NDJAMENA, CHAD

MBUNGE na kiongozi wa zamani wa upinzani nchini Chad, Saleh Kebzabo, anakabiliwa na hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria, kulingana na barua kutoka kwa waziri wa sheria iliyowasilishwa bungeni nchini humo.

Kulingana na waraka huo, mpinzani huyo anadaiwa kuwa alitoa matamshi ya kuchochea chuki na kuhatarisha usalama wakati aliomba vijana wakulima wakati wa mkutano wa kisiasa kujipanga kulinda mashamba yao dhidi ya wafugaji.

Saleh Kebzabo alikutwa na hatia ya matamshi Disemba 22 mwaka 2019 yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu wa umma.

Hayo yamo katika barua iliyosainiwa na waziri wa Sheria wa Chad Disemba 28 mwaka 2020 na kupelekwa kwa spika wa bunge la nchi hiyo.

Endapo barua ya waziri huyo wa sheria itaidhinishwa na wabunge, utaratibu wa kufungua mashitaka utaanzishwa dhidi ya kiongozi wa zamani wa upinzani.

Saleh Kebzabo anashutumiwa ni kuzuru mkoa wa Tandjile Disemba 22, ambapo kulitokea mapigano kati ya wakulima na wafugaji baada ya uharibifu wa shamba.

Kiongozi huyo wa zamani wa upinzani aliwahimiza vijana kutafuta uwezo wa kulinda mashamba ya wazazi wao kutokana na uzembe wa viongozi. Maneno ambayo yalionekana na serikali kuwa ni hatari kwa amani.