NA MWANAJUMA MMANGA

KIKOSI cha Kuzuwia Magendo KMKM kimewakamata watu tisa akiwemo nahodha wa chombo walichokuwa wakisafirishia abiria  kwa kutumia bandari bubu huko Kizimkazi Wilaya ya Kusini Unguja.

Mkuu wa Zoni ya Kusini wa KMKM,  Luteni Hassan Hussein, akizungumza baada ya kukamatwa chombo hicho aina ya faiba alisema majira ya saa sita usiku  ikiwa na abiria tisa wakijiaandaa kuondoka kuelekea  Kunduchijijini  Dar es Salaam.

Luten Hussein aliwataja watu hao tisa wakiwemo manahonda wawili ni Wahidi Mzee Juma (46) na Msaidizi wake, Shaibu Khamis Hassan (38) wote wakiwa ni wakaazi wa kjijiji cha Kizimkazi.

Aliwataja abiria waliokuwemo katika chombo hicho, ni  Kelvin Stimisa Mikwe (29), mkaazi wa Dar es Salam, Shufaa Khamis Warget (25)mkaazi wa Ungujaukuu, Mwajuma Hamza Kalaumi (25) mkaazi wa Kizimkazi.

Wengine John Emanuel Ndimo (42) mkaazi wa Dar es Salam, Yahya Hamid Suleiman (32) mkaazi wa Kibuteni, Hidaya Kassim Mtawa (41) mkaazi wa Kizimkazi, Ibrahim Yahaya Hamid ambae ni mtoto mchanga na Getude Philbert Mlenge (38) mkaazi wa Dar ess Salama.

Alisema usafirishaji  abiria  kwa kutumia bandari zisizo rasmi umeongezeka, hivyo kikosi hicho kitaongeza doria katika maeneo hayo, ili kunusuru upotevu wa mapato na kulinda usalama watu.

Naye Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kusini, Hamida Mussa Khamis, amesema serikali imekuwa ikikemea wananchi kutumia bandari zisizo rasmi, kwani zinaweza kuleta maafa makubwa na kuhatarisha hata maisha ya binaadamu.

Hivyo aliwataka manahonda kuacha tabia kama hiyo kwani serikali imekuwa ikihitaji mapato yake ambayo yanatokana na ushuru wa badarini ambazo zilizo rasmi.