KIGALI,RWANDA

ASILIMIA ya watoto waliodumaa chini ya umri wa miaka mitano imeshuka kutoka asilimia 38 hadi asilimia 33 katika miaka mitano iliyopita.

Takwimu kutoka Taasisi ya takwimu ya Kitaifa ya Rwanda zinaonyesha kuwa kushuka huko kungeweza kusababishwa na hatua za Serikali katika kuboresha chanjo na ubora wa utunzaji wa watoto, lishe na mazoea ya usafi kote nchini.

Waziri wa Afya Daniel Ngamije alisema ingawa hayo ni mafanikio kwa njia moja au nyengine, lakini maofisa wanauhakika kwamba nchi ina mambo mengi ya kufanya ili kumaliza udumavu.

“Ingawa hii ni hatua katika mwelekeo sahihi, imani yetu ni kwamba tunahitaji kufanya zaidi kutokomeza udumavu na maswala mengine yanayohusiana na afya ambayo wanawake na watoto bado wanakabiliwa nayo,” alisema wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.

Alisema utafiti wa idadi ya watu na Afya wa Rwanda, unaonyesha kwamba udumavu,utapiamlo sugu,viwango bado ni vya juu zaidi katika kaya masikini na za vijijini.

Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa asilimia 36 ya watoto katika maeneo ya vijijini walidumaa ikilinganishwa na asilimia 20 katika maeneo ya mijini.

Inaaminika inasababishwa na kutokula chakula cha kutosha au kula vyakula ambavyo havina virutubisho vya kukuza ukuaji,na maambukizo endelevu au magonjwa sugu ambayo husababisha ulaji duni wa virutubisho.

Ripoti hiyo iliunganisha kudumaa kwa kiwango cha elimu ya mama, ikisema kuwa watoto wa wanawake wasio na elimu walikuwa na uwezekano mkubwa wa kudumaa kuliko wale ambao mama zao walipata elimu.

Hatari ya kudumaa,uchunguzi tofauti wa kisayansi unasema, kwamba husababisha ukosefu wa maendeleo ya utambuzi na ufikiaji wa elimu, ikimaanisha kuwa watoto waliodumaa wana uwezo mdogo wa akili kutatua changamoto ngumu na kupata elimu.

Hatua hiyo kimsingi, inanyima uchumi wa watu wenye ubora ambao ni muhimu kufikia azma ya maendeleo ya nchi kuwa nchi ya kipato cha kati na kudumisha faida zake za kiuchumi.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Waziri Mkuu Edouard Ngirente alisema Serikali ilijitolea kuongeza juhudi mara mbili katika kuimarisha hatua muhimu za kimkakati katika sekta ya afya.

Utafiti huo, ambao ulivutia ushiriki wa rekodi na ulilenga zaidi wanawake na watoto, ulionyesha kuwa asilimia moja ya watoto walipotezwa mnamo 2020 ikilinganishwa na asilimia mbili 2015.

Kiwango cha watoto wenye uzito wa chini kilipungua kidogo kutoka asilimia tisa hadi asilimia nane katika kipindi hicho hicho.

Ngamije alisema kuwa vikwazo vya kitamaduni bado vinawazuia wanawake kupata huduma za afya, na hii inaweza kuzingatiwa kati ya wanawake wajawazito, ambao mara nyingi hushindwa kwenda kupata huduma katika kipindi cha kwanza cha ujauzito.

Ngamije pia alisisitiza hitaji la ubunifu katika huduma za afya wanazopewa wanawake na watoto kama vile kupima malaria na homa ya ini .

Alisema maswala ya udumavu ambayo yanaathiri watoto na wanawake, wakati mwengine huenda zaidi ya uwezo wao wa kiuchumi.

Kubadilisha mwenendo huo, Waziri Mkuu alionyesha kwamba Serikali ilijitolea kuimarisha mipango ya sekta nyingi iliyoanzishwa ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya. Serikali pia inaangalia kuimarisha zana mpya za ukusanyaji wa data na upanuzi wa huduma za afya karibu na raia, na pia kukuza miundombinu ya afya.