NA MOHAMED HAKIM
TIMU za mchezo wa mpira wa Magongo za KMKM na Jeshi zinatarajia kushiriki mashindano ya kuwania kombe la Mapinduzi yanayotarajia kuanza mapema mwezi ujao jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na muandishi wa habari hizi Katibu wa Chama cha Mpira wa Magongo Zanzibar, ambae ni msimamizi wa timu hizo Othman Manzi

Alisema katika mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika katika viwanja vya Lugalo jumla ya timu sita zitashiriki zikiwemo nne kutoka Tanzania Bara na mbili Zanzibar.

Manzi alisema awali Zanzibar ilitarajiwa kutoa timu tatu katika mashindano hayo, lakini kutokana na sababu mbali mbali, ambazo haziwezi kuepukika zimeifanya kuingiza timu mbili ambazo zitaungana na tano za Tanzania Bara.

“Tunatarajia kushiriki katika mashindano ya kuwania kombe la Mapinduzi kwa mchezo wa Magongo ambapo tulitaka twende na timu tatu kutoka Zanzibar, lakini kutokana na mambo mbali mbali imetulazimu kwenda na timu mbili na wenzetu Bara wataleta timu tano,”.

Alizitaja timu zitakazoshiriki ni KMKM na Jeshi kutoka Zanzibar na zile za Tanzania Bara ni Kidongo Chekundu, TPDF, Kalsa na moja kutoka mkoani Tanga pamoja na Dar es Salaam.Katibu huyo alifahamisha kwamba mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Januari 7 hadi 12 mwakani, ambapo alisema lengo la mashindano hayo ni kuyaenzi Mapinduzi matukufu ambayo yamewakomboa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

“Sababu za kuandaa mashindano hayo ni kuungana na wanamichezo wote nchini katika kuadhimisha siku hiyo muhimu kwetu ambayo imetuondoa katika ukoloni na kuwa huru katika nchi yetu,”alifahamisha.