NA MWAJUMA JUMA

MAAFANDE wa kikosi cha kuzuia magendo KMKM wameendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Zanzibar, baada ya jana kufikisha pointi 16 kufuatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Malindi.

Mchezo huo ambao ni wa ligi kuu ya Zanzibar ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong A.

Miamba hiyo ilishambuliana kwa zamu kila mmoja akisaka bao la ushindi kila mmoja akitafuta bao la kuongoza.

Malindi huo ni mchezo wa pili mfululizo kufungwa ambapo mechi iliyopita walicheza na JKU na kufungwa bao 1-0.

Katika mchezo wao huo wa jana Malindi walitanguliwa kufungwa bao na kufanikiwa kusawazisha na kuwafanya waende mapumziko wakiwa sare ya kufungana bao 1-1.

KMKM katika mchezo huo mabao yake yalifungwa na Ibrahim Abdalla  dakika ya 18  na Ibrahim Khamis Khatib dakika ya 62 wakati Malindi bao lao lilifungwa na Mohammed Rajab Vuai dakika ya 24.

Mbali na mchezo huo pia katika uwanja wa Amaan kulikuwa na mchezo kati ya Polisi na Kipanga, ambao ulimalizika kwa sare ya bila ya mabao.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa kucheza mchezo mmoja ambao utakuwa Black Sailor na Mlandege utakaochezwa uwanja wa Amaan.