NAIROBI, KENYA

SEKTA ya utalii nchini Kenya imefurahia idadi kubwa ya watalii wa ndani ambao walitembelea maeneo tofauti yenye vivutio na kuleta matumaini ya kufufuka kwa sekta hiyo ambayo iliathiriwa pakubwa na janga la Corona.

Mbali na eneo la Pwani ambalo limekuwa likitembelewa sana kutokana na mandhari nzuri ya kuvutia watalii wengi kutoka ndani ya nchi walionekana wakivutiwa na maeneo mbali mbali nchini Kenya.

Hiyo ilipelekea hoteli nyingi kufurika wageni huku bei ikiwa ni ya chini.

Wamiliki wa mahoteli walisema tegemeo lao kubwa ni watalii wa ndani ya nchi, hii ni baada ya watalii wa kigeni kususia kuzuru Kenya kwa kuhofia kuambukizwa virusi vya corona.

Walisema walitembelea hoteli ya Kisiwa cha Rusinga katika eneo la Kisumu ambapo idadi ya watalii wa ndani walionekana kuwa wengi zaidi kuliko hapo awali.

Hivi sasa hoteli hiyo inalenga kufungua tovuti ya kujiuza inayowalenga watalii wa ndani.

“Kitu ambacho tunataka kulenga zaidi ni kuwa utalii wa ndani ni mzuri zaidi. Kulingana na vivutio vingi vya utalii tulivyonavyo hapa tunataka kujenga tovuti kwa ajili ya watalii wa ndani itakayowaonyesha baadhi ya huduma tunazotoa kwenye hoteli yetu”. Mmiliki wa Hoteli.

Walisema sekta ya utalii ndio inayodaiwa kuathirika vibaya kufuatia kuibuka kwa janga la corona,baada ya safari nyingi za kimataifa kukatizwa na nchi mbali mbali ikiwemo Kenya.

Hata hivyo baadhi ya wadau wanaona kuna matumaini baada ya idadi kubwa ya watalii wa ndani kutembelea maeneo tofauti.

Baadhi yao wanaona mambo huenda yakawa mazuri zaidi ya ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

”Sekta hii ya utalii bado haijafufuka lakini katika siku zijazo kama miezi miwili mitatu hivi mambo huenda yakawa mazuri zaidi.Tatizo ambalo limekuwa kikwazo kwa kufufuka kwa sekta hii ni lile la virusi vya corona,kwani Corona bado iko na sisi”, mdau wa utalii alisema.

Katika eneo la Pwani idadi ya watalii pia ilionekana kuongezeka. Watalii wengi walitembelea fukwe za bahari kujionea mandhari nzuri ya mji huo.

Antony Mwasinje Mwalekwa ni mwenyeki wa bahari ya Jomo kenyatta mjini Mombasa alisema ni furaha kubwa kwa wapwani kuona watalii wengi wa ndani ya nchi wakitalii mji huo wa kipekee.

Alisema hiyo ni ishara ya kufufuka kwa biashara iliyokuwa inadidimia.

Wamiliki wengi wa mahoteli ya kitalii walikiri kupata hasara kubwa kutokana na janga la corona na kusababisha watu wengi kufutwa kazi.

Hata hivyo walianza kuwarejesha kazini baadhi ya wafanya kazi baada ya kuona hali inaanza kurudi vizuri kutokana na watalii wa ndani.