NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAM

BAADA kupoteza mchezo dhidi ya ihefu, uongozi wa timu ya KMC umesema umeelekeza nguvu zake katika mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania.

Mchezo huo utakaopigwa disemba 23 mwaka huu, utakuwa ni wa kurekebisha makosa iliyoyafanya na kupelekea kupokea kipigo cha 1 – 0 dhidi ya Ihefu FC zilipokutana katika uwanja wa Highlands mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumzia mchezo huo, Afisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala alisema kwa sasa wameweka kando mipango ya usajili hadi watakapomaliza hesabu mbele ya JKT Tanzania.

“Tunajua kamba ni wakati wa dirisha dogo la usajili ila ngoja tuweke kando kwanza masuala hayo mpaka pale ambapo tutamaliza mchezo wetu dhidi ya JKT Tanzania. Baada ya hapo tutaweka wazi mipango yetu kuhusu usajili na kila kitu kitakuwa sawa, mashabiki wazidi kutupa sapoti,” amesema.

Dirisha dogo la usajili kwa timu za ligi kuu Tanzania bara limefunguliwa Disemba 16 na linatarajiwa kufungwa Januari 16 mwaka ujao kipindi ambacho klabu hukitumia kuimarisha vikosi vyao.