NA MWAJUMA JUMA

TIMU za Kipanga na Polisi wametoka kifua mbele katika michezo yao ya ligi kuu ya Zanzibar iliyoendelea jana.

Timu hizo zilishuka katika viwanja viwili tofauti na kushinda bao 1-0 kila mmoja.

Kipanga walishuka katika dimba la Amaan kucheza na KVZ wakati Polisi walicheza na Hard Rock katika uwanja wa Gombani Pemba.

Katika mchezo wa Kipanga bao lao hilo la pekee liliwekwa kimiyani na mchezaji wake Abubakar Mkubwa Ali mnamo dakika ya 40.

Kwa upande wa timu ya Polisi ambao walicheza na Hard Rock bao lao hilo lilifungwa na mchezaji wao Ali Khatib.

Kipanga na KVZ walicheza wakiwa pungufu baada ya wachezaji wao kutolewa nje na mwamuzi Ali Ramadhan Kibo kwa vitendo vyao vya kufanya faulu mbaya.

Wachezaji hao ni Abdilahi Suleiman Kombo wa Kipanga ambae alimfanyia faulu Seif Said dakika ya 50 na Makarani Miruchu Makarani wa KVZ yeye alitolewa dakika ya 69 kwa kumkanyaga Neva Adelin.

Aidha katika uwanja wa Mao Zedong nako kulikuwa na mchezo kati ya Black Sailor na Zimamoto ambao ulimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1.

Ligi hiyo leo itaendelea tena kwa michezo miwili ambapo katika uwanja wa Amaan JKU itacheza na Malindi na Mao Zedong Chuoni watakutana na Mafunzo.