaji wa polisi Fred Enanga.

Tume ya uchaguzi imepiga marufuku kampeni katika wilaya na miji kadhaa ikisema kwamba wilaya hizo zina idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona na huenda kampeni zinazoendelea zinaweza kuongeza kasi ya maambikizi.

Wilaya zilizopigwa marufuku kfanyika kwa kampeni za kisiasa ni pamoja na  Mbarara, Kabarole, Luweero, Kasese, Masaka, Wakiso, Jinja, Kalungu, Kazo, Kampala na Tororo.

Wanasiasa wa upinzani hata hivyo wamesema hatua hiyo ni ya kisiasa kwa sababu sehemu ambapo kampeni zimepigwa marufuku ni ngome za kisiasa hasa za mgombea wa upinzani anayemnyima usingizi Yoweri Museveni, Bobi Wine.

Yoweri Museveni anagombea urais kwa muhula wa sita, tayari amemaliza kufanya kampeni katika baadhi ya sehemu hizo zilizozuiliwa kufanyika kampeni kwa wakati huu na ndizo ambazo zimesalia kwa Bobi Wine.

Tume ya uchaguzi hata hivyo, imesema kwamba rais Museveni anaweza kuendelea kuzindua miradi ya serikali katika sehemu ambazo kampeni zimepigwa marufuku.

“Hatua ya tume ya uchaguzi imeniathiri sana. Wilaya ya Wakiso ina wapiga kura milioni 1.5 Kampala ina wapiga kura milioni moja, Jinja na Masaka zina maelfu ya wapiga kura. Najiuliza, ni wapi nitatoa kura iwapo sitafanya kampeni?” alisema Generali Henry Tukukunde, mgombea wa urais.

Wagombea wa viti mbalimbali wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kufanya kampeni. Idadi ya wapiga kura katika wilaya ambapo tume ya uchaguzi imepiga marufuku kampeni ya moja kwa moja.

Katika kuthibitisha matumizi ya nguvu ya vikosi vua usalama nchini humo, mgombea wa urais kupitia chama cha Forum for democratic change FDC Patrick Amuriat, amenyunyuziwa pilipili machoni na kukimbizwa hospitali.

Mgombea huyo alikuwa kwenye msafara na kuzuiliwa na polisi alipokuwa safarini kwenda katika mkutano wa kampeni wilayani Tororo, ambapo alifungua dirisha la gari yake kuzungumza na polisi, ndipo ofisa wa polisi alipochukua fursa hiyo kumnyunyuzia pilipili machoni.

Wakati huo huo, mtoto wa rais Yoweri Museveni aliyewahi kuwa mshauri wake na hivi karibuni kumteua kuongoza kikosi cha ulinzi wa rais, Muhoozi Kainerugaba, amesema kuwa wakoloni wanaounga mkono upinzani watashindwa.

Luteni jenerali Muhoozi aliwaonya wale aliwataja kama wakoloni wanaounga mkono upinzani nchini Uganda na kusema kuwa watashindwa vibaya sana katika uchaguzi mkuu wa Januari 14.

Muhoozi amelazimika kutoa ujumbe huo kufuatia wakili wa Bobi Wine, Robert Amsterdam kuomba jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kuwaajibisha maofisa wa vyombo vya usalama wanaotumia mkono wa chuma dhidi ya viongozi na wafusi wa upinzani nchini Uganda.

Muhoozi alimalizia ujumbe kwa kutumia maneno ya kwanza ya wimbo wa taifa wa Afrika Kusini “Nkosi Sikelei iAfrica” maana yake, “Mungu ibariki Afrika!”. Na kueleza kuwa waafrika watashinda wale wote ambao kila mara wanataka kuwatawala.”

Maofisa wa ngazi ya juu katika serikali ya Uganda wamemshambulia mkuu wa shirika la kufuatilia haki za kibinadamu -Human Rights Watch, Ken Roth wakimshutumu kwa kuingilia katika siasa za nchi hiyo.

Miongoni mwa maofisa waliomshambulia Roth ni balozi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa Adonia Ayebare, baada ya kukosoa hatua ya tume ya uchaguzi kupiga marufuku kampeni za moja kwa moja katika wilaya kadhaa ambazo wachambuzi wa siasa Uganda wanasema Bobi Wine ana umaarufu mkubwa.

“Tafadhali achana kabisa na siasa za Uganda pamoja na mikakati yetu ya kupambana na virusi vya Corona. Hatuna haja na ukosoaji wako,” ameandika Balozi Ayebaye akiongeza kwamba Ken Roth ameshindwa kabisa kutekeleza kazi yake katika shirika la kufuatilia haki za kibinadamu – Human Rights Watch na kuangusha shirika hilo kwa jumla.

“Shirika la HRW limekuwa kundi la wanaharakati wa kisiasa kwa lengo la kuvuruga siasa za Afrika,” ameongezea kuandika balozi Ayebare.

Mashambulizi hayo ya twitter dhidi ya Ken Roth pia yamemhusisha msimamizi wa habari wa Rais Yoweri Museveni Don Wanyama, aliyeandika “swala la ni nani maarufu wapi, litaamuliwa na wapiga kura wa Uganda Januari 14 na wala sio mawakala wa ukoloni wanakaa katika nchi za magahribi. Heshimu uhuru wetu”.

Waandishi wa habari nchini Uganda wamesusia kikao na maofisa wa ngazi ya juu wa usalama wakilalamikia ukandamizaji wa polisi na wanajeshi dhidi yao na wamelalamika kwamba maofisa wa polisi wanawalenga wakiwa kazini, hasa wale wanaoandika habari za siasa.

Wandishi walitaka msemaji wa jeshi Brig Flavia Byekwaso kuwaomba msahama kabla ya kuwahutubia kuhusu maandalizi ya kusherehekea siku ya wanajeshi Uganda maarufu Tarehe sita.

Byekwaso hata hivyo amekatakaa kuomba msamaha na hivyo kupelekea waandishi kuondoka katika kikao hicho. Maofisa wengine wa usalama akiwemo Maj Gen. Henry Matsiko nao wamekataa kuomba msamaha.

“Hatutaandika habari kuhusu maofisa wa usalama hadi mtakapotuheshimu na kuheshimu kazi yetu.” Mmoja wa waandishi wa habari alisema.