NA HUSNA SHEHA

KIJANA wa miaka 28 aliyedaiwa kupatikana na dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 1.2968 anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani Disemba 22 mwaka huu, kwa kuanza kusikilizwa mashahidi.

Kijana huyo ambae ametakiwa kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 400,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili watakaomdhamini kwa kina hicho hicho cha fedha za maandishi, pamoja na barua ya sheha na kitambulisho cha Mzanzibari kwa uthibitisho.

Hakimu Makame Khamis, alimpa dhamana hiyo mshitakiwa Khamis Hamad Yahya, mkaazi wa Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja, baada ya kuiomba mahakama kumpatia dhamana.

Mshitakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana na kutakiwa kufika tena mahakamani hapo Disemba 22 mwaka huu kwa kuendelea na kesi yake.

Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Khamis Othman, alidai kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na dawa za kulevya kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) cha sheria namba 9 ya mwaka 2009, kama kilivyorekebishwa na kifungu cha 11 (a) cha sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa kuwa Novemba 17 mwaka huu majira ya saa 8:00 mchana huko Kinyasini Sokoni Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini Unguja, mshitakiwa huyo alipatikana na kete 52 aina ya heroini zenye uzito wa 1.2968 gramu, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Awali mshitakiwa huyo aliposomewa kosa lake alikataa, nao upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo tayari umekamilika, na kuiomba mahakama kumpangia tarehe nyengine kwa ajili ya kusikiliza mashahidi.