NA MARYAM HASSAN

KESI ya unyang’anyi wa kutumia nguvu inayomkabili mshitakiwa Samuel Masunga Ilanga umaarufu ‘Taiga’ (24) mkaazi wa Kisakasaka, inatarajiwa kusikilizwa tena Januari 11 mwakani.

Hatua hiyo imekuja kufuatia upande wa mashitaka kushindwa kuwasilisha mashahidi katika shauri hilo na kupelekea kuahirishwa.

Maamuzi ya kuahirishwa kwa shauri hilo, yametolewa na Hakimu Said Hemed Khalfan wa mahakama ya mkoa Mwera, ambapo awali upande wa mashitaka uliokuwa ukiwakilishwa na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor, kueleza kuwa hawajapokea shahidi.

Wakili huyo aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo na kupanga tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi, pamoja na kutoa tena hati za wito kwa mashahidi.

Hakimu Said alikubaliana na upande wa mashitaka na kupanga kusikiliza ushahidi Januari 11 mwakani.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, kosa la hilo ni kinyume na kifungu cha 280 cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.