BEIJING,CHINA

MAHAKAMA ya Hong Kong imempatia dhamana tajiri anayemiliki vyombo vya habari na mwanaharakati wa demokrasia Jimmy Lai.

Tajiri huyo alikuwa akishikiliwa kwa tuhuma za kukiuka sheria mpya ya usalama wa taifa ya China.

Kigogo huyo mwanzilishi wa gazeti la Apple Daily, linalofahamika kwa msimamo wake wa ukosoaji dhidi ya serikali ya China, amekuwa akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono vuguvugu za demokrasia za Hong Kong, akitumia mitandao ya kijamii na kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya kigeni.

Anakabiliwa na mashitaka kwa kutuhumiwa kushirikiana na vyombo vya kigeni chini ya sheria mpya ya usalama wa taifa.

Lai alikuwa kizuizini tangu alipokamatwa na kufunguliwa mashitaka Disemba 2 kwa kesi nyengine tofauti.

Mahakama ya Juu ya Hong Kong ilimpatia dhamana ya karibu dola milioni 1.3 za Kimarekani.

Ripoti zinasema kwamba atapigwa marufuku kutoka nyumbani kwake, kufanya mahojiano na vyombo vya habari, na kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii.