NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa klabu ya Simba SC, Sven Vandenbroeck, amewataka mashabiki wa timu hiyo kutowalaumu wachezaji pale wanapofanya vibaya.
Simba juzi ilicheza mchezo wa kombe la Shirikisho la Azam (ASFA) dhidi ya kikosi cha Majimaji FC.
Kwenye mchezo huo wekundu hao wa msimbazi walifanikiwa kupata ushindi wa mabao 5-0 mchezo uliopigwa kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo Sven, alisema matokeo waliyo yapata wameyafurahia lakini aliwataka mashabiki kuacha kuwapa shutuma wachezaji wake.
Alisema wachezaji wake wanajituma sana na kwa muda tangu wamerejea nchini Nigeria wamekuwa wanasumbuliwa na majeruhu lakini wanacheza kwa moyo mmoja na kujituma.
“Sitaki kuona wachezaji wangu wakilaumiwa kwani wanajituma sana ukizingatia wamekuwa na majeruhi tangu wamerudi Nigeria , kama ni lawama naomba nibebeshwe mimi,” alisema
Sven alilazimika kutoa kuali hiyo kutokana na lawama zilizokuwa zikitolewa na mashabiki juu ya wachezaji wake kupoteza mchezo kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya FC Platinum mchezo klabu bingwa Afrika.