NA MARYAM HASSAN

LEO kijana aliyedaiwa kuvunja nyumba anayoishi Amour Salim Mohammed anatarajiwa kupanda katika mahakama ya mkoa Mwera, kuanza kusikilizwa ushahidi.

Mshitakiwa huyo ni Shaaban Abas Rajabu (27) mkaazi wa Mboriborini, ambae alifikishwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Khamis Ali Simai.

Mshitakiwa huyo alipelekwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana aliyopewa na mahakama ya mkoa Mwera, aliyotakiwa kusaini bondi ya shilingi 2,000,000 pamoja na wadhamini wawili waliotakiwa kusaini kima hicho hicho cha fedha.

Aidha wadhamini ambao watamdhamini Shaaban, wametakiwa kuwasilisha kopi ya kitambulisho cha Mzanzibar Mkaazi na barua ya Sheha wa Shehiya anayoishi, lakini mshitakiwa huyo alishindwa kutekeleza masharti hayo na badala yake kupelekwa rumande.

Kwa mujibu wa maelezo ya wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Ayoub Nassor, alisema ifikapo Disemba 30 watawasilisha mashahidi katika kesi kesi hiyo.

Kijana huyo anadaiwa kutenda kosa la kuvunja nyumba ya kuishi kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo, kinyume na kifungu cha 292 (1) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Kosa hilo anadaiwa kutenda Novemba 13 mwaka huu majira ya saa 5:43 za mchana, huko Jumbi wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Mshitakiwa huyo anadaiwa kuingia ndani ya nyumba ya kuishi ya Amour Salim Mohammed kwa dhamira ya kutenda kosa la wizi ndani humo, jambo ambalo ni kosa kisheria.