SEHEMU YA PILI
Na Mohamed Mzee Ali, SUZA.
Ahlan wasahalan. Bado nipo na wanahabari kuhakikisha kuwa tunaiva katika chungu kimoja, ili kuepuka makosa wanayoyafanya katika lugha ya Kiswahili.
Huwa nachukizwa na makosa hayo, lakini sitachoka kuwasaidia wenzangu hao na kutaka waelewe kuwa Kiswahili ni tunu kubwa kwao na wanapaswa kukikienzi, kukipenda na kukilinda.
Nikianza na kufuatilia makosa yanayofanywa na wanahabari wenzangu niliwasikia wakisema “ watu watano wamekamatwa katika msitu wa hifadhi wakichana mbao”.
Kiswahili fasaha na sahihi mbao haichanwi bali hupasuliwa . Hii inatokana na kwamba mbao zinatokana na magogo na kawaida magogo hupasuliwa na kupatikana mbao hizo.
Zamani kulikuwa na wimbo unaosema ‘seremala nipasulie mbao walia kweche msumeno”. Kwa maana hiyo usahihi wa kauli iliyotolewa na wanahabari hapo awali ni kusema”watu watano wamekamatwa katika msitu wa hifadhi wakipasua mbao”.
Nilimsikia mwanahabari mmoja akisema” kwa jina naitwa Fulani bin Fulani”. Si sahihi katika lugha ya Kiswahili kusema “kwa jina naitwa”, bali mwanahabari huyo alitakuwa kusema “ jina langu Fulani bin Fulani” au “naitwa Fulani bin Fulani”.
Aidha, nilimsikia mwanahabari mwengine akisema” kwa majina naitwa Fulani bin Fulani”. Si sahihi kusema hivyo hata kidogo. Usahihi ni kusema “ naitwa Fulani bin Fulani”.
Waswahili wengi siku hizi wanaiga tu kama kasuku wakiwemo wanahabari. Nilimsikia mwanahabari mmoja anasema “mwisho wa siku”. Katika Kiswahili hatuna “mwisho wa siku”. Kalima hii imechukuliwa katika Kiingereza ambayo ni “at the end of the day”.
Kiswahili kina hazina kubwa ya maneno na wala si kama wanavyodhani baadhi ya watu. Si vyema kutumia maneno ya wenzetu wakati ya kwetu yapo. Hivyo, si vyema kutumia “mwisho wa siku” na badala yake watumie “ hatimaye” au “mwishowe”.
Nimemsikia mtangazaji mmoja katika redio ya Taifa na wala sio FM akisema “Habari ya wewe”. Niliguna na kujisemea leo Mswahili anainanga lugha yake kama hivi? Si sahihi hata kidogo kutamka alivyosema.
Kauli kama hiyo ilinikumbusha nilipokuwa nasoma Khartoum miaka hiyo nilikuwa na wenzangu kutoka Uganda kama Hassan Delu, Suleiman Kisule, Suleiman Kasuja, Mudathir Ajotia nk. Hawa kwao ilikuwa ni kusema “habari ya wewe” au “habari ya kwako”.
Inashangaza kwa mzawa wa lugha tamu ya Kiswahili kusema hivyo kama walivyokuwa wakisema marafiki zangu wa Kiganda. Jee ! kuna shida gani kusema “ habari gani” au hata “habari yako”?.
Imekuwa ni jambo la kawaida sasa kusikia katika ZBC na redio nyengine kutamka majina ya pahala kwa mfumo wa Kiingereza. Kwa kweli inakirihisha.Mathalan, nilimsikia mtangazaji akitangaza tangazo la kifo kwa kusema” kilichotokea Mnazimmoja Hospitali”
Kutamka hivyo si sahihi katika lugha ya Kiswahili, bali alitakiwa aseme “kilichotokea Hospitali ya Mnazimmoja”. Sambamba na hilo kuna wanaosema “Bububu Skuli” badala ya “Skuli ya Bububu” na kadhalika.
Hivi sasa inaonekana kuzoeleka kuwasikia baadhi ya wanahabari wakitamka neno “mida” badala ya “muda”. Kwa mfano nilimsikia mtangazaji mmoja akisema” kunako mida ya saa sita tutakuwa tena hewani”.
Jamani Kiswahili kina wenyewe. Hakuna katika lugha hiyo matumizi ya neno “mida”. Neno linalotumika ni “muda” nalo ni kupima urefu wa wakati. Mathalan, mtihani huu utakuwa muda wa saa moja.
Mwengine kwenye FM fulani nilimsikia akisema “lisaa moja iliyobaki”. Nikajiuliza huyu mtu wa kabila gani na anazungumza lugha gani?. Kama Kiswahili hakisewmi hivyo, bali huwa tunasema” saa moja iliyobaki”.
Aidha, mtangazaji utamsikia akisema” zimebaki dakika 20 kutimia saa sita” au hivi sasa zimebaki dakika 20 kuendea saa sita”. Hiki si Kiswahili fasaha hata kidogo. Usahihi wa kutaja wakati ni kusema “ Hivi sasa ni saa sita kasoro dakika 20”.
Salaale! Makubwa hivi sasa watangazaji na waandishi wa habari wamefikia hadi kusema na kutumia neno’ kuboa”. Neno hili si la Kiswahili. Ni neno la Kiingereza “Boring” au “bore” au “boredom”.
Neno hili maana yake ni “kuchosha” kwa Kiswahili, lakini leo wanahabari wanasema “ anatuboa” badala ya “anatuchosha”. Hivi karibuni nilisoma gazeti la Mwanaspoti liliandika “Simba haipoi wala haiboi”. Hii ni hatari kwa ufisadi huu unaofanywa katika lugha ya Kiswahili.
Nililazimka kucheka. Kicheko si cha furaha, kwani sio kila kicheko ni cha furaha bali chengine huwa cha msiba na fadhaa. Nilimsikia mtangazaji mmoja akisema” nilikuwepo sipo”. Si sahihi kusema hivyo, bali alipaswa kusema “sikuwepo”.
Mkabala na kauli hiyo kuna wengine utawasikia wakisema “nilipofika nilimkuta hayupo”. Hapa alitakiwa kusema”nilipofika sikumkuta” au “nilipofika hayupo”.
Kadhalika nilimsikia mtangazaji mmoja wa FM moja akisema” alikuwepo hajui”. La haula! Kwanini asiseme “ alikuwa hajui”.
Mpaka nimefika umri huu au ni kwa kuwa ni mshamba, sijasikia walionitangulia wakisema “Mdada”. Mdada kwa lugha ya watangazaji wa siku hizi ni “dada”. Je kuna uzito gani kutamka “dada”. Utamsikia mtangazaji anasema” mdada wa kazi” badala wa “dada wa kazi”. Pia wengine husema “wamama” badala ya “mama”.
Nimesikia redio moja katika kipindi chake cha michezo mtangazaji anasema”Timu A na timu B zimesare”. Kiswahili hatusemi hivyo, bali alipaswa kusema “Timu A na Timu B zimetoka sare”.
Kwa upande wa matamshi ndio hatari. Wanahabari wengi wajui lugha yao na ni hatari sana kwa mustakbali wa Kiswahili. Mara kadhaa huwa nawasikia watangazaji na waandishi wakisema” salasini” badala ya “thalathini”, “samanini” badala ya “thamanini”.
Aidha, nimeona maneno yameandikwa katika magazeti kama “kudhorota” badala ya “kuzorota”,”hafla” badala ya “ghafla”. Mfano Makamu wa Pili wa Rais alifanya ziara ya “hafla” ZRB badala ya “ghafla”. Pia wengine kuandika “gafla” badala ya “ghafla”.
Neno “hafla” ni sherehe maalum. Mfano hafla ya kutunuku vyeti. Na “ghafla” ni tukio la kuzuka lisilotarajiwa. Mfano alifariki ghafla.
Kuna msamiati umezuka hivi karibuni katika tasnia ya michezo ambao ni “ amecheza sivyo ndivyo au ndivyo sivyo”. Kiswahili hakina msamiati huo bali ni kusema tu “amecheza sivyo”.
Maneno mengine niliyowasikia wanahabari wakivuruga ni “Haizuru”badala ya “haidhuru”, “haina zara” badala ya “haina dhara” na “amevaa zahabu” badala ya “amevaa dhahabu”.
Aidha , nilimsikia mtangazaji mmoja anasema” amejipamba kwa dhahabu kedekede”. Matamshi kama haya si sahihi bali alipaswa kusema” amejipamba kwa dhahabu kochokocho”.
Nimegundua kuwa waandishi na watangazaji wanafanya makosa makubwa katika matumizi ya maneno mawili ambayo ni “baada” na “badala”. Mara nyingi pahala pa badala hutumia baada na kinyume chake.
Mathalan, watangazaji wa mpira “ ameingia mchezaji Khamis Ndemla baada ya Joash Onyango”. Hapa alitakiwa atumie neno badala na sio baada.
Nimesoma gazeti moja litolewalo nchini limeandika”ngono ni haki ya faraha baina ya mke na mume”. Kauli kama hii ni makosa makubwa katika Kiswahili, bali alipaswa kuandika”Ngono ni haki ya faragha baina ya mke na mume”. Kwa maana hiyo Kiswahili ni faragha na wala si faraha.
Cha ajabu na ni ajabu. Nilimsikia mtangazaji mmoja anatamka “vyupa” ikiwa ni wingi wa “chupa”. Jee! Mtangazaji kama huyu anafaa kuwa mwanahabari wa kuuelimisha umma wakati uwezo wake wa lugha ni hafifu? .Hasara.
Matamshi mabovu kwa watangazaji hayakuishia kwa yaliyotangulia, bali nimewasikia pia wakitamka “zana” badala ya “dhana”, “zarau” badala ya “dharau”, “samani” badala ya “thamani” na kadhalika.
Cha kushangaza zaidi mwanahabari mmoja nilimsikia akitamka neno “hadisi” badala ya “hadithi” huku akiwa hana habari kabisa kuwa anakiuka maadili ya nchi kwa kutukana. Yote hayo ni kwa kuwa masikini hajui lugha. Lakini , alipaswa kuutumia msemo “kama huyajui uliza wenzio”.
Nilisoma gazeti moja nalo mhariri hakuwa makini kutoa makosa. Aliliacha neno “tene” badala ya “tena”. Maneno haya yana tafauti kubwa baina ya mbingu na ardhi. Kwa hakika neno “ tene” siliwezi kulitamka mbele za watu au kuliandika. Hivyo, wanahabari kaeni na wataalamu wa lugha kujifunza kwao.
Erevuka na shairi lifuatalo:
LUGHA BWANA !
Ukitaka ufaidi Lugha uwe ni mweledi
Usifanye ukaidi Tuliza yako fuadi
Maana hujijadidi Na neno likashitadi
Lugha bwana !
Karibuni mukale Musidhani kufaidi
Musidhani wali tele Kitoweo na kadidi
Ila jalasa ukale Ubarizi makusudi
Lugha bwana!
Na mchele upotele Usidhani wafaidi
Kwamba madukani tele Kumbe kwao ubaidi
Kauli hiyo kelele Njaa imepiga hodi
Lugha bwana!
Karibu kwetu Uzini Si kufanya ufisadi
Ni kijiji cha Uzini Ndio hasa makusudi
Si tendo la kishetani Adhabu yake ni hadi
Lugha bwana!
Kusema ‘nnavitako’ Si shutuma na inadi
Bali apita uliko Ufahamu makusudi
Kikae kwao ni huko Kusini ni yao jadi
Lugha bwana!
Hili neno kusokota Si kamba ilo jadidi
Wala sembe kusokota Kuwana kwa makusudi
Mwanamke kukamata Kinguvu na hana budi
Lugha bwana!
Pia kupiga ukotwa Nguvu sheti ishadidi
Mwanamke husokotwa Ridhaa kwake baidi
Ni kubaka kwa kuitwa Lugha iliyojadidi
Lugha bwana!
Mohamed Mzee Ali (Tere), SUZA.
Mwisho.