NA ABOUD MAHMOUD
KIKUNDI cha Mazoezi cha Kitambinoma Fitness Club kinatrajia kupokea wageni 120 kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania mwishoni mwa wiki hii.
Akizungumza na Zanzibar leo Katibu Mtendaji wa Kitambinoma, Mohammed Saleh Ameir, alisema wageni hao wanatoka vikundi vya mazoezi watashiriki mambo mbali mbali yalioandaliwa na wenyeji wao.
Katibu huyo alivitaja vikundi hivyo ni pamoja na Faita Jogging and Sports Club na Wakali Jogging Sports Club zote za Dar es Salaam,Uluguru Jogging and Sports Club ya Morogoro na Muungano Jogging Sports Club kutoka Dodoma.
Katibu huyo alisema kwamba mara baada ya kufika visiwani humu wageni hao watashirikiana na vikundi vyengine katika bonanza la kitaifa linalotarajiwa kufanyika Januari 1 mwakani.
Mohammed alisema siku ya pili watakua na mazoezi ya pamoja ambayo yatafanyika kwa kuzunguka Mji Mkongwe na baadae wataelekea shamba kwa ajili ya chakula cha mchana na kushiriki michezo ikiwemo kuvuta kamba, mpira wa mikono na michezo ya baharini na Januari 3 wageni hao wataondoka na kurudi nyumbani.
“Wageni wetu wakifika hapa tumeandaa shughuli mbali mbali ikiwemo kushiriki katika mazoezi ya kitaifa na baadae tutafanya mazoezi sisi na wageni wetu baadae tutaelekea shamba na tukimaliza siku inayofuata wataondoka na kurudi majumbani mwao,”alisema.
Katibu huyo alifahamisha kwamba lengo la wageni hao kufika visiwani humu ni kukuza ushirikiano wa michezo,kushiriki bonanza la kitaifa la mazoezi,kuziendeleza klabu zao mbali na kujenga afya pamoja na kutafuta njia mbadala kwa miradi ambayo itasaidia kuinua vikundi hivyo pamoja na kupata ajira.